Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Utani wa jadi usigeuzwe uhasama uwanjani

Mashabiki Wa Simba V Yanga Mashabiki wa Vilabu vya Simba na Yanga

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sote tunafahamu huwa mchezo wa soka ndio uliothibitika kuwa na idadi kubwa ya wadau zaidi duniani kuliko michezo mingine yote ambapo ufuatiliaji wa kila siku wa mechi za ligi na mashindano mbalimbali duniani ni kitu cha kawaida kwa wadau wa mchezo huo na ni sehemu ya maisha yao ya kila siku katika ratiba za maisha.

Kwa kuwa mazoea hujenga tabia, hivyo wadau wengi wa mchezo wa soka wamejengewa tabia ya maisha inayotokana na mazoea yaliyopo katika mchezo wa soka na kuwafanya kuishi maisha yanayoendana na mchezo huo hata kwa wale ambao wanahudumia sekta nyingine tofauti na soka.

Miongoni mwa tabia ya wadau wa mchezo wa soka iliyojengwa na ushindani unaotokana na mchezo husika ni tabia ya uvumilivu wa mashabiki ambao huwa nao pale timu inapopoteza mechi ya kwanza dhidi ya mshindani wake katika ligi au mashindano fulani na kuwa na moyo wa kusubiri mechi ya marejeano bila kujali kuwa itakuwa ni ya ugenini au nyumbani.

Na uvumilivu huo katika mchezo wa soka huwapo hata kama timu hiyo itakuwa imepoteza mechi zote mbili za ligi au mashindano fulani kwa mpinzani wake, lakini bado moyo wa kusubiri msimu ujao huwa upo kwa mashabiki kwa sababu ndio tabia iliyojengeka kutokana na mazoea ya mchezo wa soka.

Na hii mara nyingi huufanya mchezo kuendelea kufuatiliwa kila siku na shabiki wa timu inayoshinda kufarijika katika kipindi cha mafanikio ya timu anayoishabikia, huku anayeshindwa kuendelea kuwa na subira ya msimu au miaka ijayo.

Kwa mfano, hapa kwetu Tanzania ambapo mashindano ya Ligi Kuu ya soka yalianzishwa rasmi 1965, lakini mfumo wa timu zinazoshiriki ligi hiyo kucheza mechi zao katika uwanja wa nyumbani ulianzishwa 1977 baada ya viongozi wa soka wa wakati huo kujifunza kutoka Ligi Kuu ya Scotland na kuleta utaratibu huo ambao ni endelevu katika mchezo wa soka unaotumika duniani kote .

Hivyo, tabia hiyo ya kusubiri mechi ijayo baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa mpinzani wako ni tabia ambayo wanajamii wa mchezo wa soka wanatakiwa kujivunia kwani inaongeza uvumilivu kwa mpenzi wa timu timu fulani iliyofungwa kuwa na moyo wa kusubiri mechi ya marudiano au mechi ya msimu ujao ili kulipiza kisasi kwa mpinzani wake aliyemfunga na kujivunia baada ya kulipiza kwa matokeo ya uwanjani.

Nauzungumzia utamaduni huo wa kuwa na uwezo wa kuvumilia kwa sababu sote tunafahamu kuwa hapa kwetu tunao utamaduni katika mchezo wa soka unaohusiana na timu kongwe za Simba na Yanga ambao mashabiki na wapenzi wa timu hizi wamekuwa wakitaniana na kuendelea kuwepo kwa utani huo wa zaidi ya miaka 70.

Na hii imezifanya klabu hizi mbili kuwa miongoni mwa vivutio vinavyotumika katika kutengeneza historia ya soka la Tanzania.

Ndio maana huwezi kuzungumizia historia ya soka la Tanzania katika sehemu yoyote bila kugusia uwepo wa klabu hizi ambazo miongoni mwa vitu vilivyosababisha kuendelea kuwepo kwa mashabiki wao ni utamaduni wa kusubiri mechi ijayo au msimu ujao.

Na hii ni kwa timu illiyopoteza mchezo huku iliyoshinda ikitoa faraja kwa washabiki wake.Hivyo utamaduni huo unatakiwa kuendelezwa kwa manufaa ya soka kwa sababu faida zake katika jamii ni kubwa kutokana na uwezo wa kuvumilia uliojengwa na mazoea.

Nimezungumzia uwezo wa kuvumilia kuwa ni utamaduni uliojengwa na mchezo wa soka wenyewe kwa mashabiki pale timu zao zinapopoteza mechi kwa sababu wiki iliyopita tulishuhudia tukio lililoonekana kuhusisha mashabiki wa timu mojawapo kuzuia mashabiki wa timu nyingine kufuatilia mechi ya timu yao uwanjani na kusababisha kutokea kwa vurugu jukwaani .

Hakika tukio hilo ni miongoni mwa vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi kwani tukio kama hilo ni kiashiria cha upungufu wa uvumilivu kwa mashabiki wa soka ambao katika hali ya kawaida wanatakiwa kuwa na tabia ya kuvumilia chochote kinachohusiana na mchezo wa soka kwa timu wanayoishabikia.

Hivyo kwa tukio lile nadhani ni wakati wa kila mdau hivi sasa anayehusika na mchezo wa soka kutumia elimu, uzoefu na maarifa ili kusambaza elimu na uelewa kuhusu maana halisi ya ushindani wa mchezo wa soka ambao hutakiwa kuwa uwanjani, huku nje ya uwanja utani ndio ukitamalaki baada ya mashabiki wa timu zinazoshindana uwanjani.

Lakini pia elimu inayotakiwa kutolewa kwa mashabiki ni kuhusu utamaduni unaotakiwa kujengwa kupitia mchezo wa soka kwa mashabiki na wadau wa soka katika sehemu mbalimbali.

Hivyo kwa makala haya, naomba wadau na mashabiki katika mechi zijazo wajitokeze na waonyeshe kwa vitendo kuwa maana ya ushabiki ni kutaniana na sio kuchukiana na itakuwa vyema iwapo kama watachanganyikana kwa pamoja ili kuonyesha umuhimu wa kushindana uwanjani, lakini kushirikiana nje ya uwanja hasa kwa mashabiki wa klabu hizi kongwe hapa nchini.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz