Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wafugaji zitumieni ranchi, kufuga kisasa na kibiashara

5011bd0be16fe9de969123117c6f73d2.jpeg Wafugaji zitumieni ranchi, kufuga kisasa na kibiashara

Thu, 25 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MIGOGORO ya wakulima na wafugaji ni eneo ambalo limekuwa lina changamoto za muda mrefu nchini na mazao mbalimbali ya wakulima yakiharibiwa kutokana na ufugaji usiokuwa wenye tija.

Kutokana na changamoto hizo, wakulima wamekuwa wakiwalalamikia wafugaji, hivyo hivyo na upande huo unaolalamikiwa bila kujali ukiendelea kufuga mifugo yao katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye mazao ya wakulima jambo lililosabasha maeneo mengine kuwapo kwa matukio ya mapigano.

Katika juhudi za kuhakikisha ufugaji unakuwa wenye tija na uendelevu zaidi, Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) hivi karibuni imepangua tozo kwa mikataba mipya ya upangishaji katika vitalu vya uwekezaji vya kampuni hiyo, jambo litakalosaidia uboreshaji wa sekta ya mifugo kwa ujumla.

Sio kwamba kupunguzwa kwa tozo hiyo hadi kufikia Sh 3,500 kwa ekari moja kwa mwaka itasaidia tu kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji, lakini pia ni eneo mojawapo litakazosaidia kuifanya sekta ya ufugaji kuwa bora na ya kisasa zaidi.

Aidha, mpango huo utasaidia pia kuwawezesha wafugaji wadogo wanaohitaji kufuga kisasa na kibiashara ili kuondokana na ufugaji wa kienyeji na usiokuwa na tija.

Haina ubishi kuwa bado wapo wafugaji nchini tena wenye mifugo mingi ambao bado wanahama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya kutafuta chakula cha mifugo yao, jambo ambalo katika harakati hizo uharibifu wa aina moja hadi nyingine unaweza kutokea.

Inawezekana mlinzi wa mifugo hiyo akapata athari za kiafya ambazo zinaweza kusababisha kuambukiza katika familia husika lakini pia wanyama wakifugwa kiholela bila kujali lishe bora wanayoweza kuathiri biashara ya mifugo kitaifa na kimataifa kwa ujumla.

Kadhalika ufugaji wa aina hiyo usiokuwa na malengo unaweza kusababisha kuwapo kwa maambukizi ya magonjwa baina ya wanyama au hata kwa binadamu kwa kuwa ni ufugaji wa kuzunguka maeneo mbalimbali.

Hivyo, kwa punguzo la tozo hiyo, wafugaji wanaweza kujiunga katika vikundi na kuunganisha mifugo yao na kupata ardhi katika ranchi, jambo litakalosaidia kuwa na uhakika wa lishe kwa mifugo yao kwa wakati husika na hata kuona fahari ya kufuga kibiashara kwa kutanua soko la ndani na hata la nje.

Ikumbukwe kuwa inaelezwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kwa kuwa na mifugo mingi ambayo kwa namna moja hadi nyingine ikitumika vyema ni eneo ambalo pia linaongeza pato kwa wafugaji wenyewe na hata kwa taifa kwa ujumla.

Kutokana na kushuka kwa tozo hiyo haitegemewi kuendelea kuwapo kwa makundi ya wanyama ambao bado watakuwa wakizungushwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya kutafuta malisho, la hasha ni wakati muhimu kwa wafugaji kila mmoja kuanza kutafuta namna ya kuingia mkataba na ranchi ili kufuga kisasa na kibiashara zaidi.

Ikumbukwe kuwa kabla ya tozo hizo kushushwa hapo nyuma kulikuwa na tozo ya Sh 3,000 na 5,000 hadi 7,000 kwa ekari moja kwa mwaka, ambapo wafugaji wakubwa ndio waliokuwa na uwezo wakupata maeneo hayo, lakini kwa sasa kila Mtanzania mwenye nia ya kufuga kisasa na kibiashara anamudu kuchukua eneo hata kwa kuungana.

Kwa wafugaji kuamua na kuanza kufuga kisasa ni eneo ambalo linaweza kuongeza ajira nyingi kwa Watanzania, lakini pia kuhakikisha Tanzania inaimarika kwenye uchumi wa viwanda ambao kwa kiwango kikubwa unategemea malighafi mbalimbali zikiwamo za mifugo.

Columnist: habarileo.co.tz