Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uzalendo na safari ya Tanzania kujenga uchumi mkubwa

29a117b38264af828450d922bd1d35fa Uzalendo na safari ya Tanzania kujenga uchumi mkubwa

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA baadhi ya watu, neno uzalendo mara nyingine limekuwa likichanganywa kimatumizi na neno uraia, japo maneno hayo yana tofauti kubwa.

Mtu anaweza kuwa raia wa taifa fulani, lakini asiwe mzalendo katika taifa hilo. Kimsingi, uzalendo ni hali ya kuwa na mapenzi ya dhati, kuthamini, kutanguliza na kutetea maslahi ya taifa, kuliko mtu au kitu chochote.

Mtu mzalendo huwa tayari kulifia taifa lake huku akitetea usalama, amani, maliasili au uchumi wa taifa hilo.

Katika sayari hii ya dunia, watu wanatofautiana katika namna mbalimbali kama vile kijiografia, kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi na katika namna nyingine za uendeshaji maisha yao ya kila siku.

Kwa kuwa mataifa tofauti hutofautiana mambo mengi ikiwamo historia, kila taifa hujikuta likihitaji kutunza historia na tunu zake nyingine pamoja na misingi ya uundwaji wa taifa husika.

Mataifa na jamii nyingi ulimwenguni hupenda na kuhitaji kuona utambulisho wake, historia na misingi ya kuanzishwa na kuwepo kwake, vinalindwa dhidi ya uharibifu au mwingiliano na jamii na mataifa ya kigeni.

Na hapa ndipo dhana ya uzalendo ilipoibuka. Taifa hujengwa kwanza na ndipo watu wake huibuka na hisia za kupenda, kulinda na kutetea taifa lao kuliko mtu au kitu chochote (uzalendo).

Kadiri nchi au taifa linapopiga hatua kwenda mbele kimaendeleo, ndivyo linavyotoa mwanya mkubwa wa mwingiliano na mataifa mengine na ndivyo masuala ya utaifa na uzalendo yanavyopewa kipaumbele na kuzingatiwa zaidi.

Kwa mfano, tangu Karne za 15 hadi 19 baada ya Kristo, ulimwengu ulishuhudia maendeleo na mapinduzi makubwa katika nyanja za teknolojia, kilimo, viwanda na ukuaji wa mitaji barani Ulaya katika nchi kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Ni katika nyakati hizo pia, Ulaya ilishuhudia kuibuka kwa dhana ya utaifa na uzalendo. Hali hii kwa kiwango kikubwa ilitokana na ushindani mkubwa baina ya jamii za Bara la Ulaya, hivyo kufanya kila taifa kujiimarisha na kulinda maslahi.

Hiyo ni hali ambayo haikuweza kuepukwa. Hapo ndipo taifa moja liliibuka na kutunga sheria zilizolinda vitu kama vile viwanda na biashara kwa kutoza kodi kubwa bidhaa zilizoingia na kuzipa nafuu zile zilizozalishwa ndani ili kulinda soko na viwanda vya ndani maarufu kama protectionism policy.

Sera hizi hazikuwahi kukoma, zinashuhudiwa mpaka leo. Kwa mfano, Taifa la Marekani limekwenda mbali zaidi na kuanzisha vituo vyake nje ya nchi katika mataifa kama vile Korea Kusini, Kenya na Afrika Kusini ili kulinda maslahi yake hasa kiuchumi.

Nchi ya China pia ina kituo kama vile vya Marekani nchini Elitrea katika eneo la Pembe ya Afrika.

Hali hii inaikumba pia Tanzania kwa kuwa siyo kisiwa na hivyo haina namna ya kuepuka suala la kuimarisha sera zake hasa katika kuhimiza masuala ya utaifa na uzalendo hasa nyakati hizi tunapoelekea Tanzania ya viwanda.

Ujenzi wa Uzalendo Tanzania

Kwa kiasi kikubwa uzalendo ulijitokeza waziwazi kwa Watanzania kutoka jamii mbalimbali walipoungana na kujitokeza hadharani kupinga kuingia kwa utawala wa kigeni ulioletwa na Wajerumani mwishoni mwa Karne ya 19.

Awali, jamii nyingi zilipinga uvamizi huo kupitia makundi madogomadogo kama vile Wahehe chini ya Mtwa Mkwawa, Wanyamwezi wakiongozwa na Mtemi Mirambo na Wakibosho chini na Mangi Sina.

Baadaye mapambano yalichukua sura mpya pale makundi mbalimbali hasa Kusini Mashariki mwa iliyokuwa Tanganyika (Tanzania Bara ya leo) kama vile Wamakonde, Wamakua, Wazaramo, Wangoni, Wapogoro, Wabena, Wangindo, Wandendeule na Walugulu walipounganishwa na dhana ya maji iliyoanzishwa na Kinjekitile Ngwale na kupigana na Wajerumani kwenye vita ya Majimaji mwaka 1905-1907.

Hata hivyo, jamii hizo zilishindwa katika vita hivyo kutokana na sababu nyingi kubwa zaidi zikiwa ni ukosefu wa teknolojia ya uhakika ya kivita, maandalizi na ushirikiano hafifu.

Hata hivyo, mapambano ya kupinga kutawaliwa yaliendelea kupitia vyama vya ushirika vya wakulima kama vile Kilimanjaro Natives Co-operative Union (KNCU) cha Kilimanjaro, vyama vya wafanyakazi kama vile Chama cha Wafanyakazi wa Tanganyika kilichofahamika kama Tanganyika African Association (T.A.A ) na vyama vya kisiasa kama vile Tanganyika African National Union (TANU).

Harakati hizo zilifanyika kati ya miaka ya 1920 na kuhitimishwa Desemba 9, 1961 Tanzania Bara (Tanganyika) ilipopata uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.

Baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza, juhudi za ujenzi wa taifa jipya ziliimarishwa zaidi ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya kitaasisi, kisekta na hata kimuundo ili kuboresha na kuifanya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ili isawili mahitaji ya wakati husika.

Mabadiliko makubwa ya kimfumo yalifanyika ili kuondokana kabisa na fikra za kiukoloni ambao mizizi yake ilihitaji kung’olewa. Mwalimu Nyerere, viongozi wengine na wananchi kwa jumla waliendelea kujenga na kuimarisha uzalendo kwa namna anuai.

Moja kati ya njia hizo zilizotumika ni kukitumia lugha ya Kiswahili na kuifanya kuwa lugha ya taifa, hivyo kuwafanya Watanzania kuwa wamoja na kujali Utanzania wao zaidi kuliko utambulisho wa koo zao ndogondogo zilizopewa jina la “makabila” neno linalohitaji umakini mkubwa katika kulitumia ikizingatiwa historia yake.

Jambo hili lilisaidia na hata sasa linaendelea kulisaidia taifa kuwa na umoja, amani na maendeleo, hata katika nyakati hizi za utandawazi na sasa taifa linapoelekea uchumi wa kati mambo haya bado yanahitajika.

Utaifa na uzalendo ulishuhudiwa ukijengeka zaidi hasa pale Tanganyika ilipoungana na Zanzibar na kuzaa Taifa la Tanzania, Aprili 26, 1964. Muungano huu ulitanguliwa na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 yaliyoung’oa utawala wa ki-sultani visiwani humo.

Juhudi kubwa zilizofanywa na Mwalimu Nyerere wa Tanganyika na Abeid Amani Karume wa Zanzibar ziliwezesha kuzaliwa kwa Tanzania kama taifa, hivyo watu wake kuungana na kushirikiana kizalendo zaidi.

Muungano na ushirikiano unaohitaji zaidi katika nyakati hizi ambapo Taifa linapigana vita vya kujikomboa kutoka kwenye unyonge na utegemezi; na kujenga mifumo itakayonufaisha zaidi watu wake kuliko watu wengine.

Chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere na Abeid Karume, utaifa na uzalendo viliendelea kukita mizizi kwa kufanya kila idara ya serikali na chama kuwa na sura ya kitaifa.

Mifumo, sekta, idara na nyanja kama vile elimu, jeshi, afya, siasa na uchumi vilijengwa kwa kuzingatia na kujali utu, usawa, demokrasia na kujali haki za kibinadamu, utawala wa sheria na maendeleo ya watu.

Kwa mfano, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, Binadamu na Maendeleo cha mwaka 1974 anasisitiza kuwa, maendeleo yanatakiwa yajikite kwa watu kupitia uboreshaji wa afya zao, umri wa kuishi, elimu na kipato.

Kupitia mambo haya karibu kila Mtanzania alijihisi ni sehemu ya nchi yake na hivyo kuimarisha utaifa na uzalendo.

Uzalendo Azimio la Arusha

Mwishoni mwa miaka ya 1960, uzalendo uliimarika zaidi hasa baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967.

Azimio hili lililiingiza taifa kwenye mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea. Misingi ya azimio hili ilikuwa ni pamoja na watu kuishi kwa upendo, udugu, kufanya kazi kwa bidii, usawa na hivyo kufanya uzalendo kujikita mizizi katika taifa la Tanzania ukiachilia mbali changamoto zake.

Uzalendo wakati wa vita

Baadaye, mwishoni mwa miaka ya 1970 dunia ilishuhudia Watanzania wakiungana na kupambana dhidi ya uvamizi wa Nduli Idd Amin Dada wa Uganda.

Vita dhidi ya Idd Amin aliyeivamia sehemu ya Tanzania, mkoani Kagera na kutangaza kuwa ni mali ya Uganda vilipiganwa kuanzia mwaka 1978 na kumalizika mwaka 1979.

Ukiachilia mbali matatizo mbalimbali yaliyolikumba taifa la Tanzania kwa wakati huo, Watanzania kwa umoja na uzalendo wa kulilinda taifa lao, wakiongozwa na Mwalimu Nyerere walipigana vita vya kufa na kupona.

Mwisho wa vita, Tanzania ilifanikiwa kukomboa na kurejesha ardhi iliyovamiwa kutoka mikononi mwa wavamizi na hata kumtoa dikteta Idd Amin madarakani nchini Uganda.

Watanzania wengi walijitolea kwa hali na mali kwa taifa lao. Kwa mfano, wapo waliojitoa kwenda kupigana ‘mstari wa mbele’ na wengine walitoa chakula na michango mingine mbalimbali kwa ajili ya wapiganaji waliokuwa kwenye uwanja wa vita.

Vitendo hivi vilikuwa ni vya uzalendo wa hali ya juu vilivyoliletea taifa letu sifa na heshima kubwa machoni pa mataifa mengi duniani.

Itaendelea

Columnist: habarileo.co.tz