Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waburuza mkia watano Ligi Bara na tumbo joto

18422 Pic+singida Waburuza mkia watano Ligi Bara na tumbo joto

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BAADA ya Serikali kutangaza inatarajia kuruhusu Ligi Kuu Bara kurejea, jambo litakalofanikisha bingwa wa ligi hiyo kupatikana uwanjani, na pia timu zitakazopanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza pamoja na zile zitakazoshuka daraja, tayari viongozi wa timu zilizopo chini ya msimamo wa Ligi Kuu, .....

matumbo yao yameonekana kuwa na joto la hofu.

Baada ya janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na vizuri vya corona, kulizuka maoni mengi, huku baadhi wakitaka Ligi Kuu ifutwe kama vile ilivyofanywa kwenye baadhi ya nchi duniani.

Baadhi ya nchi duniani zimefuta ligi zao na kutoa ubingwa kwa timu zilizopo juu, huku zikiziacha timu za chini kwenye msimamo zikiendelea kupeta.

Ina maana hakuna timu zilizoshuka. Ukisikiliza maoni ya viongozi wengi hasa zilizokuwa chini ya msimamo walikuwa wakitaka Simba apewe ubingwa, lakini huku chini ya msimamo kusiwe na timu itakayoshuka daraja msimu huu.

Hata hivyo, urejeo wa Ligi Kuu kama kusudio la serikali, zimewaacha tumbo joto timu ambazo tayari zilishaanza kuona huenda zingebakishwa na kuiacha Gwambina FC ambayo inatakiwa kushinda mechi mbili tu kati ya nne ilizonazo kusubiri msimu ujao kupanda Ligi Kuu.

Kwenye makala haya, tunawaletea timu ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka daraja, na sasa zinatakiwa zijiandae kisawasawa ili zitumie nguvu zao za uwanjani kutoshuka daraja, na si mteremko...

1. Singida United (pointi 15)

Singida United ndiyo timu yenye hatari zaidi ya kushuka daraja kwenye Ligi Kuu kuliko timu nyingine yoyote ile. Wapo wachambuzi wanaona ni kama tayari imeshuka kiuhasilia, lakini si kimahesabu. Ina pointi 15 tu mpaka sasa ikiwa imesaliwa na mechi tisa tu. Si tu kwamba inashika mkia ikiwa chini, lakini inazidiwa pointi nane na timu iliyokuwa juu yake, Mbao FC. Mpaka ligi inasimamishwa, mechi ya mwisho iliifunga Mbeya City mabao 2-1, ikitoka kupoteza mechi nne mfululizo.

2. Mbao FC (pointi 23)

Ni timu ambayo imeshangaza wengi msimu huu kutokuwa na kiwango cha kawaida, kilichozoeleka. Inaweza kabisa ikawa ndiyo msimu wao wa mwisho kucheza Ligi Kuu, tangu ilipopandishwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) msimu wa 2016/17 kutokana na tuhuma za upangaji matokeo kwa timu za Geita Gold, JKT Kanembwa, Polisi Tabora na JKT Oljoro.

Iliingia kwenye Ligi Kuu na kuwa timu ya kutisha. Lakini kila msimu inaonekana kupungua makali, huku msimu huu ikiwa kwenye hatari zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ina pointi 23, ikibakiza mechi tisa tu, ikishika nafasi ya 19.

3. Alliance FC (pointi 29)

Ina pointi 29 ambazo bado haziwezi kuiweka salama kubaki Ligi Kuu msimu huu, bali inabidi ijifunge kibwebwe kisawasawa.

Kinachotoa shaka zaidi ni kwamba Alliance ndiyo timu iliyopoteza mechi zote tano za mwisho mfululizo, hadi pale ligi iliposimama kutokana na ugonjwa wa COVID-19. Inakamata nafasi ya 18, hivyo nayo imo ndani ya zile timu nne zinazonukia kushuka daraja. Ni ushindi mfululizo unaohitajika katika mechi tisa ilizobakisha kwenye ligi ili ijikwamue.

4. Mbeya City (pointi 30)

Cha kusikitisha msimu huu ni kwamba zile timu ambazo miaka michache tu iliyopita zilitamba, ziko hoi bin-taaban. Nazizungumzia Singida United, Mbao FC na hii ni Mbeya City.

Ilileta mapinduzi makubwa msimu wa 2013/14, kiasi kwamba kila timu iliyokuwa ikitaka kupanda ilitaka kuwa kama Mbeya City.

Kwa sasa iko taaban, ikiwa moja kati ya timu zinazohesabiwa kuwa zitashuka msimu huu kama zikikaa vibaya. Inakamata nafasi ya 17, ikiwa na pointi 30. Iwapo haitojirekebisha kwenye mechi zake tisa zilizobaki, msimu ujao inaweza isiwapo Ligi Kuu.

5. Ndanda FC (pointi 31)

Hii ndiyo timu yenye bahati kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani misimu yote iliyokuwa kwenye ligi imekuwa ikipona kushuka dakika za mwisho. Wengi wanataka kuona kama msimu huu nao wanaweza kupona tena. Ni timu ambayo miaka yote ina 'zali' la kubaki kwenye zile mechi za mwisho.

Msimu huu kama kawaida, inashika nafasi ya 16, ikiwa na pointi 31. Kwa mechi za karibuni kabla ya kusimamishwa, ilikuwa imeanza kufanya vema kama kawaida yake. Hata hivyo, waswahili wanasema 'siyo kila siku ni Ijumaa'. Mechi zake tisa zilizobaki zitatoa jibu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live