Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VYAMA VIJITAMBULISHE KWA UMMA ITIKADI ZAO

VYAMAMAMAMA AA VYAMA VIJITAMBULISHE KWA UMMA ITIKADI ZAO

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HAPA nyumbani, nchi yetu inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu. Nina bahati ya kutembea mijini na vijijini.

Huko ninakotembea nazungumza na watu pia. Inanisaidia kuupima upepo wa kisiasa unavyovuma. Nina bahati pia ya kushuhudia chaguzi kuu tano tangu ule wa 1995.

Nimesoma pia historia ya chaguzi za nchi hii hata kabla ya Uhuru wa Tanganyika. Ni pamoja na kampeni zake zilivyoendeshwa. Kuna yaliyo tofauti kwa mwaka huu na nyakati hizo, lakini, kuna yenye kufanana pia.

Kufahamu mwelekeo wa chaguzi Tanzania ni vema mtu akaiangazia ‘electoral base’ ya nchi kwa maana ya ngome za wapiga kura. Kwenye siasa, kila chama na mgombea huwa na ngome ya wapigakura wake.

Ili tuweze kujadili vema hili, ni vema tukubaliane kwanza kuwa, asilimi 80 ya Watanzania, wapigakura, wanaishi vijijini. Kwa mantiki hiyo, tuseme, kwa hesabu rahisi kuwa, robo tatu ya wapigakura iko maeneo ya vijijini.

Ina maana ya asilimia 75 ya wapigakura. Robo iliyobakia kwa maana ya asilimia 25, iko maeneo ya mijini.

Ngome ya wapigakura ya CCM iko vijijini, ni asilimia hiyo 75. Sasa basi, ninachokiona na ni mtazamo wangu binafsi ni kuwa, CCM katika hali zote inaweza kupoteza robo moja ya ngome yake ya kura za vijijini.

Hivyo, ikabaki na robo mbili. Ni kwa sababu, hata katika maeneo yale yanayosemwa kuwa CCM inakabiliwa na upinzani mkubwa, kama mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara, bado kwenye maeneo ya vijijini kwenye mikoa hiyo CCM inaonekana iko imara.

Kwa hali ilivyo sasa, CCM inaweza kupoteza asilimia 15 tu ya kura za mijini, lakini ina uwezo wa kupambana na kupata zaidi ya asilimia 15 za kura za mijini.

Tafsiri hapa, upinzani haupaswi kubweteka na sapoti wanayoipata mijini kupitia mikusanyiko mikubwa kwenye mikutano yao, CCM wana uzoefu wa miaka mingi wa kimbinu na kimikakati ya kuzitafuta kura hata kwenye mazingira ya kubanwa sana.

Lakini, wapanga mikakati wa CCM, bila shaka nao hawalali katika kuhakikisha wanapata walau asilimia 15 ya kura za mijini. Nini kinakosekana kwa sasa? Kinachokosekana kwa sasa ni misingi ya kiitikadi katika kuendesha kampeni za kisiasa.

Vyama vimejikita katika kutoa ahadi. Lakini, katika siasa, lililo kubwa ni itikadi. Kama chama kinafuata itikadi ya kibepari, basi, kuahidi kutoa elimu na afya bure kunakinzana na misingi ya itikadi husika.

Katika ubepari hakuna cha bure. Vyama lazima vijipambanue kiitikadi. Katika itikadi ya kijamaa, huduma za kijamii kama vile elimu na afya ni kawaida kutolewa bure au kwa gharama nafuu sana.

Mfano nchini Cuba, nchi ya kijamaa, kila mtoto anayezaliwa kwenye nchi hiyo kuna vitu viwili anavyohakikishiwa na taifa lake kuvipata bure na kwa ubora mpaka atakapokufa navyo ni elimu na afya.

Fedha za kugharamia huduma hizo hutokana na kodi inayokusanywa kutokana na shughuli za uzalishaji. Wajamaa wanaamini katika kuwatoza kodi zaidi wenye nacho ili kuwamegea wasio nacho.

Ndio mantiki hapa, kwamba anayetaka urais ni vema akawaonesha wazi wapigakura kwamba, serikali yake itafuata misingi gani ya kiitikadi katika kuendesha uchumi wa nchi.

Hapa kwetu vyama na wagombea wameshindwa kujipambanua katika itikadi. Mgombea anayetokea kwenye chama chenye sera za kibepari anasikika kama anatoka kwenye chama cha kijamaa na kinyume chake.

Wakati mwingine unaingiwa mashaka, kama kweli vyama vina itikadi zenye kueleweka. Inatokea pia, kuwa itikadi ya mgombea mara nyingi haionekani wazi anapoongea.

Duniani hapa chama cha kisiasa chenye nguvu kinatokana na kazi ya timu iliyoandaliwa vema. Si kazi ya mtu mmoja. Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni uwingi na ubora wa makada wake.

Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala si nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama. Chama chenye makada wengi wenye kuielewa itikadi, malengo na shabaha ya chama, huwa hakimtegemei mtu mmoja katika kuwapo kwake.

Hakimtegemei mtu mmoja katika kufanikisha ushindi wa chama. Hakimtegemei mtu mmoja katika kuhamasisha wanachama au umma. Katika kampeni tunazokwenda nazo tunaona kuwa, baadhi ya vyama havina kabisa hazina ya makada.

Kazi ya kuwahamasisha wapigakura inapaswa kufanywa kuanzia ngazi za chini kabisa na huko chama kinahitaji makada wa kuifanya kazi hiyo. Hata kama uchaguzi huu utapita, vyama vijizatiti kuifanya kazi hiyo ili kujiandaa kwa chaguzi zijazo.

Na hatari ya kukosekana itikadi za vyama zenye kueleweka ni uwezekano wa kama tunavyoona sasa. Hali ya kujipenyeza kwa nguvu hasi zenye kutaka kuisukuma jamii kuelekea kwenye machafuko.

Ni bahati mbaya sana siku hizi; unaposema au kuchambua mambo, haraka kuna wanaokimbilia kutafuta kabati la kukupachika; uchama, u-dini, u-kabila na mengineyo.

Tumelisahau kabati muhimu sana, nalo ni kabati la Tanzania. Na hakika, katika kila tuyafanyayo tutangulize kwanza maslahi ya nchi yetu. Nahitimisha.

Columnist: habarileo.co.tz