Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vita nzito makocha wazawa Vs wa kigeni Bara

Nabi Mgunda Pic Data Vita nzito makocha wazawa Vs wa kigeni Bara

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Duru la pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara limezidi kupamba moto kwa kila timu kucheza mechi 18 hadi sasa, lakini kubwa zaidi ni vita kati ya makocha wazawa na wageni kwenye kuwania ubingwa, nafasi za juu na kukwepa kushuka daraja.

Vita hiyo ni kama imebalansi kwani makocha wakuu wazawa wapo wanane sawa na wageni hivyo kila upande una uwezo wa kufanya maajabu kwa namna ya kipekee katika nafasi tofauti kama zilivyoainishwa hapo chini.

NNE BORA

Katika nafasi nne za juu hadi sasa baada ya kila timu kucheza mechi 18 kuna kocha mkuu mzawa mmoja peke yake aliyeifikisha timu yake hapo ambaye ni Juma Mgunda aliye nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 41.

Nafasi ya kwanza inashikiliwa na Kocha Mtunisia, Nassredine Nabi na chama lake la Yanga lenye alama 47, sita juu ya Simba iliyo nafasi pili na saba zaidi ya Azam yenye 37 inayonolewa na Mwingereza Kali Ongala.

Nafasi ya nne inashikiliwa na mgeni pia Mdachi Hans van der Pluijm, anayeinoa Singida Big Stars. Makocha wote hao bado wana nafasi za kuwania na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

NAFASI 5-10

Katika nafasi ya tano hadi 10 wazawa wamesimama imara na kuwatupilia mbali wageni kama ambavyo wao walivyofanya kwenye Top Four kwani wanne ni wazawa na wawili pekee ndio wageni.

Wazawa hao ni Salum Mayanga wa Mtibwa Sugar mwenye alama 24, Mecky Maxime wa Kagera Sugar aliye na pointi 23, sawa na Fred Felix ‘Minziro’ wa Geita Gold na mwingine ni Denis Kitambi wa Namungo mwenye alama 22, huku wageni wakiwa Mganda, Abdallah Mubiru wa Mbeya City na Mnyarwanda Thiery Hitimana wa KMC, waliopo nafasi ya tisa na 10.

Makocha wote hao kulingana na msimamo ulivyo hadi sasa bado wana nafasi ya kuwania ubingwa na wengine kuzifanya timu zao kumaliza nafasi za juu zaidi kama watapata matokeo chanya kwenye mechi zijazo.

NAFASI SALAMA

Kama ilivyo taratibu ya Ligi Kuu, kila mwisho wa msimu timu mbili hushuka daraja moja kwa moja na nyingine mbili hucheza mechi za mtoano ‘Play Off’ ya kuamua nani ashuke na nani abaki hivyo timu 12 tu ndizo zinakuwa salama.

Hadi sasa kwa namna msimamo ulivyo, baada ya timu 10 bora za juu, timu nyingine mbili zilizo kwenye nafasi ya kubaki salama ni Tanzania Prisons inayonolewa na Mkenya, Mathias Odhiambo na Dodoma Jiji chini ya Mmarekani, Melis Medo zote zikiwa na pointi 18 alama ambazo pia kutokana na msimamo ulivyo bado zipo kwenye mbio za ubingwa kwani zikishinda mechi zake zote zitafikisha alama 57 ambazo hadi sasa hakuna timu iliyozifikia.

PLAY OFF

Hapa kwenye timu ambazo kama ligi itamalizika leo zinaweza kucheza mechi za mtoano Play Off kwa maana ya zilizo nafasi ya 13 na 14 zote zinanolewa na wazawa.

Timu hizo ni Coastal Union iliyo chini ya Joseph Lazaro ikiwa na alama 15 nafasi ya 13 na Ihefu chini ya Juma Mwambusi iliyo na pointi 14 nafasi ya 14 na zote bado zinaweza kuwa bingwa kwani zikishinda mechi zote zitafikisha pointi 53 (Ihefu) na 54 kwa Coastal.

KUSHUKA DARAJA

Timu za mbili ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja hadi sasa zote ni za majeshi na moja inanolewa na mzawa na nyingine mgeni.

Ruvu Shooting ya Jeshi la kulinda Taifa (JKT), inayonolewa na mzawa Mbwana Makata na Polisi Tanzania inayonolewa na Mkongomani Mwinyi Zahera ndio zipo katika eneo hilo kila timu ikiwa na alama zisizofika 13 hadi sasa.

Vita hiyo ya makocha wazawa na wageni kuanzia nafasi ya kwanza hadi mkiani ni kama bado mbichi kwani kila timu bado ina nafasi za kuwania ubingwa lakini pia yoyote inaweza kushuka daraja.

Hiyo inaifanya ligi kuwa ngumu na yenye ushindani wa kutosha kutoka kwa kila timu na makocha hao jambo linalowapa burudani mashabiki na wadau wa soka nchini.

WASIKIE WADAU

Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni amesema makocha wazawa wanaweza kufanya vizuri na mapinduzi ya soka nchini kama wakipewa imani na kila kitu kwenye timu kama ilivyo kwa wageni.

“Mpira ni mchezo wa wazi, kila kocha ana mbinu zake lakini kwa ujumla huwezi kuwa bora kama haupewi kile unacho kihitaji.

“Naamini makocha wazawa wakipewa ushirikiano kama ilivyo kwa wageni wanaweza kufanya vizuri na kuishangaza,” alisema Kibadeni ambaye aliifikisha Simba kwenye fainali za Kombe la Caf barani Afrika mwaka 1993.

Kocha wa Ihefu, Mwambusi alisema makocha wazawa wanapitia changamoto kubwa kwenye timu lakini hupambana kadiri wawezavyo ili kupata mafanikio.

“Wazawa wanajua lakini wanapitia changamoto nyingi ambazo muda mwingine ni kuchukuliwa poa na viongozi wa timu hizo lakini kimpango wao hupambana na kuzipa timu mafanikio, kikubwa tukiaminiwa na kupewa nafasi zaidi naamini haku linaloshindikana,” alisema Mwambusi.

Mchambuzi wa soka, Edo Kumwembe naye alisema tofauti ya makocha wazawa na wageni; “Tofauti yao siyo kubwa sana lakini kila mmoja ana uimara na upungufu wake, kibaya zaidi watu wengi wanaamini wageni wanajua zaidi kuliko wazawa na kuwatukuza sana lakini wapo wazawa ambao pia ni bora,” alisema Edo.

Columnist: Mwanaspoti