Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wagombea urais; JPM, Lissu, Membe katika jicho la Nyerere

1786f10addde9ab586f356a6993c0bcf Wagombea urais; JPM, Lissu, Membe katika jicho la Nyerere

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

*Mizania sita ya kuwapima

TUNAPOELEKEA uchaguzi mkuu Oktoba, vyama mbalimbali vimekwishateua na vingine vipo hatua za mwisho za uteuzi wa wagombea kuanzia ngazi ya urais, ubunge na hata udiwani.

Kutokana na umuhimu wa uchaguzi huu, napenda kutoa maoni yangu kuhusu wagombea urais watatu ambao kwa maoni yangu ndio wenye ushindani.

Kwa leo, ningependa kutumia fikra za Nyerere ambazo naona bado ni hai kuhusu Taifa hili na maendeleo kuchambua wagombea husika kama sehemu ya mjadala mpana wa namna ya kuwapima wagombea wetu!

Kwa sababu ya umuhimu, nitawaweka wagombea watatu ambao ni Dk John Magufuli, Bernad Membe na Tundu Lissu kuona wanaenea au kupungukiwa kiasi gani katika fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu uongozi wa juu wa nchi yetu.

NYERERE NA MUUNGANO

Fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu muungano bado zipo hai. Fikra zake kwamba tunahitaji mgombea Urais ambae tutakuwa na hakika ataulinda muungano wetu ni jambo muhimu tangu zamani, sasa na siku zote.

Ukitazama mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, msimamo wake na chama chake CCM kuhusu Muungano ni thabiti. Kwamba pamoja na uwepo wa changamoto za muungano kama ilivyo kwenye mataifa mengine yaliyopata kuungana kama Uingereza (United Kingdom), bado ufumbuzi wa changamoto hizo sio kugawana vipande au kuongeza mpasuko bali kuzishughulikia kwa umakini tena hatua kwa hatua kutokana na unyeti wake.

Kwa upande wa Tundu Lissu na Benard Membe, misimamo yao kwa maneno na matendo yao na vyama vyao kuhusu muungano, bado kwa sehemu kubwa wanatumia suala hili kutafuta zaidi ushindi wa kisiasa ambalo ni tukio kuliko hatima ya muungano wenyewe.

Sauti zao zipo chini sana kuhusu uimara wa Muungano. Haiwasumbui muungano kuyumba kama itawasaidia kushinda uchaguzi huu 2020.

Tundu Lissu ameshasisitiza mara kadhaa kwa maneno ndani na nje ya Bunge kuwa si muumini wa Muungano! Kimsingi, msimamo wa Lissu kuhusu haja ya kuuvunja Muungano ni mkali zaidi ya hata ya chama chake!

Kwa upande wa Bernad Membe, hana namna zaidi ya kusimamia msimamo wa chama chake ACT ambao katika hili mwamuzi ni mgombea urais Zanzibar, Maalim Seif kuliko yeyote ndani ya chama hicho.

Msimamo wa Maalim Seif kuhusu Muungano umekuwa wa mashaka kwa kipindi chote tangu anze harakati kusaka urais zanzibar. Pengine hii ni moja ya karata muhimu kwa uhalali wake kisiasa Zanzibar.

Ingawa kutokana na ukomavu wake kisiasa ni adimu kutamka hadharani, lakini kitendo cha wafuasi wake kushabikia hadharani hivi karibuni kuwa wanataka Zanzibar yao, mbele yake yeye Maalim Seif, Bernad Membe na Zitto Kabwe, bila kuonywa, inatuma ujumbe mzito kuhusu imani na msimamo wa chama hiki kuwa wagombea wake wote na chama kama taasisi sio waumini wa Muungano!

Ni maoni yangu kwamba vyama hivi viwili, ACT na CHADEMA havioni sababu ya Muungano kwa misingi ya faida za kisiasa. Kwamba Chadema kushindwa kupenya kwenye siasa za Zanzibar imefanya wasione sababu ya Zanzibar na ACT ambayo bado imeshindwa kupenya siasa za bara, haioni sana sababu ya Tanganyika!

Lakini jambo muhimu ifahamike kwamba Muungano huu umeshavuka hatua ya kuunganishwa nchi mbili bali sasa ni Muungano wa watu wa nchi hizo mbili (sisemi dola). Hivyo ni maoni yangu kwamba Lissu na Membe sio wagombea salama kwa Muungano huu.

NYERERE NA UFISADI

Fikra za Mwalimu Nyerere kuwa rushwa ni adui wa haki na kwamba Serikali legelege haiwezi kukusanya kodi bado ni fikra sahihi na hai kwa maoni yangu.

Jambo moja ni wazi kwamba ingawa hoja hii ilikuwa turufu ya upinzani kwa miongo kadhaa baada ya Mwalimu Nyerere, lakini upinzani umeipa kisogo kabisa hoja hii baada ya JPM kuibeba kwa vitendo.

Ingawa kansa ya rushwa na ufisadi ni tatizo kubwa katika nchi zetu zinazoendelea, wagombea hawa; Tundu Lissu na Bernad Membe ama sauti yao ni ndogo sana au hawasikiki kabisa kuhusu eneo hili.

Zaidi wamesikika mara kadhaa wakitetea ufisadi kwa visingizio vya haki za binadamu katika kupambana na mafisadi.

Wagombea kuisusa agenda ya ufisadi ni kujinyonga kisiasa kwenye dunia ya wazalendo hata kama kuicha kwao kunaweza kuwanufaisha kupitia wafanyabiashara, taasisi, makampuni na hata mataifa waathirika wa operesheni ya JPM dhidi ya mafisadi ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa JPM, uwezo wake kumudu vita hii bila kujali chama wala uswahiba, imeakisi fikra za Nyerere kwa kiasi kikubwa. Mwalimu alipata kusema kwamba Rais awe na uwezo wa kuwaambia marafuiki zake kwamba “Mimi sikuchaguliwa na wananchi ili kuja kupageuza kuwa pango wa la walanguzi”. Magufuli amethibitisha uwezo huo kwa vitendo kwa

Rekodi za ndani kama kufuta bandari bubu zaidi ya 400, ufisadi Mamlaka ya Mapato (TRA), bandarini, mashirika na taasisi za umma zinaonesha alivyo makini katika kupambana na ufisadi.

Hii ni sambamba na ongezeko la makusanyo kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 mpaka zaidi shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi.

Rekodi ya Tanzania kuwa nchi ya 28 duniani kwa usimamizi thabiti wa matumizi ya Umma (WEF 2019), na ile ya imani ya watanzania kuwa Serikali yao inapambana na rushwa kufikia asilimia 78 mwaka 2019 kulinganisha na asilimia13 mwaka 2015 (Global Africa Barometer), ni kielelezo halisi kwamba JPM amefanikiwa kuakisi wosia wa Mwalimu Nyerere kuhusu kupambana na rushwa na ufisadi kuliko washindani wake kwa mbali sana.

NYERERE KUHUSU UMASKINI

Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba tunahitaji Rais anayeguswa na umasikini wa wananchi. Kwamba tukimskiliza kwa maneno na matendo tuamini kweli anasumbuka na umasikini wa wananchi hasa wanyonge.

Ukitazama Tundu Lissu na Bernad Membe wanazungumza hoja hii ingawa hawana majibu ya hakika kuhusu ufumbuzi kwa maoni yangu. Wote wana mtazamo kwamba JPM anajenga uchumi wa vitu badala ya watu kama karata yao.

JPM amewazidi sana eneo hili hasa kwanza, kwa kuzingatia ukweli ulio wazi kwamba umasikini wa huduma umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na utekelezaji wa miradi mingi ya afya, elimu, maji, umeme vijijini na barabara na madaraja vijijini.

Hatua hii kwa hakika imeongeza uwezo wa raia kuzalisha na kupunguza gharama za kufuata huduma mbali ambazo zilikuwa zaidi ya gharama ya huduma yenyewe huko tulikotoka.

Hii ni sambamba na mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kulinganisha na tulikotoka, ambapo fedha za dawa na vifaa tiba zilikuwa shilingi bilioni 35 kwa mwaka kulinganisha na shilingi bilioni 269 sasa, sawa na ongezeko la asilimia 700.

Mapinduzi makubwa ya ujenzi zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 14 mwaka 2014 mpaka asilimia saba (WHO ), moja ya sababu ni upatikanaji karibu wa huduma za afya hivyo kupunguza muda wa mgonjwa kukaa na malaria kabla ya matibabu na hivyo kupunguza kasi ya maambukizi.

Upatikanaji umeme vijijini mwaka 2010 ilikuwa vijiji 560, mwaka 2015 vijiji 2018 sawa na ongezeko la vijiji 1458 wakati mwaka 2020 vimefika vijiji 9,300 sawa na ongezeko la vijiji zaidi ya 7,000.

Upatikanaji wa maji vijijini mwaka 2010 ulikuwa asilimia 47, mwaka 2015 ikapungua kufikia asilimia 46 wakati mwaka 2020 upatikanaji umefikia asilimia 73. Yote hii ni ushahidi wa maendeleo ya watu kwani huduma hizo zinahusu watu tena zaidi vijijini.

Kwa upande mwingine, kinachoitwa maendeleo ya vitu wakosoaji wanarejea zaidi maamuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa, kufufua Shirika la ndege na mradi mkubwa wa kufua umeme wa bwawa la Nyerere.

Katika hili la ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi, JPM anawazidi kwa sababu ilikuwa hoja ya upinzani miaka yote kwa nini nchi yetu ikose reli, meli za uhakika na shirika la ndege kiasi cha kushindwa na nchi ndogo kama Rwanda.

Zaidi ya kuwa hoja ya upinzani miaka mingi, pia ripoti za tafiti kama Poverty & Human Development ya mwaka 2008, ilionesha kwamba kwa nafasi ya Tanzania kijiografia, ikiwekeza vyema katika sekta ya uchukuzi, sekta hiyo itachangia uchumi kuliko sekta yoyote.

Hivyo, kwenye mradi wa wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2100, zaidi ya umeme wote unaozalishwa sasa wa megawati 1600 ni mradi muhimu kwa kuwa msingi kwenye ujenzi wa viwanda kwa sababu itafanya Taifa kuwa na nishati ya uhakika na bei nafuu.

Umeme wa maji ni gharama nafuu zaidi kwa sababu gharama ya uendeshaji ni chini kuliko aina zingine. Hakuna nchi duniani imeendelea kwa viwanda bila umeme wa uhakika.

Sasa upinzani hausikiki ukizungumzia uendelezaji miradi hii mikubwa, ikimaanisha kwamba wakipewa dola wataifuta hivyo kuwa hasara kwa fedha iliyokwishatumika. Mgombea na chama chenye mtazamo sahihi kuhusu maendeleo ilikuwa lazma kiseme kitaendelezaje miradi hii.

JPM ameitoa nchi hii kwenye zama za kukodi ndege kwa dola milioni 43 mwaka 2012, ikafanya kazi robo ya muda wa mkataba lakin robo tatu ya muda ipo gereji (CAG report 2020), leo dola milioni 32 ananunua ndege mpya bombardier.

Nchi inanunua ndege11, kutoka ndege moja. Ni wazi kwamba haya ni mapinduzi ambayo watanzania walitamani kusikia upinzani ukisema kwa sauti utaendelezaje.

NYERERE NA UFISADI MIKATABA YA UMEME

Mwalimu Nyerere amepata kunukuliwa kwenye ripoti ya Transparency International akikosoa vikali mkataba kati ya Serikali na IPTL huku akibainisha wazi kuwa mkataba ule ulikuwa mbaya kuliko ukoloni na kuirushia lawama Taifa la Malaysia ambalo ndio kampuni yake ya Merchma ilimiliki asilimia 70 ya IPTL.

Upinzani pia ulikuwa juu ukipinga mikataba hiyo mibovu kwa miaka yote. Baada ya JPM kuchukua hatua, upinzani kwa maana ya Tundu Lissu na hata Benard Membe ama wanapinga maamuzi ya Serikali kuvunja mikataba hiyo au wanatetea kampuni hizo kuwa zimeonewa!

Tangu awamu ya pili, tatu na nne, Tanesco ilikuwa shirika linalotafuna uchumi wa Taifa hili hata kufikia kupewa ruzuku ya shilingi bilioni 400 kwa mwaka. Mgawo wa umeme na umeme hafifu ilikuwa kawaida ya Taifa hili.

Lakini leo Tanesco inaendeshwa bila ruzuku, nguzo za umeme zilizokuwa zinanunuliwa nje kwa dola, leo zinazalishwa nchini, Tanesco iliyosababisha Mkapa alete kampuni ya kimenejiment kutoka Afrika kusini kuja kuendesha, Net Group Solutions, leo inajiendesha kwa faida.

Tanesco ambayo ilipelekea hata Bunge na CAG kutoa mapendekezo ya kuligawanya kwenye mashirika matatu kupunguza hasara na kuongeza ufanisi, leo chini ya JPM, hakuna kuligawa wala kuleta kampuni ya kimenejiment kuliendesha, na sasa linajiendesha bila ruzuku.

Uamuzi wa kijasiri wa JPM kufuta mikataba ya kifisadi kama Symbion, mikataba inayohusisha vigogo wa Mataifa makubwa duniani ili kuondolea taifa mzigo, inaakisi picha halisi ya fikra za Mwalimu Nyerere.

Ni tofauti sana na Tundu Lissu ambaye yeye ameamua kwa muda mrefu kuwa mtetezi wa mafisadi hawa wa kimataifa kwa mgongo wa ati taaluma ya kisheria, ati sheria zinavunjwa na mara haki za binadamu.

Mwalimu Nyerere alipata kumtimua nchini mgiriki aliyetamba kuiweka Serikali mfukoni bila kujali haki za binadamu kwa heshima ya Taifa.

NYERERE NA MADINI YETU

Msimamo wa Nyerere kuhusu rasilimali za nchi ni usawa katika kunufaika na rasilimali hizo.

Baada ya kilio cha muda mrefu kutaka taifa lipate linachostahili kuhusu raslimali zake za madini huku zikirejewa kauli za Nyerere, JPM baada ya kuingia madarakani, alianza kutekeleza kwa vitendo.

Ni kweli kama kuna sekta imekutana na makali ya JPM ni sekta ya madini. Zimetungwa sheria na mbinu nyingi kudhibiti uporaji madini ikiwemo kujenga ukuta wa Merarani kudhibiti madini ya Tanzanite. Katika hili, JPM ameakisi msimamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu madini.

Kwa upande wa upinzani, Tundu Lissu kama mwanasiasa mwenye mrengo wa kale kuhusu dhana ya upinzani kwamba "Upinzani ni kupinga kila kitu", amejikuta akigeuka mtetezi wa kampuni za madini ili tu kumpinga JPM.

Kwa upande wa Membe, eneo la rasilimali kufaidisha nchi hajawa na msimamo bayana na zaidi imebaki akisomeka kama mtetezi zaidi wa wawekezaji huku sauti yake kuhusu maslahi ya nchi kwenye uwekezaji ikiwa chini mno.

Kimsingi Membe anasomeka kama mwanasiasa asiyeamini katika kuzikaba kampuni za madini na badala yake anasomeka kama mwanasiasa anayeamini kuwa mambo yangeweza kuendelea kama zamani! Pengine anafanya hivyo kutafuta uungwaji mkono wa mataifa makubwa yenye mkono wake katika kampuni zilizobanwa na JPM.

Hivyo katika eneo la madini, bado JPM amewaacha mbali Lissu na Membe katika kufanyia kazi fikra alizokuwa nazo Mwalimu Nyerere. Katika hili, JPM anazidi kupata turufu zaidi kwani tofauti na utabiri wa Chadema na ACT kuwa mbinyo wa JPM kwa kampuni za madini ungesambaratisha sekta hiyo na hata kushuka mauzo ya nje ya nchi (export), ambayo kwa sehemu kubwa ni dhahabu, takwimu zimeonesha tofauti.

Kwamba wakati mwaka 2015 mauzo ya dhahabu nje ilikuwa dola bilioni 1.3, mwaka 2019 mauzo ya dhahabu yalifikia dola bilioni 2.14 sawa na ongezeko la asilimia 65 (BoT reports 2016,2020).

NYERERE NA UTU NI KAZI

Moja ya misingi ambayo Mwalimu Nyerere alisisitiza katika hotuba zake kuhusu maendeleo ni kwamba ingawa watu wengi wanatamani maendeleo lakin wengi hawazungumzii kanuni ya msingi ya maendeleo ambayo ni kazi.

Kwa upande wa JPM, amefanikiwa sana kujipambanua tangu mwanzo kuwa kazi ndio msingi wa maendeleo ya mwanadamu katika ngazi yoyote.

Ndio msingi wa kaulimbiu yake Hapa Kazi Tu. Katika hili amefanikiwa sana kumuakisi Mwalimu Nyerere hasa katika mazingira ambayo Taifa lilikuwa limekwama katika mtindo wa maisha ya mishenitauni, kwamba watu walianza kuishi kwa ujanjaujanja kutokana na mfumo wa uchumi uliokuwa unavuja kwa ufisadi.

Kwa upande wa Lissu na Membe, wao katika hili sauti yao ipo chini sana. Pengine wanaogopa kupoteza kura za walioamini katika maisha ya mishemishe au mishenitauni. Hivyo katika hili bado wameshindwa kuakisi fikra sahihi za Mwalimu Nyerere kwamba maendeleo ni kazi.

Kwa kiasi kikubwa mtazamo wa Lissu na Membe sio kujenga Taifa la wazalishaji bali wachuuzi, ndio maana wanakosoa hata ujenzi wa miundombinu ya uchumi wakilinganisha na matumizi ya kawaida ambayo yangefanya taifa liendelee kuwa tegemezi.

Huwezi kujenga uchumi bila miundombinu ya umeme na usafiri. Huwezi kutengeneza ajira bila kuwa na msingi wa viwanda ambao huanza kwa miundombinu.

Hivyo kwa ujumla, vigezo hivyo sita hivyo, vinaakisi wazi kuwa katika wagombea tulionao katika uchaguzi huu ulio mbele yetu, bado JPM ndio muumini wa fikra sahihi za Mwalimu Nyerere kuhusu Tanzania na maendeleo ya mwanadamu.

Columnist: habarileo.co.tz