Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uvamizi kuni za kupikia msituni unavyoitafuna Hifadhi ya Jozani

NISHATI Uvamizi kuni za kupikia msituni unavyoitafuna Hifadhi ya Jozani

Thu, 25 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Angalizo; nusu mbioni kutoweka Suluhisho gesi haijafikshwa vijijini Umeme uliowafikia, kote hawaupikii

ATENDEA Mkanga (35), anatamani kila siku kutumia gesi kwa ajili ya kupikia, lakini anashindwa kutokana kutokuwepo kijijini kwao, hivyo anajikuta akiendelea kutumia kuni na mkaa.

Mama huyo mwenye familia ya watoto watatu anaishi katika kijiji cha Charawe, mkoa wa Kusini Unguja. Anatumia shilingi 25,000 kila mwezi kwa ajili ya kununua kuni anazotumia kupikia chakula kwa ajili ya familia yake.

Charawe ni miongoni mwa vijiji tisa, vilivyomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Jozani, ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti ya asili, licha ya kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii.

Kijiji anachoishi Atendae, kina wakazi 1,539 wanaoumudu kununua gesi, lakini wanaikosa kwa sababu ya kutokuwepo biashara hiyo kijijini hapo na kwa jumla, wakazi walioko ni kaya 480 ambazo zote zinatumia nishati za kuni na mkaa pekee kupikia.

“Duka la kuuza gesi lipo Jozani, ambako ni umbali kilomita zaidi ya 20 kutoka hapa. Pia, hakuna usafiri wa gari, usafiri pekee uliopo ni baiskeli na bodaboda ambayo kuikodi ni shilingi 5, 000,” anasema mama huyo.

Atendae anasema, wafanyabiashara wengi katika sekta ya gesi wamewekeza maeneo ya mjini na vijiji ambavyo ni maarufu kwa biashara ya utalii.

Kwa hiyo, licha ya kupenda kutumia nishati gesi, kwa imani ni rahisi, hasa ikizingatiwa upatikanaji wa kuni umekuwa mgumu, hata kuwafanya wakazi hao watumia nguvu na muda mrefu kuzipata.

“Hivi sasa serikali inapinga marufuku ukataji miti na kijiji chetu kimezungukwa na Mbuga (Hifadhi) ya Taifa ya Jozani, hivyo ni vigumu kupata kuni kwa ajili ya kupikia,” anasema.

Mkazi mwingine, Fatma Mahmoud (40), anasema licha ya gesi kukosekana, pia hata suala la uelewa kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo hakuna.

“Tukishapewa elimu juu ya matumizi ya gesi, tutaondoa hofu na tutakuwa na ari kubwa ya kuitumia,” anasema, huku akiunga hoja ya mtangulizi kwamba, kukosekana gesi, kufanya wanawake wanaendelea kuumia.

Anasema, imefika hatua wanalazimika kuamka alfajiri kwenda msituni kutafuta kuni, hivyo inawakosesha fursa nyinginezo za maendeleo.

Hadi sasa inaelezwa, matumizi ya kuni na mkaa yanazidi kuangamiza misitu ya Zanzibar na ripoti uliouopo sasa kuhusu Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka Zanzibar, inasema kila mwaka kuna ekari 100 za miti zinapotea.

Haroub Abdi Abdallah (39), ni baba mwenye watoto watano. Ana maelezo kuwa, matumizi ya kuni ya yanaharibu mazingira, pia kubadilisha rangi ya nyumba zao.

“Tunahitaji sana gesi, kwa sababu kuni zinachafua nyumba zetu hivyo inatulazimu kila mwaka kubadilisha rangi ili kuwa na mwonekano mzuri,” anasema.

Haroub, anakiri shida ya upatikanaji kuni hivi sasa umepungua tofauti na miaka 10 iliyopita, kutokana na ongezeko la wakazi wake.

UMEME UPO, HAUPIKIWI

Inaelezwa tatizo hilo la kukosekana gesi na shida ya kuni, pia lipo katika kijiji jirani cha Ukongoroni, ambacho kina kaya 240 na huduma za umeme zilizounganishwa kutoka gridi ya taifa kwa wakazi 850, lakini hautumiwi kupikia.

Mkazi wa kijijini hapo, Usheza Mwita Makame (60), anasema wanatumia kuni na mkaa, kwa sababu ndio inayopatikana kIrahisi kwao.

Usheza, ana angalizo kwamba, kuendelea kutumia kunaathiri mazingira ya Hifadhi Jozani, inapunguza idadi ya miti ya asili, wanayotumia kwa ajili ya tiba asili.

“Zamani mtu akiumwa na ugonjwa wa pumu tulikuwa tunaingia msitu kutafuta magome ya Myuwi pumu inapoa, lakini sasa umetoweka kabisa kwa sababu ya ukataji wa miti,” anasema.

Mamlaka zinaeleza kuwa ukataji miti umezidi kuangamiza misitu na sasa wakazi hao wameanza kuvamia eneo la hifadhi.

HOFU INAYOTAWALA

Msaidizi wa kiongozi wa serikali ya kijiji hicho, Fadhil Sudi Mlenge (40), anasema, licha ya mamlaka ya kiserikali kutenga eneo maalum kwa wanakijiji kukata kuni, sasa hivi eneo limepungua kutokana na kuongezeka matumizi na wanakijiji wanavamia hifadhini.

“Muda wa kutumia gesi umefika, wanakijiji wanaihitaji lakini changamoto ni jinsi ya kuipata. Hivyo, tunawaomba wafanyabiashara wasogeze huduma hii kijijini kwetu,” anasema kiongozi huyo wa serikali.

Awesu Shabani Ramadhani, Naibu Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Mazingira Jozani (JECA), inayonufaika na mgawo wa mapato yanayotokana na watalii wanaotembelea msitu huo, sasa ana hofu kutakuwapo athari zaidi, kama hatua hazitachukuliwa.

Ubashiri wake ni kwamba, pasipochukuliwa hatua za udhibiti katika miaka 20 ijayo, kuna uwezekano nusu ya msitu huo unaoingiza mapato zaidi ya Sh. bilioni 1.3 kwa mwaka, utakuwa umeathirika.

“Mbuga ya Taifa ya Jozani ndio roho ya uchumi wa wa vijiji tisa vilivyomo katika msitu huu, vikiwamo Charawe na Ukongoroni, hivyo kama juhudi za kudhibiti uharibifu hazitachukuliwa, litakuwa pigo kubwa kwa wanavijiji.

“Hivi sasa, tuhamasishe shughuli za uzalishaji mali ambazo haziharibu misitu, ikiwamo kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia umeme wa jua kwa ajili ya ili kuhakikisha wanavijiji wanakuwa na kazi mbadala na kuachana na uharibifu wa misitu,” anasema.

Awesu anasema, miti ya asili kama mikoko inayozuia maji ya bahari kuvamia vijiji na maeneo ya kilimo, ndio inayokatwa kwa wingi kwa ajili ya kuzalisha mkaa, kwa sababu wanavijiji wanaamini una mkaa mzuri.

OFISA MISITU

Rahika Hamad Suleiman, Ofisa kutoka Kitengo cha Elimu ya Misitu kwa Wanajamii katika Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka Zanzibar, anasema asilimia 65 ya wananchi Zanzibar na wanavijiji tisa kati ya 10, wanatumia kuni na mkaa kupikia.

Anasema ni hali inayosababisha baadhi ya wanyama kama Chui waliopatikana Zanzibar kwa muda mrefu, sasa wanatoweka, baada ya kushambuliwa na wanavijiji.

Pia, anawataja wanyama kama Paa Nunga na Kima Punju, ambao ni kivutio kikubwa cha utalii, wameanza kuadimika.

Anasema, pia vianzio vya maji kama mabwawa yaliyokuwa yakipatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Jozani, ambayo yalitumiwa na wanyama kunywa maji, yamekauka baada ya watu kukata miti.

“Tumefika wakati sasa kuhakikisha tunabadili mwelekeo wetu, tuko kwenye mkwamo na hatuna jinsi zaidi ya kuhamasisha wanavijiji kutumia gesi,” alisema.

Ofisa huyo anasema, Idara ya Misitu inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya gesi na majiko sanifu yanayotumia kiwango kidogo cha kuni, ili kulinda mazingira yaliyopo.

Pia anasema wauza gesi visiwani wanakiri kutofikia katika sehemu kubwa ya vijiji, kutokana na uhaba wa gesi inayoingizwa nchini.

Msambazaji wa gesi V-Gas Zanzibar, Taufiq Salum, anasema bado hawajayafikia masoko mengi ya vijijini, kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo inayoingizwa visiwani, kwani kuna upungufu wa miundombinu ya kuhifadhi.

Anaahidi changamoto hiyo itaondoka karibuni, baada ya ujenzi wa bandari ya kupakua gesi inayojengwa Mangapwani, Unguja kukamilika.

Columnist: www.tanzaniaweb.live