Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Utabiri wa hali ya hewa kwa Willy Osomba Onana

Onana Willy Esomba Willy Osomba Onana

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Willy Essomba Onana ametufungulia mbwembwe za usajili za watani wa jadi mapacha wa Kariakoo. Ametangazwa kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kutua nchini katika mitaa ya Kariakoo. Alikotoka ametisha kiasi kwamba inatia hamu kumuona.

Amefunga mabao 16 ya Ligi kuu ya Rwanda. Amefunga mabao saba katika michuano yao ya FA. Amepiga pasi kumi za mabao. Kwanini Wanasimba wasimsubiri kwa hamu pindi watakapomuona kwa mara ya kwanza uwanjani akiwa katika jezi yao mpya?

Simba walihitaji kutia nguvu katika maeneo mengi ya uwanja. Waje wachezaji wa maana ambao watapunguza umuhimu wa akina Clatous Chama uwanjani. Onana ametufungulia mlango wa kuitazama Simba mpya msimu ujao.

Nini tutajirie kutoka kwake? Moyo wangu umegawanyika. Naweka akiba ya maneno. Kuna kumbukumbu mbaya zinanijia kabla ya kutarajia makubwa kutoka kwa Onana. Miaka ya karibuni inaonekana tumezipita kichangamoto baadhi ya Ligi za nchi jirani.

Inaonekana kama vile Ligi yetu ina ushindani zaidi kuliko hizi za majirani. Aliwahi kuja mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda, Juma Balinya akatambulishwa kwa mbwembwe katika Mkutano mkuu wa Yanga lakini kilichofuata kilikuwa fedhea. Hakuonesha makali yoyote yaliyoashiria kwanini alikuwa mfungaji bora Uganda.

Agosti 2020, mshambuliaji mrefu na mwenye misuli kutoka Ghana, Michael Sarpong alitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pale Kipawa kwa ajili ya kuitumia Yanga. Wote tuliogopa.

Sarpong alitoka kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Rwanda akiwa amefunga mabao 16 kama haya ambayo Onana amefunga msimu uliopita pale Rwanda. Hata hivyo baadaye Sarpong akaonekana kuwa mshambuliaji wa kawaida tu. Atakumbukwa tu kwa bao la penalti alilomfunga Aishi Manula katika pambano la watani wa jadi baada ya Tuisila Kisinda kufanyia madhambi na Josh Onyango.

Ndani ya msimu mmoja tu Yanga walivunja mkataba wake na kisha akatokomea zake kama alivyokuja. Mifano hii miwili mibaya sipendi itokee kwa Onana kwa sababu mbalimbali. Kuna upande wa pili wa shilingi ambao unafariji kuhusu Onana.

Anakwenda katika timu kubwa kuliko alikotoka. Na ambayo ina wachezaji wakubwa kuliko alikotoka. Sidhani kama alikotoka kulikuwa na wachezaji wanaoweza kutengeneza nafasi wenye hadhi ya Chama, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe, Saidoo Ntibazonkinza na wengineo.

Ninapoisema ‘na wengineo’ namaanisha kwamba Simba itaimarisha zaidi kikosi chake msimu huu na huenda Onana akajikuta akicheza na wachezaji wazuri zaidi kuliko ambao tayari wapo Simba. Ni suala la mabosi wa Simba kutofanya makosa katika dirisha hili.

Kama ni mshambuliaji mzuri basi atafunga tu. Simba ya hapa karibuni hauwezi kuifananisha na timu za Rwanda au nyingine za Afrika Mashariki. Kama ni mchezaji mzuri atafunga tu. Bahati nzuri kwake ni kwamba huenda akajikuta anachezea Simba nzuri kuliko Yanga ambayo Sarpong na Balinya walichezea.

Kama ni mshambuliaji mzuri atafunga tu. kama ni mtengenezaji mzuri atatengeneza na watu watafunga. Licha ya Simba kukosa ubingwa lakini Simba ndio timu ambayo ilifunga mabao mengi zaidi msimu uliopita wa Ligi kuu. Inaonyesha wanatengeneza nafasi nyingi na kufunga zaidi.

Nabakiza akiba ya maneno pia kwa Onana kutokana na mlinganisho fulani ambao naufanya kwa Sarpong. Wote wawili wamekuja nchini wakitokea Afrika Magharibi katika nchi za kisoka. Sarpong alitokea Ghana wakati Onana ametokea Cameroon.

Kwa mujibu wa umri wao, uwe wa ukweli au wa uongo, Sarpong alikuja nchini akiwa na miaka 25 wakati Onana amekuja na umri wa miaka 23. Ni ngumu kwa wachezaji wa umri huu kuja nchini kama wana ubora mkubwa. Mara nyingi huwa wanabebwa na ukubwa wa mataifa yao katika rekodi za soka.

Nilipomtazama Sarpong kwa mara ya kwanza nilishangaa kwanini mshambuliaji wa umbile lake, anayetoka Ghana, mwenye umri wake, anaweza kuja kucheza Tanzania. Alipoanza kucheza nilielewa ni kwanini yupo pande za Afrika Mashariki licha ya kusumbua Rwanda.

Ni kama ilivyokuwa kwa Yikpe. Kwa mchezaji wa umbo lile, anayetokea Ivory Coast, kama angekuwa mshambuliaji hatari sidhani kama angekuwa upande huu. Na sasa ni zamu ya Onana kunithibitishia kwamba nina mawazo potofu.

Na pale tu atakaponithibitishia kwamba nina imani potofu basi sidhani kama Onana atakuwa na maisha marefu Simba. Wachezaji wa mataifa hayo huwa wanauzika mapema sokoni kuliko wachezaji wanaotoka mataifa kama Tanzania, Swaziland au Comoro.

Mwisho wa siku kitu cha msingi kwa Onana ni kujaribu kurudisha utatu wenye hatari ambao ulikuwepo Simba miaka ya karibuni lakini umetoweka. Simba waliwahi kuwa na washambuliaji watatu hatari waliotengeneza utatu mtakatifu.

Walikuwepo John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu kwa wakati mmoja. Msimu mzuri wa mwisho wa Simba kabla ya utawala wa Yanga wote walifunga mabao zaidi ya 12 kila mmoja. Baada ya wao kuanza kutetereka Simba ikaanza kutetereka.

Kama Moses Phiri akiwa fiti, halafu Jean baleke akaendeleza fomu yake, kisha Onana akawa moto,kuna uwezekano wakarudisha utatu mtakatifu pale Simba. Ni namna tu ambavyo kocha, Robertinho ataweza kuwatumia maana nasikia hapatani sana na Phiri ambaye tayari alishakuwa mshambuliaji bora wa Simba kabla ya kuumia, na kabla ya ujio wa Baleke.

Ujio wa Onana unaweza kuwa mwisho wa zama za John Bocco lakini pia unatarajia kumuondoa Habib Kyombo ambaye licha ya Wanasimba kuwa na matarajio makubwa kwa Kyombo baada ya kumpora kutoka SIngida United msimu uliopita lakini hakukidhi matarajio.

Columnist: Mwanaspoti