Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uteuzi wa Mpango unatia matumaini

WAZIRI MPANGO Uteuzi wa Mpango unatia matumaini

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Uteuzi huo umefanywa kujaza nafasi hiyo ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Rais Samia aliyeapishwa kuwa rais kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli, Machi 17, mwaka huu.

Katika mitandao ya kijamii na kwenye baadhi ya magazeti majina kadhaa ya wanasiasa yalikuwa yakitajwa, huku ikielezwa kuwa mmoja wao angeteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa katika taifa letu.

Baada ya uteuzi wa Dk. Mpango jana, jina hilo liliwasilishwa bungeni asubuhi na kupigiwa kura na wabunge, ambao walimthibitisha kwa kura 363, sawa na asilimia 100, hivyo kudhihirisha kwamba uteuzi wa Rais kwa kushauriana na chama chake (CCM) ulikuwa sahihi.

Baada ya uteuzi huo na baada ya kuthibitishwa na Bunge, wengi walimwelezea Dk. Mpango kwamba ni mtu sahihi, huku wakimwelezea kuwa ni mtu wa Mungu, mwadilifu, mchapa kazi na sifa nyingine nyingi ndani na n je ya Bunge.

Hata yeye alipozungumza bungeni kabla ya kuthibitishwa, alidhihirisha jinsi gani anaguswa sana na matatizo yanayoikabili nchi yetu hususan umaskini na utayari wake wa kumsaidia Rais Samia kuyatafutia ufumbuzi kwa maslahi ya Watanzania wote.

Kikubwa aliahidi kumsaidia Rais Samia kuhakikisha miradi iliyoanzishwa na Dk. Magufuli utekelezaji wake utaendelea, huku pia akijinadi kwamba ni mchukia rushwa na udokoaji wa fedha za umma. Kadhalika aliahidi usimamizi wa rasilimali za umma na kwamba kwa hilo hana upole.

Tunampongeza sana Rais Samia kwa kumteua Dk. Mpango, ambaye ni mtumishi wa umma anayekidhi sifa karibu zote ambazo tuliziainisha kwenye safu hii Machi 25, mwaka huu za mtu anayefaa kuwa makamu wa rais.

Sifa tulizozieleza ni uadilifu, utiifu, kuchukia rushwa, kushehimu haki za binadamu, demokrasia, na utawala bora, mchapa kazi, mzalendo wa kweli, mbunifu, mwenye rekodi nzuri katika utendaji, mkomavu, mtulivu, anayeheshimika sana katika jamii, asiye na ubaguzi wa dini, rangi na itikadi za kisiasa.

Pia ambaye atamsaidia Rais Samia kutatua kero za wanyonge, kusimamia ukuaji wa uchumi, nidhamu ya utendaji na uwajibikaji serikalini, anayeweza kumsaidia kurejesha uhusiano mzuri na jumuiya ya kimataifa na asiye na matamanio ya kuunda mitandao kwa ajili ya kusaka uongozi wa juu wa nchi.

Tunathubutu kusema kwamba Samia ameonyesha kwamba kweli ni rais kama alivyosema wakati wa mazishi ya kitaifa ya Hayati Dk. Magufuli jijini Dodoma Machi 21.

Huu tunaona ni mwanzo mzuri katika uongozi wa Rais Samia, baada ya kumteua mtu ambaye ametoa utumishi wa kutukuka kwenye taifa letu na ambaye hajawahi kupata doa lolote.

Tunampongeza sana Dk. Mpango kwa kuaminiwa na Rais Samia, hivyo amemteua kuwa msaidizi wake, ambaye pia atakuwa mshauri wake mkuu.

Tuna matumaini kwamba serikali itaendelea kutekeleza miradi yote ikiwamo ya kimkakati pamoja na kutoa huduma zingine muhimu za elimu, afya pamoja na kuwajali na kuwatatulia kero wanyonge.

Columnist: ippmedia.com