Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waamuzi Bongo wanalipwa laki tatu

Waaamuzi Pic Posho Waamuzi Bongo wanalipwa laki tatu

Fri, 6 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jana tulianza mfululizo wa ripoti maalumu juu ya waamuzi wa soka nchini na kuona namna walivyo muhimu katika mchezo huo, wanavyopatikana na madaraja yao sambamba na ukweli juu na wamiliki wa waamuzi pamoja na mambo mengine kuhusiana na wao na soka la Tanzania kwa ujumla.

Leo tunaendelea na ripoti hiyo kwa kuangalia vitendea kazi vyao, wanavipataje na posho zao na changamoto wanazokabiliana nazo kutoka kituo kimoja kwenda kingine na malimbikizo ya madeni wanayodai na jinsi wanavyokumbana na vitisho. Kivipi? Endelea nayo upate majibu kamili.

MTIHANI WA VITENDEA KAZI

Umewahi kujiuliza, waamuzi wanapokuwa uwanjani na kupendeza na jezi zao za rangi ya chungwa au njano, nyeusi kama sio nyekundu au rangi nyingine yoyote wanapata wapi vifaa vyao vya kazi.

Tofauti na timu, kwa waamuzi, jezi zinazovaliwa na wote kwenye mchezo huo huwa ni mali ya mtu mmoja, ni wajibu wake kuhakikisha ni safi.

“Huo ndiyo utaratibu, mwamuzi anaponunua jezi, kama ni ya rangi nyesi, basi sharti anunue pea nne kwa ajili yake na wenzake wawili,” anasema mwamuzi mkongwe, Israel Nkongo.

Anasema vivyo hivyo kwenye jezi za rangi nyingine, mwamuzi anaponunua lazima anunue na tatu za ziada kwa ajili ya washika vibendera na kamisaa wa mechi hiyo.

“Atavaa nani? Hilo utalifahamu pale mtakapopangiwa kuchezesha mechi, mkikutana siku moja kabla ya mechi ndipo mnapanga, tuvae jezi gani kwa kuwa kila mmoja anakuwa amekuja na seti zake, huo ndiyo utaratibu wetu nchini,” anasema.

Mmoja wa waamuzi wakongwe, Isihaka Shirikisho anasema moja ya vitu muhimu kwenye kabati la mwamuzi ni kuwa na jezi tofauti zisizopungua pea sita mpaka nane ambazo kila moja inakuwa na seti nne.

“Kazi ya uamuzi ni kazi kama kazi nyingine, sharti uwe na vitendea kazi japo kuna baadhi ya kazi vitendea kazi unavikuta kazini, kwenye uamuzi unapoingia lazima uhakikishe una vitendea kazi vyako,” anasema.

VIFAA NI POSHO YA MECHI

Mwamuzi wa Ligi Kuu anapokuwa kwenye mechi, inaelezwa analipwa kati ya Sh300,000 hadi 350,000 kwa mechi, pesa ambayo inajumlisha nauli ya kutoka anakoishi kufika kwenye kituo cha kazi na gharama za malazi na chakula.

“Ukipiga hesabu kwa haraka haraka, pesa ya posho kwa mwamuzi wa Ligi Kuu inaweza kufika gharama ya vitendea kazi vyake vyote anavyopaswa kuwa navyo,” anasema Israel Nkongo.

Akitolea mfano gharama za kiatu kwa mwamuzi, kuwa cha bei ya chini uwa ni Sh 45,000 na kile cha bei kubwa ni Sh 120,000, lakini pia jezi ambayo moja ni Sh 25,000 mara nne, hivyo laki moja.

“Kibendera ni Sh 35,000, kuna filimbi ambazo zinahitajika kuwa tofauti tofauti ili ikitokea mashabiki wana filimbi yenye mlio kama wako uweze kubadilisha, kadi na vifaa vingine vinavyohitajika kwa waamuzi,” anasema Nkongo.

UNAFUU HUKO HAPA!

Ukiachana na vifaa ambavyo huwa ni mali binafsi ya mwamuzi, Nkongo anasema pia chama cha waamuzi huwa vina vifaa, ingawa asilimia kubwa waamuzi hutumia vifaa binafsi.

“Pia, kama ikitokea ligi ina mdhamini, hapo ndipo kila mwamuzi wa ligi ile atapewa vifaa ambavyo atavitunza kama mali yake, kinyume na hapo ni mwamuzi kujinunulia vitendea kazi,” anasema.

Ukiachana na vifaa vingine kama filimbi, kibendera na njumu, katika jezi, mwamuzi aliyepangwa kwenye mechi lazima awe na pea nne za jezi kwa ajili yake na wenzake.

“Mnapokutana kwenye kituo, mnakubaliana mvae aina ipi, kama ni nyekundu, nyeusi au vinginevyo, lakini kila mmoja katika huo mchezo anapaswa kuwa na pea nne za jezi kwa ajili ya wenzake pia,” anasema Nkongo.

Anasema baada ya mechi, gharama za kufua jezi ni juu ya mwamuzi anayezimiliki, hivyo wanapotoka uwanjani zinakusanywa anarudishiwa mwamuzi husika.

“Huo ndiyo utaratibu, tunajitegemea kwenye vifaa, unafuu kwetu ni inapotokea ligi ina mdhamini, kama hakuna mdhamini hakuna namna nyingine zaidi ya kila mmoja kujitegemea vifaa vyake vya kazi.”

MALIPO YAO YAKO HIVI

Waamuzi wanalipwa posho zao kulingana na madaraja na aina ya mechi na mmoja ya waamuzi hao anafichua, waamuzi wa Ligi Kuu hulipwa Sh350,000, Championship Sh75,000 hadi Sh100,000 huku wale wa First League nao hulipwa Sh50,000 hadi Sh75,000.

“Hata hivyo, msimu huu mmoja wa wadhamini wa Ligi Kuu walitoa 500,000 kama posho ya waamuzi lakini kutokana na Ligi ya Championship na First League kutokuwa na wadhamini, imelazimika Sh50,000 kwenda kusapoti First League na Sh100,000 kwenda Championship.

UKIDAI TU, MSALA

Umewahi kukutana na ‘rungu’ hilo, wapo wanaodai waliondolewa kwenye orodha ya waamuzi baada ya kudai posho kwenye moja ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza.

Mwamuzi, Bam Bilasho wa Dodoma aliyekutana na mkasa huo anasema, wapo wengi ambao wameingia kwenye jahazi hilo, akiwamo yeye ambaye aliondolewa mwaka 2020 akiwa anachezesha Ligi Daraja la Kwanza sasa ni Championship.

Akisimulia mkasa huo, Bilasho alisema mwaka 2020, alienda kuchezesha mchezo kati ya timu ya Boma na JKT Mlale, wilayani Kyela mkoani Mbeya.

“Tumemaliza mechi jamaa anatuambia hakuna hela nikamwambia msiniletee ujinga hapa nilileta mtiti mpaka walilipa.

“Na yule bwana msimamizi alitoa hela yake mfukoni nikwambia acha kabisaa unanitoaje Dodoma unakuja kunileta huku halafu hunilipi?

“Baada ya hapo inaonekana wale jamaa walisema huyu jamaa ni msumbufu tumuondoe na walinisimamisha na nilimwambia jamaa awaambie, sipendi upuuzi,” alisema mwamuzi huyo.Bilasho alisema: “Nawajua waamuzi wanaodai hakuna mwamuzi wa Ligi Kuu ambaye hadai, mwaka jana wanadai, Ligi ya Wanawake wanadai hiyo ndio hawajawahi kulipwa hata 100. ligi zote za wanaume wanadai,”alisema.

Columnist: Mwanaspoti