Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uwekezaji VETA ukuze uzalishaji mali

77 Saba Saba DSM

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAONESHO ya Kimataifa ya 44 ya Biashara Dar es Saaam (DITF) yamemalizika hivi karibuni viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam. Katika maonesho hayo mambo mbalimbali yalifanyika mabandani na kati ya yaliyonivutia ni wingi wa bidhaa zilizotengenezwa nchini.

Bidhaa zilizokuwepo ni pamoja na dawa, samani na bidhaa nyingi za ufundi kama vile utengenezaji wa mashine mbalimbali za ufundi. Ubunifu wa mashine hizi umefanywa na Watanzania kutoka mashirika mbalimbali, watu binafsi na taasisi mbalimbali za elimu nchini.

Binafsi nilivutiwa zaidi na bidhaa ambazo zimetengenezwa na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (Veta) ambacho ni kati ya taasisi za elimu zilizojitokeza kwenye maonesho hayo.

Katika banda lao asilimia kubwa ya shughuli zilizokuwa zikioneshwa ni zile zilizobuniwa na wanafunzi na wakufunzi wa chuoni hapo. Niliguswa na mashine ya kuzidua ubuyu iliyotengenezwa na Mkufunzi wa Chuo cha VETA Morogoro, Fredrick Uliki.

Mashine hiyo ina uwezo wa kutenganisha ubuyu na mbegu zake kisha kutoa unga kutokana na utenganishwaji huo. Unga huo ndio unaotumika kutengeneza juisi ya ubuyu, inayotajwa kuwa moja ya juisi zenye virutubisho vingi nchini.

Uwezo huo ni kati ya jitihada ambazo binafsi ninaziona kuwa ni mwanzo mzuri kuhakikisha Tanzania ya viwanda inavyoweza kufanikiwa. Uwezo huu wa kutengeneza mashine unatoa majibu Watanzania wanaweza kufanya mambo makubwa hivyo wanapaswa kusaidiwa zaidi.

Watu kama hawa wakiwezeshwa kuzalisha mashine kama hizo kwa wingi zaidi, hakuna sababu ya kuziagiza kutoka nje ya nchi. Ninashauri wawekezaji zaidi kuendeleza uwezo wa uzalishaji mashine nyingi zaidi hapo VETA.

Mashine hiyo itoe mwanga kuwa kumbe Tanzania inaweza kutengeneza mashine za kisasa zenye kurahisisha kazi mbalimbali. Kikubwa kinachotakiwa kwa watu binafsi au taasisi kwenda kuziona hizi fursa na kuwekezaji zaidi ili uzalishaji uwe mkubwa wenye tija.

Hakika mashine kama hii ya kuzidua ubuyu zikiwa nyingi nchini zitavutia wajasiriamali wengi kujiingiza kwenye biashara ya juisi ya ubuyu kwa kuwa watakuwa na uhakika wa kuzalisha juisi nyingi zaidi itakayokuwa inachagizwa na uwezo wa mashine hizo.

Uzalishaji wa sasa unafanyika kienyeji ambapo wanaanza kwa kuuloweka ubuyu wote kwenye maji na kuuchemsha kabla ya kuutenganisha, kisha kuuchuja na kuzalisha juisi hiyo.

Ninapenda kuishauri VETA kuwa na siku maalumu ya kuonesha bidhaa kutoka wabunifu wao kama hawa na kuvishindanisha vyuo vyao nchi nzima ili kupata mbunifu bora zaidi yao.

Nimetumia mfano mdogo wa mzalishaji wa mashine ya kuzidua ubuyu lakini katika vyuo hivyo kuna wabunifu ambao wanaweza kutengeneza mashine za kutoa suluhisho. Kikubwa wataalamu hao wasaidiwe kuzalisha kwa wingi mashine zitokanazo na ubunifu wao huo zikatumike kuleta tija katika jamii.

Uwezo kama huu ndio unaoweza kuchagiza Tanzania ya viwanda kwa kuwa mashine ikiwa ni kiungo muhimu katika viwanda kinachochagiza kufanya uzalishaji kwani zitapatikana nchini.

Columnist: habarileo.co.tz