Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Van Gaal anapopambana na nchi ya ahadi ya Messi

Van Gaal X Messi Ligi Van Gaal anapopambana na nchi ya ahadi ya Messi

Mon, 11 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hadithi inayosisimua sana wakati mwingine inafanana na uongo. Waingereza katika ubora wao wa lugha ya Kiingereza huwa wanatumia neno ‘fairy tale’. Kwamba simulizi imesisimua sana kisha inaonekana kama vile ni igizo.

Nilikuwa namsoma Louis Van Gaal mahala. Mara hii umemsahau? Yule kocha wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi. Anaamini kwamba Kombe la Dunia 2022 lilipangwa kwa ajili ya Lionel Messi kulitwaa kabla hajastaafu soka. Anaamini kwamba Fifa na wakubwa wengine wa mpira walitaka Messi atwae Kombe la Dunia kabla hajastaafu. Nimesikia minong’ono hii mahala kabla ya Van Gaal kudai hili. Sijashangazwa sana na Van Gaal katika hili kwa sababu ni hasimu wake Messi. Waliwahi kutiana vikumbo katika pambano la robo fainali wakati Messi akielekea kutwaa Kombe la Dunia.

Hivyo sijashangazwa sana na Van Gaal. Ana sababu nyingi. Nimeshangazwa tu na baadhi ya watu walioendelea kuamini hisia kwamba huenda Fifa walitamani kumuona Messi akitwaa Kombe la Dunia pale Qatar. Inawezekana kuna watu binafsi ndani ya taasisi ya Fifa wao kama binadamu walitaka Messi atwae kombe hilo, lakini siamini kama kama taasisi walikuwa na ajenda hiyo.

Mechi ya kwanza Argentina walinyooshwa na Saudia Arabia. Dunia ilibaki mdomo wazi. Kama ambavyo safari nzima ya Messi kwenda kutwaa Kombe la Dunia ilivyoshangaza, basi ndivyo ambavyo ushindi wa Saudi Arabia katika pambano hilo ulishangaza wengi.

Huwa inatokea katika mechi moja au huwa inatokea katika michuano fulani kwa timu fulani kutwaa kombe bila matarajio ya wengi. Kama ambavyo Senegal waliifunga Ufaransa katika Kombe la Dunia 2002, basi ndivyo hivyo Wagiriki waliishangaza dunia 2004 kwa kutwaa taji la Euro pale Ureno.

Kama ambavyo Cameroon waliishangaza dunia 1990 kwa kumchapa bingwa mtetezi Argentina, basi ndivyo ambavyo Leicester City waliishangaza dunia kwa kutwaa taji la Ligi Kuu England 2016. Mambo haya hutokea katika mechi moja ya soka au michuano fulani.

Baada ya kichapo kutoka kwa Waarabu ambacho ni wazi kwamba watu wengi waliamini kwamba Messi na Argentina hawana chao pale Qatar, ghafla wakajikusanya na kucheza pambano lijalo dhidi ya Mexico. Wakashinda mabao 2-0 bila ya utata wowote ule. Wamexico wamepotea katika soka. Haishangazi kuona wakifungwa na timu kubwa.

Bado hakuna aliyeona kwamba Argentina wangeweza kuchukua kombe hilo licha ya ushindi huu. Hofu ilikuwa kwa Wafaransa na Wabrazili, hasa kwa namna ambavyo walikuwa wanatandaza kandanda. Ungeweza kudhani kwamba Cristiano Ronaldo alikuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa Kombe la Dunia kuliko Messi.

Wakacheza na Poland kisha Australia. Nani anaweza kushangaa Argentina kushinda mechi hizi? Isingeshangaza sana. Kama Argentina ingefungwa mechi hizo ingeweza kuwa habari nzuri lakini wao kushinda haikuwa habari ya kushangaza. Hapa pia ilidhihirika kwamba Argentina walikuwa na bahati ya kupita katika njia nzuri. Sawa, unaweza kufungwa na Saudi Arabia kwa bahati mbaya lakini kama ukifungwa tena na Poland au Australia basi haustahili kutwaa Kombe la Dunia. Wakati mwingine tatizo sio mwanzo mbaya bali ni mwendelezo mbaya.

Mwaka 1990 licha ya kuchapwa na Cameroon katika mechi ya ufunguzi, lakini Argentina walirudi katika mwendelezo wa ubora kiasi cha kuweza kutinga katika fainali ambayo kwao ilikuwa ya pili mfululizo. Hata hivyo walichapwa na Ujerumani Magharibi katika pambano la kisasi. Kumbuka 1986 Argentina iliifunga Ujerumani Magharibi katika pambano la fainali pale Mexico.

Baada ya hapo Argentina walicheza dhidi ya Uholanzi. Hapa ndipo ilipokuja vita ya Messi na Van Gaal. Walivaana katika mstari wa benchi la ufundi la Uholanzi lakini wakapambana katika dakika 90 za uwanjani. Pambano lilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Hii ilikuwa nafasi ya yeyote kuichukua. Huwa inasemwa kwamba penalti zinakoswa. Argentina walipata nne halafu Uholanzi wakapata tatu. Walikosa kwa sababu ya Fifa? Hapana. Walikosa wenyewe. Walikuwa wamesimama hatua 12 kutoka katika lango la Emiliano Martinez. Kushindwa kumfunga zote halikuwa kosa la Fifa.

Ikaja mechi ya nusu fainali dhidi ya Croatia. Hawa jamaa wanaijulia michuano ya Kombe la Dunia, lakini hawajui namna ya kuimalizia. Mwaka 1998 wakiwa chini ya Davor Suker walifika nusu fainali wakacheza dhidi ya mwenyeji Ufaransa. Waliongoza katika pambano lile lakini Lilian Thuram alichomoa bao moja na kisha kufunga jingine la ushindi.

Mwaka 2018 walicheza fainali pale Russia dhidi ya Ufaransa, lakini wakageuzwa kuwa watoto wadogo. Haikushangaza kuona safari hii tena katika nusu fainali wakichapwa na Argentina. Pambano lao la nusu fainali halikuwa na maajabu makubwa kwao. Halafu ikaja fainali. Wafaransa walikuwa ovyo wakafungwa mabao mawili ya haraka haraka. Hakukuwa na bao la dhuluma. Lakini kuna kesi ya mchezaji anayeitwa Kolo Muani. Alishindwa nini kuukwamisha mpira katika nyavu za Martinez dakika ya 118 ya mchezo? Alikuwa ametazamana na Martinez ana kwa ana. Dakika chache tu kabla mwamuzi hajapuliza kipenga. Alishindwa nini kufunga?

Fifa wangefanya nini kama Kolo angefunga? Hakuna ambacho wangeweza kufanya. Baada ya hapo mechi ikaenda katika matuta. Wafaransa wakapiga penalti zao kizembe. Mmoja baada ya mwingine akapiga penalti yake kizembe huku Messi na wenzake wakipiga kwa usahihi.

Mwisho wa siku hakuna timu ambayo imewahi kutetea Kombe la Dunia tangu mwaka 1962 ilipotetea taji ililotwaa awali 1958 ikiwa nchi ya pili baada ya Italia iliyobeba 1934 na 1938. Haikushangaza kwamba Wafaransa walishindwa kutetea taji. Endapo Messi na wenzake wasingemalizia kazi yao, basi Wafaransa wangekuwa taifa la kwanza kutetea Kombe la Dunia. Bahati mbaya kwao Mungu mpaka sasa hajatuletea taifa hilo. Mwisho wa siku aliamua tu kututengenezea mwisho mwema wa Messi. Inaitwa fairy tale. Kwamba baada ya kilio cha wengi kumuona mmoja kati ya Messi au Ronaldo akitwaa Kombe la Dunia ikaangukia kwa Messi ambaye katika ubora wake amewahi kuondoka akilia pale Maracana, Brazil baada ya kukosa kombe dhidi ya Wajerumani.

Ni hadithi nzuri katika maisha yake ya soka. Ni hadithi nzuri kwa mashabiki wake. Ni hadithi nzuri kwa kila anayeupenda mchezo wa soka. Wachache wamechukia kwa sababu ya upinzani wake na Ronaldo lakini ukweli ni kwamba dunia imeshuhudia mwanasoka bora zaidi kuwahi kutokea akitwaa Kombe la Dunia. Ametwaa akiwa na miaka 35. Ndoto nzuri iliyoishia pazuri. Bahati pia ilimuandama katika michuano yenyewe.

Fikiria namna ambavyo alishindwa kutwaa Kombe la Dunia akiwa na wachezaji bora zaidi ya hawa. Alishindwa kutwaa Kombe la Dunia akiwa na Gonzalo Higuain, Carlos Tevez, Sergio Aguero, Javier Mascherano na wengineo. Ametwaa akiwa na wachezaji wa kawaida tu.

Ingekuwa katika maandiko basi Messi amefika katika nchi ya ahadi kama Mussa. Haikuwa kazi rahisi sana, lakini Van Gaal anahakikisha basi anapambana. Sioni kama anachosema kina ukweli wowote lakini yeye sio mwanadamu wa kwanza kupambana na wanadamu wengine ambao Mungu aliwafikisha katika nchi zao za ahadi.

Columnist: Mwanaspoti