Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wachezaji wapewe muda wa kutosha kupumzika

Sopu Azam Fc.jpeg Wachezaji wapewe muda wa kutosha kupumzika

Tue, 30 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maisha ya mwanamichezo yamejaa presha na stress nyingi sana kutokana na miiko ya kiweledi na hali ya kusaka matokeo.

Mwanamichezo anatakiwa kuishi maisha yenye miiko mingi ili kulinda mwili wake usipoteze umbo la kianamichezo.

Wakati wa msimu wa mashindano, mwanamichezo ni kama mtumwa, au mgonjwa anayetakiwa kuishi kwa tahadhari.

Usile chakula hiki, usinywe kinywaji kile na usiende mahali pale. Wanamichezo kama binadamu wengine hujikuta kwenye wakati mgumu kujiuzuia kuyafanya mambo haya ambayo wengi huyapenda.

Kwa hiyo msimu ukiisha, wanataka kupumzika na kufanya kila kitu ambacho walikikosa ili kufidia.

Hapo ndipo utasikia Mohamed Hussein Tshabalala kaenda Dubai, Neymar kaenda Ibiza au Messi kaenda Tanzania kupanda mlima Kilimanjaro n.k.

Wanataka wajiweke mbali kabisa na michezo na kupumzisha akili na miili yao.

Wachezaji wakikosa mapumziko mazuri, hawawezi kujiandaa vizuri na msimu mpya. Na wasipojiandaa vizuri, hawawezi kufanya vizuri kwenye msimu husika. Na hii ndiyo hofu yangu na ndiyo maana ya andiko hili.

Kama kuna mwaka ambao umezivua nguo mamlaka za soka hapa nchini, basi ni huu 2023, hasa katika siku za mwisho kuelekea kumalizika kwa msimu wa 2022/23.

Baada ya panga pangua yaa ratiba tangu mwanzo wa msimu, hatimaye jipu likatumbukia mwishoni na kuacha maumivu makali kwenye mwili wa soka la nchi yetu.

Tarehe ya mechi za mizunguko miwili ya mwisho ya ligi na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports vimeleta mtafaruku mkubwa sana.

Mei pili, waandaaji wa mashindano ya Azam Sports Federation Cup, TFF, walitoa taarifa ya kubadilisha tarehe za mechi mbili za nusu fainali.

Azam FC na Simba ambao walikuwa wakutane Mei 6, ikasogezwa siku moja mbele hadi Mei 7. Singida Big Stars na Yanga, ambao walikuwa wakutane Mei 7, wakabidi wasubiri hadi watakapopangiwa siku nyingine isiyo na jina.

Ikapita wiki nzima bila kujua tarehe ya mechi hiyo...hatimaye mechi ikachezwa Mei 21. Nusu fainali zikafanyika bila kujua tarehe ya fainali. Ikapita tena wiki moja, ndiyo ikajulikana.

Unajiuliza, wenye mashindano hawakujua kama kutakuwa na fainali? Kwenye ligi kuu nako hali ilikuwa hivyo hivyo.

Mei 18, Bodi ya Ligi ilitoka na taarifa kwamba mechi za mizunguko miwili ya mwisho zilizopangwa kufanyika Mei 24 na Mei 28, zimeahirishwa hadi zitakapopangiwa tarehe nyingine.

Siku iliyofuata, Mei 19, Bodi hiyo hiyo ikaja na taarifa nyingine kwamba mechi zile zimerudishwa kwenye tarehe yake ya awali, kasoro mechi mbili zinazoihusu Yanga; dhidi ya Mbeya City na TZ Prisons ambazo zitafanyika Juni 6 na 9.

Mei 20 ikatoka taarifa nyingine kwamba mechi zote za mizunguko miwili ya mwisho zimeahirishwa hadi Juni 6 na 9...hatari!

Awali ligi yetu ilipangwa kumalizika Mei 28, sasa itamalizika Juni 9. Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports ilipangwa kufanyika Juni 3 sasa itafanyika Juni 12.

Juni 18, kutakuwa na mechi za CAF, kufuzu AFCON 202, maana yake kuna wachezaji watatoka kumaliza msimu na kuunga moja kwa moja kwenye timu za taifa.

Wachezaji hawa kama binadamu watakuwa wamechoka sana. Je, watapata muda wa kutosha wa kupumzika? Wachezaji hutakiwa kupumzika angalau kwa wiki tatu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Kwa hiyo kama wachezaji wetu watapumzika baada ya mechi za kufuzu AFCON, yaani baada ya Juni 18, maana yake watatakiwa kupumzika hadi angalau Julai 8. Baada ya mapumziko hayo ndiyo warudi kazini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Na maandalizi hayo kiufundi huhitaji wiki tatu. Maana yake kama wataanza Julai 9, wataendelea nayo hadi wiki ya kwanza ya Agosti, na kumalizika angalau Agosti 6.

Baada ya hapo kutakuwa na mashindano ya ngao ya jamii ambayo msimu huu yametengenezewa mfumo tofauti.

Endapo yataanza Wikendi ya Agosti 12 na kufanyika wiki moja, maana yake yataisha Wikendi ya Agosti 18. Wiki moja baada ya hapo ndiyo msimu uanze.

Kwa kanuni, kwa mazoea na kwa kawaida, ligi ya Tanzania huanza nusu ya pili ya mwezi Agosti, kuanzia Agosti 15 hadi 20.

Sasa kama itakuwa hivyo maana yake tayari kutakuwa na muingiliano wa wiki moja. Ili kuondoa huo mkanganyiko, ligi inatakiwa ianze aidha Agosti mwishoni au Septemba mwanzoni.

Hii itasaidia kuwapa muda wa kutosha wa kupumzika wachezaji wetu ili waje na betri zilizochajiwa vizuri kwa ajili ya marathoni za msimu wa 2023/24. Na msimu mpya utakapoanza, kusiwe na pangua pangua ya ratiba itakayokuja kusababisha tena mkanganyiko mwishoni.

Columnist: www.tanzaniaweb.live