Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waamuzi Ligi Kuu jiangalieni

Simba Vs Singida Chama.jpeg Waamuzi Ligi Kuu jiangalieni

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi karibuni gazeti hili lilichapisha makala takriban mara nne mfululizo katika matoleo yake za mahojiano maalumu na mwamuzi wa kwanza mwanamke hapa nchini, Elizabeth Kalinga ambaye pamoja na mambo mengi mengineyo alizungumzia mambo mengi ya uwanjani.

Elizabeth ambaye kwa sasa ni mstaafu alizungumzia ubora wa mchezo ni kufuata kanuni na kwa waamuzi ni lazima kuzitekeleza kama ilivyo kwa wasimamizi wa mchezo, mashabiki na wachezaji.

Sheria za soka zipo 17, lakini kanuni ambazo hutungwa kwa kuzingatia sheria zinasemaje hizi huja kila baada ya msimu kumalizika na huandaliwa kwa ajili ya kutumiwa msimu unaofuata kwa kushirikisha mamlaka na wadau.

Kimsingi, kanuni hazipaswi kwenda tofauti na sheria na ndio maana katika usimamizi wa kanuni, mwamuzi na mamlaka za soka na hata klabu huzingatia misingi ya sheria zilizopo. Na ndivyo inavyokuwa.

Ligi Kuu Bara kwa sasa iko katika raundi ya tano, ambapo timu zinaendelea kuikata zikibakisha takriban mechi 25 ili kuihitimisha mwakani. Kila timu imejiandaa na inapambana kuweka mambo sawa ikiwa na lengo la kuwania ubingwa wa nchi.

Hata hivyo kuna mechi kadhaa zinazohusisha vigogo vya soka nchini - kwa maana ya Simba, yanga na Azam FC kumeanza kuonekana mambo ambayo yasipokemewa huenda yakaturudisha kulekule ambako waamuzi walikuwa wakilaumiwa kwa kuuharibu mchezo huo miaka ya nyuma kutokana na uamuzi wanaoufanya.

Tusingependa kuitaja michezo hiyo kwa sababu mchezo wa soka kama ilivyo mingi mingineyo huchezwa hadharani, lakini mashabiki na wadau wa soka walioifuatilia ni mashahidi wa namna waamuzi ‘walivyomeza filimbi’ katika baadhi ya matukio yaliyojiri kwenye mechi hizo.

Kuna namna ambavyo waamuzi hawakuwa sahihi kabisa katika kusimamia sheria 17 za soka na hii ni ama kwa makusudi au bahati mbaya, lakini walikwenda ndivyo sivyo na ni wazi kwamba wanastahili kulaumiwa kwa matukio hayo.

Tumeamua kulisema hili mapema tukirejea alichokisema mwamuzi Elizabeth kuwa, waamuzi ndio kila kitu katika mchezo wa soka kwani wao ndio wanaoibeba furaha au huzuni ya mashabiki kabla na baada ya michezo.

Kwa sababu ligi yetu imepiga hatua kubwa duniani ikitajwa kuwa namba tano barani Afrika, hakuna sababu ya kuanza kuifanya ianze kuchukiwa.

Tukumbuke kwamba ligi hii inafuatiliwa na dunia nzima kiupitia matangazo ya runinga, hivyo hakuna sababu ya kuirudisha nyuma.

Tunalisema hivyo tukizingatia kwamba tunao udhamini wa mabilioni ya fedha yaliyowekezwa katika uendeshaji wa ligi hii na pia inakaribisha mastaa mbalimbali kutoka nje wanaokimbilia hapa nchini kuja kuinyayua zaidi ligi yetu. Hivyo hatutaki wachache waturudishe tulikotoka.

Columnist: Mwanaspoti