Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wafipa na mila za kurithiana

Wafipa Wafipa na mila za kurithiana

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MILA na desturi za makabila mbalimbali hupaswa kuenziwa na kuendelezwa na jamii husika, hasa tamaduni nzuri na kutokomeza zile mbaya, ambapo kwa pamoja leo tunaangazia jamii ya Wafipa, waishio katika mkoa wa Rukwa.

Watu wengi wamekwishaandika kuhusu utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali wakiwemo Wafipa, hata hivyo, bado yapo mengi hayajaandikwa na yaliyoandikwa yameandikwa na wageni.

Wafipa ndilo kabila kubwa kuliko mengine yaliyopo katika mkoa wa Rukwa. Makabila mengine ni Wamambwe, Wanyamangwa na Wakwa ambayo yameishi mkoani humo kwa miaka mingi huku pia ikielezwa kuwa yote haya chimbuko lake ni kabila la Wafipa.

Katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunajaribu kuangazia, kwa kifupi, kuhusu masuala ya utamaduni, imani, ndoa, na masuala ya misiba na urithi.

Kama ilivyo kwa makabila mengine nchini, Wafipa wana utajiri wa historia ya utamaduni, mila na desturi za kipekee zinazowatofautisha na makabila mengine.

Kiasili Wafipa walikuwa wahunzi mahiri wa zana za kilimo na shughuli kuu za uchumi kwa jamii hii ni kilimo na ufugaji. Baadhi hujishughulisha na uvuvi na uwindaji.

Chakula kikuu cha Wafipa kinaelezwa kuwa ni ugali wa ulezi na maharage na mwanamke hakuruhusiwa kula mayai wala nyama ya kuku. Waliamini kuwa iwapo kama mwanamke angekula nyama ya kuku na mayai wakati wa kujifungua angepata matatizo makubwa kwa kuwa mtoto wakati wa ujauzito wake angekuwa mnene sana.

Lakini mwanamke baada ya kujifungua, licha ya kulishwa vyakula vya aina mbalimbali ili kuhakikisha afya yake inaimarika haraka, pia aliruhusiwa kwa wakati huo kunywa mchuzi wa kuku.

Anapochinjwa kuku, firigisi iliandaliwa rasmi kwa ajili ya baba mwenye nyumba kwa mgeni aliyesababisha kuku kuchinjwa na si vinginevyo. Kadhalika pombe iliyotengenezwa kwa ulezi maarufu ‘kimpumu’ ni kinywaji kilichothaminiwa sana na kupendwa.

Pombe hiyo ilikuwa ikinywewa kwa mirija na watu wa rika zote wakiwemo watoto wakati wa jioni na hasa baada ya shughuli za kilimo. Pombe hiyo pia ilitumika katika sherehe za harusi na misiba.

Kuhusu mavazi ya asili ya Wafipa, machapisho mbalimbali yanabainisha kuwa wanaume walikuwa wakivaa kipande cha ngozi ya ng’ombe au mbuzi kwa ajili ya kujisitiri sehemu za siri tu huku mwili mwingine ukibaki wazi.

Kwa upande wa wanawake walivaa vipande vya ngozi za wanyama kujisitiri sehemu zao za siri na kufunika matiti. Kadhalika walivaa shanga kiunoni na shingoni. Baadaye walianza kuvaa vipande vya nguo, hususan kaniki ambazo zilitengenezwa na jirani zao wa kabila la Wakwa waishio katika Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga kwa sasa.

Inaelezwa kuwa jamii ya Wakwa enzi hizo walikuwa wakulima hodari wa pamba ambapo baadaye walivumbua kinu cha kuchambua nyuzi za pamba kisha wakaanzisha ‘kiwanda’ cha kutengeneza nguo za pamba.

IMANI

Wafipa katika imani ya dini yao ya asili waliamini kwamba kuna Mungu ambaye anaishi juu mbinguni. Hii ni kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, na walimtambua Mungu huyu kwa majina kadha wa kadha kama vile ‘Leza’ kwa maana ya Mungu muumbaji.

Hii inajidhihirisha hata leo ambapo Wafipa wanamtaja Mungu Leza katika salamu zao. Kwa mfano wanapokutana wanasalimiana, “Postuta” ikimaanisha, “Una uzima ndani mwako?” na anayesalimiwa anajibu “Tata Itu Kalesa” maana yake ikiwa “Ndio, ninao uzima shauri ya Mungu Baba”.

Neno “Lesa” katika Kalesa ndilo linaloonesha jina Leza ambalo kwa sasa Z inatamkika kama S kuonesha jinsi tangu zamani walivyokuwa wakimtukuza Mungu wa Mbinguni.

Wafipa pia walimtambua Mungu wa mbinguni kwa jina la ‘Ndaka’ ambayo maana yake ni jua wakimaanisha kuwa ana nguvu kama jua.

Katika salamu pia mtu anaweza kujibu kwa kusema “Ndakaitu kalesa” akimaanisha kuwa “Niko mzima kwa shauri ya Mungu baba ambaye ni jua”. Na pia walimtambua Mungu kama ‘Umwene Nkulu’ kwamba ni mfalme wa wafalme wote.

HARUSI NA NDOA

Kama ilivyo kwa jamii nyingi, suala la ndoa kwa Wafipa linaheshimiwa. Ndoa hufanywa kwa kufuata taratibu za kimila. Kijana akifikia umri wa kuoa hushauriwa na wazazi wake kuhusu ukoo mzuri wa kutafuta mke.

Masuala yanayozingatiwa ni pamoja na kuchapa kazi, kuepuka koo zenye magonjwa na zisizokuwa na uzao. Kijana akishaoa hukaa karibu na wazazi kwa muda wa mwaka mmoja ili kujifunza jinsi ya kuendesha familia baada ya hapo huweza kujenga sehemu nyingine.

Utii kwa wakubwa ulisisitizwa sana kwa kuwa Mfipa alijengwa kuamini pia kwamba watu wakubwa kwa umri ni wawakilishi wa Lesa hapa duniani.

Pia walikuwa na sherehe kubwa mbili kwa mwaka, kabla ya kunyesha kwa mvua na baada ya mavuno ambapo walitoa sadaka ya mazao na pombe kwa Lesa ikiwa ni dalili ya kumtolea heshima na kumshukuru kwa neema ya mvua na mavuno mazuri aliyowajalia.

MISIBA NA URITHI

Kwa Wafipa kuonesha huzuni ya kufiwa, wote hupaswa kunyoa nywele zote kichwani na hili hufanyika kwa ndugu wote wa marehemu, kisha baada ya kumaliza msiba ilikuwa ni shurti kwenda kuoga maji ya mtoni.

Wakati wa maombolezo, waombolezaji hawakuoga, na hivyo baada ya kunyolewa nywele huenda kuoga au kunawa, ikiwa ni njia ya kujitakasa na pepo wabaya ambao wanaweza kuleta kifo.

Baada ya hapo kinatolewa chakula cha jioni, ‘i chiloosha’. Mkuu wa ukoo wa upande wa baba alikula kuku na kwa heshima sana alipewa firigisi ‘i’inkushu’ ambayo kwa Wafipa ni nyama ya heshima sana, na kwa kawaida hailiwi na wote. Naye humega na kugawa kidogo kidogo kwa baadhi ya wanaukoo.

Mjumbe au mkuu wa kijiji naye alichinjiwa kuku, ikiwa ina maana kuku wa kusafisha mji, na huyo kuku aliliwa na jumbe pamoja na wazee wengine wa kijiji ili kukisafisha hicho kijiji.

Mtu haruhusiwi kuchukua mifupa ya nyama ya msibani na hii ni kwa tahadhari ya mtu kufanyia uchawi kama Wafipa wanavyoamini. Baadaye watu wote hutangaziwa mrithi ni nani, hasa baada ya kikao cha wanandugu kukaa, na hapo hutolewa chakula na baada ya chakula watu huondoka.

Moto wa msibani pia huzimwa siku hiyo na mzimaji hujulikana kama ‘Kayeemba’, na majivu yote hutupwa chooni. Kuzimwa kwa moto huo huonesha kwamba msiba umeisha.

Katika kumaliza msiba kwa Wafipa, jambo la kwanza ambalo mpaka sasa linafanyika ni kuitishwa kwa mkutano wa awali wa wanandugu ukiongozwa na Mzee wa boma au wakuu wa ukoo wa kila upande mume na mke, kwa pamoja hujadili nani atamrithi marehemu, ‘akakwiliya’.

Mkutano huu wa ‘akakwiliya’ hufanyika kwa siri kidogo ili wanandugu wawe huru kujadili nani hasa anastahili kukabidhiwa jukumu hilo la urithi, ambapo baada ya mkutano huo wa kificho hatimaye hufuatiwa na mkutano wa hadharani ambao kila mtu anayetaka anaweza kuhudhuria.

Wanaoweza kurithiana ni watoto wa baba mkubwa na mdogo, watoto wa mama mkubwa na mdogo, Binamu na pia mtoto anaweza kumrithi baba yake kama ndugu wa baba huyo wameisha, hata hivyo urithi huo ni wa kusaidia kumtunza mjane au mgane na si kuchukua uhusika wa kuwa mke na mume.

Pia mjukuu anaweza kumrithi babu au bibi kuwa mume wake au mke wake (kama cheo cha kupewa tu).

Lakini cha kushangaza zaidi katika mila hii ya kurithiana: msichana anaweza kumrithi shangazi yake na mume wa shangazi akawa mume wake, ambapo zamani ilikuwa hata shangazi akiwa hai, mfano akiumwa kwa muda mrefu msichana (mpwa) wa shangazi alipelekwa kwa shangazi yake ili kumsaidia katika kazi zote hata kulala na baba (mume wa shangazi) ili kumzuia mumewe huyo asilale nje ya ndoa.

Zamani mrithi hukabidhiwa mali zote za marehemu, hasa mume, ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake wote aliokuwa nao na wao kumpa heshima yake kama baba mpya.

Kama mtoto wa kwanza katika familia ndiye aliyekufa basi urithi huenda upande wa baba na anapokufa mtoto mwingine inakuwa zamu ya upande wa mama wa marehemu.

Baada ya uamuzi kufikiwa wa nani atakuwa mrithi, basi akina mama walioko kwenye chumba cha maombolezo hupelekewa taarifa na wakiafiki huitikia kwa kusema “mwandila ta” na kama hawakubaliani nao hupewa fursa ya kutoa mawazo yao.

Endapo akina mama wamekubaliana na uteuzi wa mrithi, basi mama mmoja huchaguliwa kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala, ambapo kama mrithi ametoka upande wa kiumeni basi mfagiaji huwa wa upande wa kikeni na lazima pafagiliwe siku hiyo hiyo.

Kwa Wafipa vumbi linalotolewa baada ya kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala linamwagwa chooni. Hii ni kwa ajili ya tahadhari ya mchawi kuchukua vumbi hiyo na kufanyia uchawi kama inavyoaminika.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz