Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waarabu walivyoupeleka mpira katika mfuko wa jeans

Neymar Al Hial Sm Neymar

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilianza kama mzaha. Ilianzia wapi? Walianza kununua klabu za Ulaya. Ikaenda wapi? Wakapeleka kombe la dunia Qatar. Halafu? Wakamchukua Cristiano Ronaldo, mchezaji mwenye jina kubwa duniani wakampeleka zao Saudia Arabia. Halafu nini kimefuata? Wiki hii iliyoisha wamecheza mchezo maarufu unaoitwa Chess.

Wameucheza katika ofisi za Fifa na kuipeleka michuano ya kombe la dunia pale Saudia Arabia mwaka 2034. Akili iliyotumika ni kubwa. Ni wazi noti zao zimeinunua Fifa lakini akili iliyotumika kupeleka kombe la dunia pale Riyadh na miji mingine ya Saudi Arabia nimeipenda.

Kitu cha kwanza ni kombe la dunia lijalo litafanyika Amerika Kaskazini. Litafanyika Marekani, Mexico na Canada. Kwa Marekani hii itakuwa mara ya pili. Kwa Mexico itakuwa mara ya tatu. Waliandaa mwaka 1970, kisha mwaka 1986 katika fainali ambazo ziliitwa ‘fainali za Diego Maradona’ halafu wanaenda kuandaa tena fainali zijazo. Hii itakuwa mwaka 2026.

Kwa akili kubwa zaidi Fifa wamepeleka michuano ya kombe la dunia mwaka 2030 katika nchi nyingi na mabara mengi. Kisa? Kuazimisha miaka 100 tangu kuanza kombe la dunia. Kumbuka michuano ya kwanza ya kombe la dunia ilifanyika mwaka 1930 pale Uruguay. Wakati huo timu zikisafiri kwa Meli kwenda kucheza michuano hiyo.

Michuano hii itaandaliwa na wenyeji watatu. Hispania, Ureno na Morocco. Halafu kuna mechi kadhaa za kumbukumbu zitachezwa katika nchi za Argentina, Paraguay na Uruguay ambako michuano hii ilifanyika kwa mara ya kwanza. Sikiliza, watu wa FIFA wana akili nzuri. Hii haikupangwa kwa bahati mbaya kama unavyodhani.

Mwaka 2026 michuano itakuwa imeandaliwa Amerika Kaskazini. Mwaka 2030 michuano itakuwa imeandaliwa Ulaya na Afrika. Kwa Ulaya unamaanisha Hispania na Ureno. Kwa Afrika unamaanisha Morocco. Lakini hapo hapo itakuwa inamaanisha kuna mechi zimeandaliwa Amerika Kusini kupitia kwa Argentina, Paraguay na Uruguay.

Kwa kuangalia kabla ya hapo kombe la dunia litakuwa limeandaliwa Amerika Kusini basi inamaanisha mechi za kombe la dunia kwa michuano miwili zitakuwa zimeandaliwa Amerika Kaskazini, Ulaya, Afrika, Amerika Kusini. Nani wanabakia? Ni Asia na Australia.

Haikushangaza kuona Saudi Arabia na Australia zikiwa zimebakia kuandaa kuombea la dunia la mwaka 2034. Ulikuwa mchezo wa kuigiza baada ya Australia kuamua kujitoa. Unajua walijitoaje? Hauwezi kujua. Unachoweza kubashiri ni bahasha ilitembea na Australia haikuonekana kama nchi ya kisoka. Acha wakaandae Rugby.

Mwishowe walibaki rafiki zetu Saudi Arabia. Haikuwa bahati mbaya. Ulikuwa mchezo uliopangwa kwa akili. Akili ambayo ilitokana na bahasha ambayo Waarabu wanaitembeza katika soka. Wameziacha baadhi ya nchi za Ulaya zikiwa zimenuna. Nchi ambazo zina uchumi mkubwa lakini huwa tunazichukulia kama nchi za kisoka.

Nadhani ambaye atakuwa amenuna zaidi atakuwa Mwingereza. Mara ya mwisho aliandaa kombe la dunia mwaka 1966. Anatamani kuandaa tena. Ana kila sababu. Hapa katikati alijaribu kupambana kutaka kuandaa lakini akazidiwa Kete na Mrusi pamoja na Mwarabu wa Qatar. Fifa imeupeleka mpira katika ‘mwenye nacho ataongezewa’. Wote hawa walitumia pesa kupata nafasi.

Na sasa imetumika akili hii iliyoambatana na bahasha. Jaribu kufikiria. Majuzi tu kombe la dunia lilikuwa ukanda huo. Kulikuwa na sababu gani ya kuurudisha tena mpira katika ukanda huo?

Hata hivyo rafiki zangu Fifa hawakutaka lawama. Walichofanya ni kutumia michuano miwili ijayo ya kombe la dunia kuisambaza kwa haraka michuano hii hili wapate uhalali wa kuipeleka Saudi Arabia. Wamefanikiwa.

Sio kwa bahati kwamba kwa sasa kila kitu kinakwenda kwa Waarabu. Wana pesa. Wameuweka mpira mkononi. Wana ajenda yao. Wamezinunua timu kubwa Ulaya na bado wanataka kununua nyingine. Wamenunua wachezaji wakubwa na bado wataendelea kuwanunua. Na sasa wameiweka mfukoni Fifa na wanapanga walitakalo.

Pesa inaongea. Ungeangalia mwenendo tu wa namna Mwarabu anavyotumia pesa katika soka ungejua tu lilibaki suala la muda kabla ya kombe la dunia kuchezwa Saudi Arabia.

Usiongee kuhusu soka peke yake. Sasa hivi wapo tayari kumwaga pesa ili Beyonce akaimbie matajiri katika boti pale Riyadh.

Siku moja kabla ya kutangazwa Kombe la Dunia kuchezwa Saudi Arabia pambano la Tyson Fury na Francis Ngannou lilikuwa linachezwa Riyadh. Huu ni mwendelezo wao wa kukaribisha mechi za ngumi zichezwe pale kwao. Tayari mabondia wengi wakubwa wameshakwenda kupigana pale. Na bado wengi watakwenda.

Huku katika soka nahisi siku wakishindwa kupandisha soka lao si ajabu ukasikia raundi ya kwanza ya Ligi Kuu England inachezwa katika ardhi ya Saudi Arabia. Hakuna unachoweza kufanya. Pesa inaongea na Mwarabu ameamua kutumia pesa zake. Kuna kitu ambacho wanataka kukifanya hata kama wengine hatukifahamu vyema.

Ogopa mtu ambaye anatumia pesa bila ya kuingiza faida ya papo kwa papo. Waarabu wameamua kufanya hivyo katika michezo na hakuna anayeweza kuwazuia. Labda tuwasifu Manchester United kwa kuzuia timu yao isiuzwe kwa Waarabu na kuamua timu yao iende kwa Mwingereza mwenzao. Tayari Mwarabu alishafika katika dau la juu kabisa.

Tusubiri kuona filamu hii itaishia wapi lakini mpaka sasa Mwarabu ametisha katika filamu hii.

Hakuna wa kumzuia. Rafiki zangu FIFA wamekuwa wepesi zaidi katika vita hii na tayari wamesalimu amri kwa Mwarabu kama wachezaji wengi wakubwa wanavyosalimu amri.

Kwa ambao watabahatika kuwa hai watatuambia kombe la dunia la mwaka 2034 litakuwa vipi. Kitu cha kwanza cha uhakika ni kwamba michuano yenyewe nayo italazimika kufanyika Desemba katika kipindi cha baridi. Ni kama ambavyo ilifanyika Qatar licha ya watu wengi kutoamini kama ingefanyika.

Pia tunataka kujua kama kuna masharti ya imani za Kiislamu yatalegezwa.

Nilikuwa Qatar na sisi walevi tulikunywa pombe kama kawaida. Vipi pale Saudia maisha yatakuwa yale yale au ndugu zangu FIFA hawakuzingatia yote haya kwa sababu ya bahasha za kakhi?

Tusubiri na kuona ambacho kitatokea. Kwa sasa tuendelee kuona filamu hii ambayo Mwarabu kauweka mpira mfukoni.

Columnist: Mwanaspoti