Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vigogo 152 mtegoni miradi iliyokataliwa na Mwenge

Vigogo Pc Data Vigogo 152 mtegoni miradi iliyokataliwa na Mwenge

Tue, 19 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Ni mtego! Hivyo ndivyo inavyoweza kutafsiriwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuagiza uchunguzi wa kina na hatua stahiki dhidi ya watendaji wa Serikali waliohusika kutekeleza miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh65.3 bilioni, iliyokataliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Miradi hiyo kutoka sekta za elimu, maji, barabara na ujenzi wa majengo ya umma, ilikataliwa na kiongozi huyo, Luteni Josephine Mwambashi baada ya kuitilia mashaka kutokana na ama kukosa ubora kulingana na thamani halisi ya fedha au kuwapo kwa mkanganyiko kwenye taarifa ya matumizi ya fedha.

Taarifa za kukataliwa kwa miradi hiyo kutoka wilaya na halmashauri 38 za mikoa 19 nchini, zilitolewa kwa Rais Samia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa hafla ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere zilizofanyika uwanja wa Magufuli mjini Chato Oktoba 14.

Uchunguzi kufanyika

Baada ya kupokea taarifa hiyo pamoja na matokeo ya uchunguzi wa awali wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Rais Samia aliagiza uchunguzi wa kina na hatua stahiki dhidi ya watakaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine na sababu zilizochangia miradi hiyo kukataliwa.

Ukiwaodnoa watendaji na wakuu wa idara ndani ya halmashauri husika, kimahesabu, amri ya Rais Samia pia inaweza kuwanasa wateule wake 152 ambao ni wakuu wa mikoa 19, wakuu wa wilaya 38, makatibu tawala 19 wa mikoa na wenzao 38 wa wilaya pamoja na wakurugenzi watendaji wa halmashauri 38.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, miradi iliyokataliwa iko katika mikoa ya Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Simiyu, Mwanza, Pwani, Tabora, Morogoro, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Kigoma na Geita.

Wilaya 38 ambako miradi ilikataliwa ni Muheza, Lushoto, Kilindi, Kiteto, Hanang’, Rombo, Hai, Longido, Rorya, Butiama, Busega, Bariadi, Magu, Ilemela, Sengerema, Tabora, Igunga, Bahi, Chemba, Dodoma na Kongwa.

Waziri Mhagama alitaja wilaya nyingine kuwa ni Kilosa, Morogoro, Bagamoyo, Ilala, Kinondoni, Temeke, Kilwa, Masasi, Namtumbo, Nyasa, Sumbawanga, Mpanda, Uvinza, Kigoma, Kasulu, Mbogwe na Geita.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya miradi hiyo kukataliwa, Rais Samia alisema hiyo ni ishara kuwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri hawana ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

“Viongozi wa maeneo husika wanakuwa wapi wakati miradi inatekelezwa chini ya kiwango? Hii ni ishara kuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu….. Hii iwe ni onyo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema Rais, huku akiagiza idadi ya miradi yenye dosari ipungue wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022.

Miradi iliyokataliwa Dodoma

Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoa Dodoma, Tumsifu Mwasamale alilieleza Mwananchi kuwa miradi mitano kati ya 36 ya iliyotembelewa na Mwenge mkoani humo, ilikataliwa.

Kwa Wilaya ya Bahi, mradi uliokataliwa ni ule wa ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (Veta) wenye thamani Sh1.6 bilioni ambao licha ya taratibu za kifedha kukiukwa, pia kulikuwa na hitilafu kwenye nyaraka za uambatanisho.

Miradi mengine iliyokataliwa wilayani humo ni ujenzi wa ofisi ya mkurugenzi wenye thamani ya Sh4.1 bilioni na ule wa ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya sekondari ya Chinangali wenye thamani ya zaidi ya Sh110.1 milioni baada ya nyaraka zake kukutwa na dosari.

Miradi iliyokataliwa wilayani Kongwa ni ujenzi wa chuo cha Veta wenye thamani ya Sh1.8 bilioni pamoja na mradi wa kuchimba kisima cha maji wenye thamani ya Sh272.4 milioni, ambayo yote ilibainika kuwa na dosari katika mikataba na nyaraka za utekelezaji.

Akizungumzia agizo la Rais Samia kuhusu uchunguzi wa miradi hiyo, Mwasamale alisema tayari ofisi ya mkuu wa mkoa imewaandikia barua wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kutaka maelezo ya kuhusu miradi iliyokataliwa na hatua zilizofikiwa kutekeleza maagizo ya kiongozi wa mbio za Mwenge kuhusu miradi husika.

“Watu waliohusika kusababisha dosari hizo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwasamale

Jumla ya miradi 36 yenye thamani ya zaidi ya Sh41.8 bilioni iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Dodoma.

Mkoa wa Mtwara

Mkoani Mtwara, Mwenge wa Uhuru ulikataa kuzindua miradi miwili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi wenye thamani ya zaidi ya Sh500 milioni na mradi wa maji wa Chipole wenye thamani ya zaidi ya Sh400 milioni kutokana na mkanganyiko kwenye hesabu za fedha.

Mkuu wa wilaya ya Masasi, Claudia Kita alisema kuwa dosari zilizokuwepo ni pamoja na taarifa za fedha kutooana na nyaraka pamoja na kukosekana kwa baadhi ya nyaraka za matumizi. Hata hivyo, alisema tayari dosari zimerekebishwa na taarifa kuwasilishwa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mtwara, Enock Ngailo alisema taarifa za uchunguzi wa miradi hiyo tayari imewasilishwa makao makuu ya taasisi hiyo kwa uamuzi na maelekezo ya nini kifanyike.

Kilimanajaro

Kwa upande wa mkoa wa Kilimanjaro, Kiongozi wa mbio za Mwenge, Luten Josephine Mwambashi alikataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Longoi wilayani Hai baada ya kutilia mashaka taarifa za utekelezaji ikiwemo madai ya mradi kutokamilika licha ya zaidi ya Sh300 milioni kutumika.

Miradi iliyokataliwa Manyara

Mkoani Manyara, Mwenge wa Uhuru ulikataa miradi miwili ikiwamo ule wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya mkuu wa wilaya ya Kiteto na ujenzi wa zahanati ya Mogitu wilayani Hanang’ baada ya kutilia mashaka taarifa zake.

Akizungumzia uchunguzi wa taarifa za miradi hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu alisema ufuatiliaji umebaini kuwa hakukuwa na ufujaji katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Mogitu, isipokuwa aliyesoma taarifa ndiye alijichanganya wakati wa usomaji.

“Bado tunaendelea na uchunguzi kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya mkuu wa wilaya ya Kiteto,” alisema Makungu.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga alisema tayari kamati maalum ya uchunguzi inayojumuisha wataalam kutoka Takukuru, taasisi na idara mbalimbali ikiwemo ya ujenzi, imeundwa na uongozi wa mkoa kuchunguza utekelezaji wa mradi huo.

Mkoa wa Mara

Kwa mkoa wa Mara, kiongozi wa mbio za Mwenge alikataa kuzindua mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula Sekondari ya Robanda wilayani Serengeti wenye thamani ya zaidi ya Sh113milioni baada ya baadhi ya nyaraka zikiwamo za ununuzi na kupokea vifaa vya ujenzi kukosekana.

Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Seren

geti, Emmanuel Lighuda, alisema uchunguzi wa mradi huo unaendelea na ukikamilika taarifa zitawasilishwa mamlaka husika kwa uamuzi na hatua zaidi.

Aidha, kiongozi wa mbio hizo, alikataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi nchini (Veta) Wilaya ya Butiama kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi makubwa ya fedha yasiyoendana na thamani ya majengo.

Alisema banda la walinzi pekee hadi kukamilika litagharimu Sh10 milioni, thamani aliyosema ni kubwa kuliko ujenzi ulivyofanyika.

Kiongozi huyo alisema baadhi ya majengo yamejengwa kwa gharama kubwa.

“Hicho kibanda cha walinzi hapo kilipo kimegharimu zaidi ya Sh4 milioni na bado kimeombewa zaidi ya Sh5 milioni eti hadi kukamilika kitagharimu Sh10 milioni, sasa banda hilo pekee ligharimu Sh10 milioni kweli? Inatia shaka,” alisema.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa chuo hicho, alisema ujenzi huo unatumia mkataba wa zamani wa Sh1.6 bilioni tofauti na Sh2.2 bilioni zilizobadilishwa, huku akishangazwa kuona unaotumika ni mkataba wa zamani wakati kuna majengo yalibadilishwa kutokana na mkataba mpya.

Alieleza jinsi wasimamizi wa mradi huo walivyoshindwa kuonyesha nyaraka mbalimbali za mradi husika zikiwamo barua za kupokea fedha kutoka serikalini.

Soko la Samaki Kirumba Mwanza kwa mara nyingine

Kukataliwa kwa miradi pia kulishuhudiwa mkoani Mwanza baada ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, kukataa kuzindua mradi wa ujenzi wa mizani katika Soko la Kimataifa la Samaki Kirumba wilayani Ilemela uliogharimu zaidi ya Sh373 milioni.

Miongoni mwa sababu za mradi huo kukataliwa kwa mara ya pili mfululizo na mbio za Mwenge ni kugundulika kwa tofauti ya S95.1 milioni kati ya taarifa ya utekelezaji uliotaja gharama iliyotumika kuwa ni Sh373, wakati mahesabu yaliyofanywa na wakimbiza mwenge ulionyesha kuwa fedha zilizotumika ni Sh261 milioni.

Kwa mara ya kwanza, mradi huo ulikataliwa Septemba Mosi, 2018 na aliyekuwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru wakati huo, Charles Kabeho baada ya kubaini dosari.

Miradi ya Dar es Salaam

Mkoani Dar es Salaam, miradi mitano kati ya 46 iliyotembelewa na mwenge ilikataliwa na baada ya kubainika kuwa na kasoro.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)-Mwenge ambayo ni kati ya barabara tano zilizopo katika fungu la saba zinazojengwa mkoani humo zenye urefu wa kilomita 7.8 zilizojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh 26 bilioni.

Soko la Bwawani-Mwananyamala lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh1.3 bilioni na kiwanda cha mbolea cha Mabwepande huku Takukuru ikiagizwa kuichunguza.

Mradi mwingine uliokataliwa ni ujenzi wa barabara za Nzasa-Kilungule-Buza wenye thamani ya zaidi ya Sh19 bilioni uliokutwa na dosari ya wananchi waliohamishwa kupisha ujenzi kutoshirikishwa huku pia kukiwa na ukinzani katika nyaraka ikiwemo mikataba ya ujenzi.

Kiongozi wa mbio za Mwenge pia alitilia mashaka taarifa za zaidi ya Sh3 bilioni kudaiwa kutumika kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi huo baada ya kukosekana kwa hati za malipo wala taarifa ya taratibu zilizotumika kufanya malipo hayo.

Mkanganyiko mwingine uliobainika kwenye mradi huo ni mkataba kuonyesha kuwa gharama ya ujenzi ni zaidi ya Sh19 bilioni wakati maelezo ya wataalam yanadai ujenzi utagharimu Sh16 bilioni, huku kiasi kilichobaki cha Sh3 bilioni kitatumika kujenga stendi lakini mkataba ukiwa hauonyeshi mchanganuo huo.

Taarifa nyingine iliyoibua utata ni zile za mradi kugharimu zaidi ya Sh22 bilioni kwa maelezo kwamba kiasi cha Sh19 bilioni ni gharama kabla ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Imeandikwa na Peter Saramba na Saada Amir (Mwanza) Joseph Lyimo (Manyara), Sharon Sauwa (Dodoma), Bahati Chume (Kilimanjaro), Mwanamkasy Mahendo (Mtwara), Anthony Mayunga (Mara), Bakari Kiango na Aurea Simtowe

Columnist: mwananchidigital