Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wachezaji waepuke haya kipindi hiki cha mapumziko

Simba SC LLLOL Wachezaji waepuke haya kipindi hiki cha mapumziko

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati ligi mbalimbali nchini zikiwa zimemalizika huku timu na wachezaji wakiendelea kujiandaa na msimu ujao, madaktari wameonya mambo kadhaa kwa mastaa kipindi hiki cha mapumziko ili kulinda viwango na afya zao kwa ujumla.

Mara nyingi ligi zinapomalizika wachezaji wengi hupenda kujiachia mitaani, kushiriki michuano isiyo rasmi ‘Ndondo’, kustarehe kupita kiasi, lakini kutozingatia mlo.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya madaktari wa timu za ligi kuu wameonya na kuwashauri mastaa matumizi sahihi ya muda huu wakati ligi imeisha wakijiandaa na msimu mpya wa 2023/24.

Pia viongozi wamepigilia msumali baadhi ya mambo yanayotakiwa kufanywa na wachezaji ili kulinda ubora wao na vipaji kwa maslahi yao huku wakifunguka adhabu na faini kwa watakaoenda kinyume.

MECHI ZA NDONDO

Asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la ushindani wamezalishwa kupitia michuano isiyo rasmi ‘Ndondo’ na wengi wao huamini huko ndio kuna fursa ya ajira na kipato.

Mara nyingi ligi zinapo simama wengi huanza kusaka zilipo ligi za mchangani wakiamini watakutana na wenzao kubadilishana mawazo na kupoteza muda, lakini zaidi wakiwaza pesa.

Ikumbukwe wachezaji wengi husajiliwa na timu kwa mwaka mmoja, hivyo ligi zinapomalizika huwa hawana chochote mifukoni na kuamua kujikita kwenye michuano hiyo.

Hata hivyo kama haitoshi mastaa wengi huamua kutumia nafasi hiyo kujichanganya na wana kitaani waliopotezana nao kwa muda mrefu, hivyo kuamua kuzama huko kwa kujichangamsha.

Pia baadhi hutumia muda huo kujifua kupitia ndondo wakiamini ligi ikirejea watakuwa imara kuweza kuhimili mikiki mikiki ya soka kuendana na hali ya mabadiliko ya kazi zao uwanjani bila kujali usalama wa afya zao.

Wapo wengine ambao huambulia majeraha kutokana na viwanja vinavyotumika kwa michuano hiyo na kujikuta wakijeruhiwa na kurejea kwenye timu zao wakichechemea.

STAREHE

Kipindi cha mapumziko kwa wachezaji huwa kinaambatana na mambo mengi haswa inapofika hatua ya kila mmoja kuondoka kambini kurejea mitaani ambapo baadhi yao hujiachia kupitiliza.

Wachezaji wengi hutumia muda wa mapumziko kula bata sana bila kujali afya zao, ambapo kwa kiasi kikubwa hupotezwa zaidi na ‘Warembo’ wa kitaa kutokana na umaarufu wao wa kusakata kabumbu.

Kutokana na hali hiyo baadhi hujikuta wakishuka viwango kutokana na starehe nyingi lakini kupoteza muelekeo kwenye kazi zao za mpira na baadaye kushindwa kuendelea na kipaji chao.

Kutokana na kutokuwa na usimamizi wowote mchezaji huamua kujiachia sehemu yoyote na mtu yeyote bila tahadhari kama alivyokuwa kambini na wachezaji wenzake.

ISHU ZA MISOSI

Baada ya timu kuvunja kambi na wachezaji kurejea makwao, huko mitaani hali huwa ni tofauti kwa mastaa kutamani kula kula hovyo kila msosi wanaokutana nao.

Hali nyingine huonekana kama simba mnyama mwenye njaa anapofika mwituni kukutana na swala namna anavyobughia, sawa na baadhi ya mastaa wanapofika mtaani kubwia vyakula bila kufuata maelekezo ya kiafya.

Kipindi kama hiki ndio utakuta wachezaji wakitafuna aidha chipsi, nyama, ugali, ndizi na aina yoyote ya chakula bila kufuata muda au aina yam lo uliopangwa katika kulinda afya na kipaji chake.

Kawaida mchezaji awapo kambini huwa inafuatwa zaidi mpangilio wa ratiba kuanzia mazoezi, mapumziko, chakula na kubadilishana mawazo na wenzake na siyo kila muda atafanya yote kwa pamoja.

RATIBA NZURI

Ratiba ya wachezaji huwa inaeleweka kuwa iwapo timu itakuwa na mazoezi mathalani asubuhi, mchezaji ataoga, kupata chakula ya mchana na kupumzika (kulala) kwa masaa manane au zaidi.

Lakini baada ya ligi kumalizika wapo wachezaji ambao husahau ratiba ya mazoezi na kupumzika akijikuta analala muda wowote kwa masaa anayojisikia hali ambayo humuathiri kiafya na kipaji chake.

Muda mwingi unamkuta mchezaji anazurula barabarani hata kushiriki shughuli mbalimbali bila kutenga muda wa mapumziko akiamini itamjenga kufahamika zaidi mtaani kwake.

WASIKIE WATAALAM

Daktari wa Tanzania Prisons, Kilulu Masuga anasema licha ya mchezaji kuwa mtu mzima kutoweza kufuatiliwa hadi nyumbani, lakini lazima wazingatie utaratibu namna ya kuishi nje ya kambi haswa kipindi kama hiki.

Anasema kawaida timu zinapovunja kambi makocha na viongozi hutoa program kwa wachezaji kuzingatia utaratibu wa kuishi ili wanaporejea kikosini wawe imara na bora kwa uwezo uleule.

“Lakini kwa wale wanaojitambua lazima wanafuata maelekezo, siyo kama wengine unakuta muda huo anaenda kwenye ndondo, starehe kuliko kujitawala hadi kujisahau mipaka yake,”

“Hali hiyo ya kujiachia kupitiliza humuathiri kwanza kisaikolojia kwa sababu anawaza alipokuwa na mazingira anayoenda ni tofauti hivyo kipaji chake kupotea,”

“Wapo wachezaji tunawaona mitaani wanashiriki ndondo, wanazurula, lakini lazima wazingatie pia mlo kama wanavyokuwa wanaishi kambini japokuwa kuna ile ya kutumia mara moja kutojiathiri kwa ujumla,” anasema Masuga.

“Mfano hizi ndondo utakuta majereha mengi hususani eneo la goti na misuri kubana na ninaamini wale wachezaji wanaojitambua lazima wazingatie utaratibu ikiwamo ratiba zao za mazoezi na kupumzika,” anasema daktari huyo.

Naye daktari wa Namungo, Hilal Mfugwa anasema mara nyingi wachezaji wanapoondoka kambini, hurejea kikosini na mabadiliko mengi na zaidi ni kuongezeka uzito kutokana na kutozingatia milo.

Anasema Namungo huwa na utaratibu wa kuwapima wachezaji kabla ya kuvunja kambi lakini kutoa elimu ya namna ya kula vyakula akibainisha kuwa ishu ya Ndondo huwa na athari kubwa.

“Mara nyingi inaonesha wachezaji wanapotoka makwao huwa wanaongezeka uzito na hali hiyo husababishwa na kula sana, hata muda mwingine huathiri kiwango chao,” “Kuhusu ndondo ni faida kwa wale wachezaji wanaotafuta usajili lakini kwa yule mchezaji mwenye uzoefu na ligi ya ushindani haina afya yoyote,” anasema Mfugwa.

VIONGOZI SASA

Katibu mkuu wa Namungo, Ally Suleiman anasema kutopata muda wa kutosha kupumzika kwa mchezaji, starehe na kutozingatia mlo sahihi inaweza kuua kipaji kwa ujumla. Anasema kutokana na hali hiyo, Namungo iliweka masharti makali kwa wachezaji wake ikiwamo kutoshiriki ndondo, kukesha au kuzurula kwenye maeneo ya starehe kwani adhabu yake imeelezwa wazi kwenye mikataba.

“Tulipojua hilo tuliamua kuweka faini kwa wanaokunywa soda au juisi na kukaa maeneo ya baa, lakini wale wa ndondo ni kukatwa mishahara, lakini tukaenda mbali zaidi kufuatilia mchezaji mmoja mmoja,”

“Tukaamua kabla ya kuvunja kambi tunakutana kujadiliana kuanzia uongozi na benchi la ufundi kuweka maelekezo wale ambao tutahitaji kusajili kuongeza nguvu tunawafuatilia mienendo yao,” anasema Suleiman.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Dodoma Jiji, Johnson Fortunatus anasema iwapo atakosa mapumziko, kutozingatia mlo stahiki, kushiriki ndondo na kujiweka kwenye starehe lazima atapoteza kiwango chake.

Anasema Dodoma Jiji katika kuhakikisha wanaendelea kulinda vipaji walipiga marufuku ndondo, ulevi au kwenda kinyume na utaratibu wa timu akifafanua kuwa hadi sasa wachezaji zaidi ya 10 walishafukuzwa wengine kusitishiwa mikataba.

“Mfano wapo watatu niliwaondoa kwa kushiriki ndondo, wawili nikasitisha mikataba kwa ulevi wa kupindukia, wengine kadhaa walichelewa kurudi kambini bila sababu za msingi,”

“Kwa maana hiyo mimi binafsi licha ya ripoti ya kocha kupendekeza mchezaji fulani, lazima niangalie nidhamu yake ikoje kabla ya kiwango chake uwanjani,’

“Kwanza naangalia jina la Taasisi, lakini mchezaji anaweza kustaafu kwa miaka 37 akijitunza vizuri tofauti na mtumishi mwingine wa umma anayefikisha miaka 55 hadi 60, hivyo lazima wazingatie mlo, mazoezi aache kujiachia” anasema Fortunatus.

Columnist: Mwanaspoti