Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uzuri wa Tanzania ni katika misingi ya uongozi uliotukuka

002bdae3348f16c6e5adf7825c03389f.png Uzuri wa Tanzania ni katika misingi ya uongozi uliotukuka

Thu, 29 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

*Vijana wa leo wanalo la kujivunia kuijenga nchi yao?

TANZANIA ni taifa lenye utitiri wa mema mengi ya asili yaliowekwa si na mwanadamu bali na Mungu mwenyewe yakisimamiwa vyema na viongozi wa nchi wakiwamo waasisi wa taifa hili.

Viongozi na waasisi hao ni wengi lakini kwa uwakilishi historia ya nchi katika amani na utulivu haiwezi kukamilika bila kumtaja Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume wa Zanzibar. Viongozi hawa ndio hasa mfano wa kuigwa katika vita dhidi ya ukoloni, umaskini na siasa chafu dhidi ya nchi za Afrika.

Ukiangalia maliasili ya mbuga na hifadhi za wanyama, uoto wa asili, mito, mabonde, maziwa, mabwawa, bahari, milima, vyakula, nyimbo, sanaa na ngoma za asili. Vyote hivi vinaingia katika utamaduni wa asili unaobeba dhima nzima ya maana ya nchi huru na watu wake.

Ni nchi iliyojaliwa kuwa na makabila zaidi ya 124 lakini watu wa makabila hayo wote wakiunganishwa kwa umoja, mshikamano, amani na upendo kupitia urithi wa kimaadili na siasa safi pamoja na lugha adhimu ya Kiswahili.

Uzuri wa Tanzania unaweza kuuona unapokwenda nje ya nchi hii. Unapojionea maisha, asili na utamaduni wa watu wa nchi hiyo unavyowatenga watu kwa makabila, dini na rangi ndipo utafahamu umuhimu wa kuthamini na kuitunza Tanzania.

Hiki ndicho kimenisukuma kusema bila kigugumizi kwamba, ifikie mahali Watanzania tujivunie kujenga nchi yetu kwa nguvu na juhudi zetu kwa kujiuliza maswali muhimu namna ninavyochangia katika maendeleo yake.

Nchi hii mpaka hapa ilipo mababu zetu na wengi huko nyuma waliumia mpaka kufika ilivyo leo. Wengine walipoteza Maisha huku wengi wakapata ulemavu wa kudumu kwasababu tu ya kuikomboa nchi. Walitumia muda mwingi kuijenga nchi kisiasa kwanza kwa kuimarisha umoja na mshikamano wa watu na wa kifikra kabla ya kuangalia shughuli za maendeleo.

Watu waliumia kudai uhuru wa nchi kutoka kwa wakoloni Waingereza mpaka nchi kuwa huru mwaka 1961. Miaka ya 1970 na 1980 wakati dikteta Nduli Idi Amin wa Uganda alipojaribu kuvamia nchi hii, kizazi cha miaka hiyo kilipambana bure bila kulipwa senti yoyote kulinda hii nchi.

Watu walipoteza maisha yao, mali zao na familia zao kwasababu ya Tanzania bila ujira na kulipwa na yeyote mpaka tukamshinda Idi Amin katika vita hiyo iliyokuwa kati yam waka 1978 hadi 1979.

Athari kubwa za vita hii zilijidhihirisha katika miaka ya 1980 wakati uchumi wan chi ulivyoyumba na waliokuwepo nyakati hizo wanakumbuka mgao wa vyakula na huduma duni za kijamii zilizokuwepo.

Baada ya vita na Idd Amini, nchi ikaingia kwenye njaa kubwa sana na anguko la uchumi, watu wakakubali kufunga mikanda bila kula siku nzima kwasababu ya Tanzania. Fikilia maumivu haya waliyoyapata wenzetu huko nyuma kwasababu ya Tanzania hii unayoiona leo bila kulipwa na yeyote.

Najiuliza mimi na wewe, kijana wa kizazi hiki unajivunia nini mpaka sasa? Kama Mababu zetu walikubali mpaka kufa na kupoteza kila kitu chao kuijenga Tanzania unayoiona leo, wewe wa kizazi hiki unajivunia nini?

Sisi kizazi cha leo tunajivunia nini? Tumeikuta Tanzania iliyojengwa kwa damu na jasho za mababu zetu huko nyuma. Watu walipoteza maisha yao, kuumia na kufungishwa mikanda mpaka unaiona Tanzania hii ya leo, kwanini usijivunie kuwa sehemu ya ujenzi wa nchi yako na kuzuia kutumika kwa siasa chafu kuangamiza nchi yako?

Hivi kizazi chetu hiki cha leo utajivunia lipi la kujitoa ili mradi nchi isonge, mababu zetu walishakufa, kupoteza viungo vyao na mali zao kwa jasho na damu, nyakati hizo simulizi rasmi za kihistoria zinaeleza jinsi walivyoziacha hata familia zao, wazazi, wake na watoto wao kwa ajili ya Tanzania.

Kizazi cha leo kinapaswa kujiuliza maswali nimeifanyia nini nchi yangu na si nchi yangu imenifanyia nini. Natamani vijana waliotayari kujibana na kuona Fahari hiyo ya kushiriki kuijenga nchi.

Amani, utulivu na maendeleo tunayoyaona leo na kujigamba nayo pamoja na kujivunia kila mahali kwamba nchi yetu ina amani, mshikamano, umoja na maendeleo, ni matokeo ya jasho na damu la mababu zetu huko nyuma kujenga misingi imara na ya kudumu ya Tanzania ijayo. Wewe unajivunia nini?

Iko falsafa moja alipenda sana kuitumia Rais mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (marehemu) katika hotuba zake nyingi hasa zilizogusa masuala ya ukombozi wa Afrika, akisisitiza ukombozi wa fikra na kuweka bayana kwamba, Afrika itajengwa na Waafrika wenyewe, Tanzania ikiwemo.

Ukitegemea nchi ijengwe na wengine hatari yake ni kukubali fikra na matakwa ya mtu yenye masharti ya kumnufaisha yeye badala ya nchi husika.

Nchi itaburuzwa na kamwe dhamira ya dhati inayoelezwa na kila mgombea wakati wa uchaguzi wa kisiasa unaotoa ridhaa ya kikatiba ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na ahadi ya yale watakayoyatekeleza ikiwa watapewa ridhaa, haitafikiwa.

Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni serikali ilianza utekelezaji wa tozo ya miamala ya simu kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii kama barabara hasa vijijini. Hakuna asiyejua kuwa Rais Samia ameagiza wizara zinazoguswa na suala hilo ikiwemo Wizara ya Fedha na Mipango, mawaziri kukaa na kuangalia namna ya kupunguza kiwango.

Kauli ya Rais Samia haimaanishi kufutwa kwa tozo hiyo iliyo kwa mujibu wa sheria, bali kufanyika marekebisho ya gharama zinazokatwa wananchi kutokana na malalamiko kuwa ni kubwa. Hili naona ni jema sana kwa kuwa limebeba hoja ya ujenzi shiriki wa nchi ninaouzungumzia hapa.

Ni kheri kuchangishana kidogo kidogo sisi wenyewe tusaidie ujenzi wa nchi yetu kwani waswahili walisema haba nah aba, hujaza kibaba. Hiyo hela inaenda kwenye mfuko wa pamoja (Solidarity Fund) na moja kwa moja kwenye shughuli za maendeleo.

Watanzania tunapaswa kujisikia fahari kutoa kidogo ili kitatue kero zetu maeneo mbalimbali hasa vijijini. Katika hili, viongozi wanapaswa kusimamia ipasavyo kupata matokeo chanya ya matumizi ya fedha husika.

Ni huzuni na kilio cha kila kiongozi mwenye dhamira njema kwa mjamzito kufika hospitalini akose dawa na huduma bora. Maeneo yasio na barabara nzuri hata kama ni za udongo maendeleo kufika huko kwa haraka ni ndoto.

Changamoto ya watoto wetu baadhi kukosa mikopo na kusoma kwenye mazingira magumu huko vijijini ya umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 20 kutoka nyumbani hadi shuleni ni kubwa, inahitaji uwajibikaji wa kila mtu.

Ni wakati sasa wa kila Mtanzania kujisikia fahari kuwa sehemu ya kutatua kero za jamii ambazo zinakugusa maisha ya kila mtu.Tukumbuke kuwa nchi hii itajengwa na sisi wananchi wenyewe na kwa pamoja tutaweza.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa namba ya simu 0657475347

Columnist: www.habarileo.co.tz