Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vurugu za mashabiki Brazil, Argentina ni darasa

Vuruguuuuu Vurugu za mashabiki Brazil, Argentina ni darasa

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jumatano usiku wiki iliyopita katika mechi ya kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2026 kati ya Brazil na Argentina nchini Brazil ilishuhudiwa vurugu za mashabiki wahuni wa soka wa nchi hizi.

Vurugu hizi zilitokea kwenye Uwanja wa Maracana wa jijini Rio de Janeiro wakati nyimbo za taifa zinaimbwa, na kuzua taharuki na kusababisha mechi hiyo kuchelewa kuanza kwa dakika 30.

Polisi maalum wa wakutuliza ghasia walijibu mapigo kwa kuwavamia mashabiki hao waliokuwa nyuma ya goli kuanza kuwatenganisha na huku wakitoa vichapo kwa kutumia fimbo zao na virungu.

Mashabiki wa Argentina walijibu mapigo kwa kurusha viti walivyong’oa uwanjani hapo na kuwarushia polisi hao ambao walionekana wanaijua vyema kazi ya kukabiliana na uhalifu huo.

Iliwalazimu wachezaji wa timu zote kwenda uelekeo walipo mashabiki hao wakiongozwa na manahodha wa timu zote mbili Messi na Morquinhos na kuwasihi kuwa watulivu ili mechi hiyo iendelee.

Angalau hatua hii ilichangia kutuliza hali hiyo ingawa wachezaji wa Argentina walirudi katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa dakika 10 kusubiri hali itulie.

Hatimaye hali hiyo ilitulia na mchezo huo ambao ulikuwa umebeba hisia za hali ya juu kwa timu zote mbili, ilishuhudiwa Brazili ikichezea kichapo cha bao 1-0 ikiwa nyumbani.

Vurugu hizo ni kama vile pia zilichochea wachezaji kwani mechi ilipoanza ni kama vile walikuwa katika hali kukamiana na hivyo mchezo kutawaliwa na faulo za mara kwa mara.

Hali iliyochangia kusimama mara kwa mara na huku kadi kadhaa za njano zikitolewa pande zote hatimaye kadi nyekundu ilitoka dakika ya 81 kwa mchezaji wa Brazil, Joelinton.

Katika kundi hili la timu za Amerika ya Kusini timu ya Argentina imefuzu ushiriki wa Kombe la Dunia 2026 kwani ndio kinara wa kundi hilo mpaka sasa na itaenda katika fainali hizo zitakazoandaliwa kwa pamoja na Canada, Mexico na Marekani, ikiwa bingwa mtetezi baada ya kulitwaa taji hilo 2022 kule Qatar.

Tukio la vurugu kwa mashabiki wa soka ni moja ya vitu tishio kwa maisha na afya za watazamaji hii ni kutokana na viwanja vya soka kubeba maelfu ya mashabiki wanaojazana.

Inapotokea vurugu kama zile huwa zinatishia aliyekuwemo na asiyekuwemo katika fujo kuweza kupata majeraha au kifo kutokana na mazingira ya viwanja yalivyo ya watu kujaa na kubanana.

Habari nzuri siku hiyo hapakuwa na kifo isipokuwa shabiki mmoja wa Argentina alijeruhiwa vibaya na kuvuja damu nyingi kichwani, alipewa huduma ya kwanza na kupelekwa haraka hospitalini.

Nchi hizi mbili zinasifika kuwa na uhasama wa kisoka na huku mashabiki wao ni vichaa wa soka katika ngazi ya taifa na klabu hivyo fujo kutokea haikushangaza.

Mtakumbuka ni mwezi huu huu imeshuhudiwa vurugu za mashabiki kwenye uwanja huo huo kabla ya mechi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Amerika ya Kusini maarufu kama Copa Libertadores kati ya klabu ya Fluminense ya Brazili na Boca Junior ya Argentina.

Kwa hiyo tayari vyombo vya usalama vilikuwa vimejipanga vyema kukabiliana na matukio ya uhalifu ya namna hiyo ambapo wanasaikoloji na ustawi wa jamii wanaita ni Hooliganism.

Hapa wanamaanisha vitendo hivi vya kihalifu vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kufanya mambo ya kihuni lama fujo, kupigana, kutoa lugha chafu, kuharibu na kushambulia watu wengine.

Tafiti za vurugu michezoni zinaonyesha kuwa mara nyingi chanzo cha kutokea vurugu ni uwepo mashabiki wa daraja la chini la wafanyakazi, unywaji pombe, wingi wa watu na upinzani wa timu.

Na shida kubwa ya soka huwa inabeba hisia, ndio mana katika mechi kama ile kwa mashabiki na wachezaji wenyewe inakuwa ni mpambano kama vile ni jambo la uadui.

Leo tuone athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na vurugu katika viwanja vya soka.

VURUGU NI HATARI

Mtakumbuka viwanja huwa vinabeba maelfu ya mashabiki ambao huwa na makundi mbalimbali ikiwamo watoto, wanawake, wazee, walemavu.

Haya ndio makundi ambayo yanakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha au kupata majeraha inapotokea hali kama ile katika uwanja uliojaza watu wengi.

Uwanja kama Maracana ambao una rekodi ya kipekee ya kubeba watu 199,854 mwaka 1950 katika fainali ya Kombe la Dunia kati ya Brazili na Uruguay, siku hiyo tayari tiketi 69,000 zilikuwa zimeuzwa.

Kutokana na msongamano mkubwa kama huu inapotokea vurugu hatari ya kupoteza maisha inakuwa kubwa kutokana na kukanyagana au kubanana katika eneo lenye nafasi ndogo kupenya.

Vifo vinaweza kutokea kutokana na kukosa hewa au kujeruhiwa maeneo nyeti ya mwili ikiwamo maeneo ya kichwani, tumboni au kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha makubwa.

Mfano katika mechi hiyo mara baada ya mapigano ya mashabiki hao kuanza wapo ambao walioamua kukimbilia uwanjani kuomba msaada wa polisi kutokana na ile hofu ya kujeruhiwa.

Kipindi kama hiki mtu anaweza kupata majeraha wakati anatafuta namna ya kupata msaada au njia rahisi itakayompeleka eneo ambalo ni salama.

Kutokana na mazingira ya uwanja yanavyokuwa huwa na vizuizi ili usiende upande mwingine hivyo kuwalazimu kuruka au kupanda na kuchumpa upande mwingine hatimaye kujijeruhi.

Kutokana na wingi wa watu ni rahisi pia kujeruhiwa na vile vitu vinavyorushiwa ikiwamo viti, chupa, viatu, simu, mikanda na vifaa vingine ambavyo vinaweza kujeruhi vinapompata mtu mwilini.

Kuwemo katika vurugu kama hizi na kuwahi kujeruhiwa au kukoswakosa kujeruhi kunaweza kumwathiri mtu kisaikolojia hatimaye kutotaka kwenda tena katika viwanja vya soka.

FUNDISHO LIPO HAPA

Pamoja na nahodha wa Lionel Messi kuwalaumu Polisi kwa kuchukua hatua kali na kuanza kuwachapa mashabiki lakini bado polisi hao walionesha weledi wa kazi yao kwani dakika 30 tu hali ikawa shwari.

Vile vile umakini wa Polisi ndio pia ilichangia mashabiki kuwa salama kwani palikuwa na majeruhi mmoja tu aliyewahishwa hospitali na pia ndio waliondoa vizingiti kuruhusu mashabiki waliokimbilia uwanjani eneo salama kukwepa vurugu hizo.

Wakati Polisi wakifanya kazi zao pale uwanjani, watu wa huduma ya kwanza nao hawakuwa nyuma kwani haraka walionyesha utayari wa kutoa msaada wa dharura.

Columnist: Mwanaspoti