Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usimamizi shirikishi wa misitu unavyoleta manufaa vijijini

454acf75d37616a0710fd6124742c8ce Usimamizi shirikishi wa misitu unavyoleta manufaa vijijini

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHERIA ya Misitu ya mwaka 2002, inasema jamii inaweza kulinda, kuhifadhi, kusimamia na kutumia kiuendelevu misitu katika ardhi ya kijiji ili kukidhi mahitaji yao ya kimaendeleo ya muda mrefu.

Taarifa ya Tathmini ya Misitu nchini ya mwaka 2015, inaonesha kuwa hekta milioni 21.6 sawa na asilimia 45 zinamilikiwa na Serikali za Vijiji, hekta milioni 15.48 (asilimia 35) zinamilikiwa na Serikali Kuu (TFS,TAWA na TANAPA), Serikali za Mitaa zinamiliki hekta milioni 3.36 (asilimia 7), Sekta binafsi 3.36 (asilimia 7), Mataji wazi (General land), helta milioni 2.4 (asilimia 5) na miliki nyingine ya misitu 0.48 (asilimia 1).

Mpaka sasa, zaidi ya hekta milioni mbili za misitu ndizo zinazosimamiwa na serikali za vijiji kwa njia endelevu baada ya kupimwa katika vijiji takribani 1,000 nchini kote.

Jamii zinazosimamia misitu hiyo zina shauku ya kujua jinsi wanavyoweza kunufaika kutokana na uvunaji endelevu.

Pamoja na sheria pia kuna Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998 ambayo inatamka wazi kuwa madaraka ya kusimamia rasilimali misitu kwa uendelevu yamekabidhiwa sekta ya misitu.

Utekelezaji wa sera hiyo unalenga maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kusimamia rasilimali misitu ya nchi katika ngazi zote kwa maendeleo endelevu na kusimamia shughuli za viwanda na shughuli zilizojikita kwenye misitu ili kuchangia maendeleo ya taifa na mgawo wa faida kwa uwiano sahihi baina ya wadau.

Lengo lingine ni kuhifadhi mifumo ikolojia ya kipekee ya nchi na bayoanuwai kwa kuzingatia mahitaji ya jamii kupitia mbinu zinazofaa za usimamiaji na matumizi.

Sera inaelekeza kuwepo matumizi ya mifumo ya taasisi na muundo upasao wa rasilimali watu na mahitaji ya fedha yanayotakiwa kukidhi masharti ya maendeleo yatamaniwayo.

Halikadhalika kuna miongozo juu ya jinsi misitu kwenye ardhi ya kijiji

inavyoweza kuvunwa kwa njia endelevu na kunufaisha jamii vijijini.

Mwongozo huu unazilenga kamati za maliasili za vijiji, kundi ambalo hupanga mipango ya uvunaji endelevu katika misitu ya vijiji vyao.

Halmashauri za wilaya pia zinaweza kunufaika kutokana na

mwongozo wa kisheria katika mchakato nzima wa kuvuna.

Mwongozo huu umegawanyika katika hatua kuu mbili. Hatua ya kwanza

inahusu kuanzisha na kutangazwa msitu wa hifadhi wa kijiji na hatua

ya pili inahusu maandalizi ya uvunaji katika msitu wa hifadhi wa kijiji.

Baadhi ya vijiji katika wilaya za Kilosa, Mvomero, Morogoro, Kilwa, Liwale, Ruangwa, Nachingwea, Tunduru, Nyasa, Mbinga, Handeni, Kipindi na Mpwapwa sasa vinanufaika na dhana hii ya vijiji kumiliki misitu.

Dhana hiyo inajulikana kama Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) ambayo imesababisha mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii pamoja na ulinzi wa mazingira.

Ni dhana ambayo imefikia vijiji vya wilaya hizo kupitia miradi mbalimbali kama Programu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Mradi wa Kuleta Mageuzi Kupitia Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST), Mpingo Conservation Development Initiative (MCDI), Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori Duniani (WWF) na mingine mingi ambayo imechochea maendeleo na uendelevu wa rasilimali misitu.

Miradi hiyo ambayo inatafsiri sheria na sera ya misitu kwa vitendo imekuwa ikibuniwa na mashirika ya kiraia ambapo TTCS na CoFoREST inatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

Kwa upande wa FORVAC, inafadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Wizara ya Maliasili na Utalii, lengo la wafadhili hao ni kuona misitu ya Tanzania inakuwa salama kutokana na matumizi endelevu ya jamii inayoizunguka.

Moja ya malengo ya miradi hiyo ambayo inatekelezwa katika vijiji ni kuchochea uhifadhi, usawa wa kijinsia, ukuzaji uchumi, huduma za jamii na maendeleo ambapo asilimia kubwa ya hayo yanaonekana.

TFCG na MJUMITA kupitia miradi yao ya TTCS na sasa CoFoREST wameweza kubadilisha maisha ya wanavijiji zaidi ya 40 na kuchangia USMJ katika hekta zaidi ya milioni mbili.

Baadhi ya vijiji ambavyo vinatajwa kufanya mapinduzi chanya kupitia USMJ ni Ulaya Mbuyuni, Kitunduweta, Mlilingwa, Msolokelo, Maharaka, Diguzi, Matuli vinavyopatikana mkoani Morogoro.

Aidha, kupitia miradi yao wameweza kufika kijiji cha Mahenge, wilayani Kilolo mkoani Iringa, Mtawatawa wilayani Liwale mkoani Lindi na Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Vijiji hivyo kwa miaka isiyozidi 10 vimeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 5 na kuwekeza kwenye ujenzi wa shule, zahanati, visima vya maji, ofisi za vijiji, bima za afya, mikopo, kilimo hifadhi, mpango wa matumizi bora ya ardhi na mingine mingi.

Mafanikio yanaoneka pia kupitia FORVAC ambayo ipo kwenye wilaya 12, lengo likiwa ni kuhakikisha mnyororo wa thamani wa mazoa ya misitu unaonekana huku uhifadhi ukiongezeka.

Shirika la MCDI na WWF ni wadau wengine ambao wanatajwa katika mikoa ya kusini kama wakombozi wao kiuchumi, kimaendeleo na uhifadhi.

Ni kupitia MCDI na wadau wenzake sasa wamewezesha Kijiji cha Nanjilinji wilayani Kilwa mkoani Lindi kuanzisha miradi mbalimbali baada ya kuzalisha zaidi ya shilingi milioni 800 na sasa kumiliki nyumba ya wageni yenye vyumba 18 iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 100.

Nanjilinji kupitia USMJ ndio kijiji ambacho mjamzito kujifungua kwake ni fursa kwani kijiji kimekubaliana kutoa shilingi 50,000, jambo ambalo halipo popote Tanzania.

Pia kijiji hicho kimetoa kipaumbele cha elimu kwa kuwanunulia wanafunzi sare za shule, kujenga shule, nyumba za walimu, ujenzi wa ofisi ya kisasa iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 70.

Hayo yapo pia katika kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ambapo wanafunzi wanakula shule, wananunuliwa madaftari, kalamu na chaki hivyo kuongeza ufaulu.

Kijiji cha Mtawatawa chenyewe kimewezeshwa kujenga zahanati, nyumba ya mtendaji, kununua trekta, kujenga darasa, kununua pikipiki, ujenzi wa choo na kumlipa mwalimu mshahara kwa miaka mitano sasa ili afundishe shule ya serikali.

Mtendaji wa Kijiji cha Mtawatawa, Benadetha Kitang'ita anasema hayo yote yametokea kupitia elimu inayotolewa na FORVAC, MJUMITA, TFCG, MCDI na Serikali.

Yote hayo yanafanyika kwa kuzingatia usawa wa kijinsia hali ambayo inatajwa kuchochea USMJ kwani jamii nzima inaona faida tofauti na zamani ambapo kulikuwa na kundi kubwa la wanaume kunufaika zaidi.

Mtendaji wa Kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Philemon Dastan anasema usawa wa kijinsia umeonekana kupitia bima ya afya na uzalishaji wa mbao kuanzia uvunaji.

Hadija Athuman ambaye ni Katibu wa Kamati ya Maliasili Kijiji cha Sautimoja anasema miradi ya USMJ imewafanya wawe na usawa wa kijinsia katika kazi.

Naye Shakila Bushir anasema pamoja na kutambua umuhimu wa kuhifadhi kwa njia endelevu pia wamejengewa kujiamini kama wanawake ambapo yeye anashiriki kwenye ulinzi wa msitu.

Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo anasema miradi ya USMJ imekuwa chachu ya mabadiliko na mitazamo ya kijinsia hali ambayo imeleta usawa.

"Awali rasilimali misitu ilijulikana kama chanzo cha mapato kwa wanaume lakini TTCS imeweza kubadilisha mtazamo huo hapa kwetu Kilosa hivyo nadiriki kusema kwa sasa kuna usawa wa kijinsia," anasema.

Kwa upande wake, Edward Kimweri Ofisa Misitu wilaya ya Mvomero amesema dhana ya mapato ipo ila heshima kwa jamii husika imeongezeka.

Meneja Mradi wa CoFoREST, Chales Leonard anasema usawa wa kijinsia ni moja ya vipaumbele vyao kwani hawataki mtu aachwe nyuma kwenye maendeleo.

"Sisi tangu awali tulikuwa tunaamini dhana ya jinsia ndio njia ya kufanikisha mradi jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi fulani," anasema.

Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo anasema miradi yao inajikita kwenye kuangalia namna sera na sheria ya misitu vinavyoweza kutumika kuondoa changamoto za kiuchumi, kijamii, uhifadhi na maendeleo kwa vijiji husika.

Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahima Njaidi anasema thamani ya misitu ya vijiji inatakiwa kubadilisha maisha ya wanavijiji katika kila sekta na hilo linafanyika.

"Sisi hatupeleki miradi ili tuonekane tumepeleka. Tunataka mabadiliko ambayo yatagusa usawa kwa kijinsia ili thamani ya misitu ionekane," anasema.

Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe anasema wameamua kuwekeza katika USMJ kutokana na kuhusisha kundi kubwa la wananchi hasa wa vijijini.

Msoffe anasema hekta milioni 22 ambazo zipo kwenye misitu ya vijiji ikisimamiwa kwa mfumo wa USMJ itachangia mabadiliko chanya na endelevu.

Mtaalamu na Msimamizi wa Misitu WA FORVAC, Alex Njahani anasema kiuhalisia matarajio yao yanaonekana kuanza kuzaa matunda.

Njahani amesema mabadiliko chanya kwa wanavijiji wanaozunguka miradi ndio matamanio yetu hasa kwa wilaya 12 ambazo tunatekeleza miradi.

Mafanikio hayo ya USMJ kwa baadhi ya vijiji yamewaridhisha wafadhili wa miradi ambao ni pamoja na SDC ambapo Mkuu wa Idara na Kipato kutoka Ubalozi wa Uswisi, Peter Sidler anaweka bayana.

Sidler anasema uwekezaji wa zaidi ya bilioni 20 kwenye eneo hilo una manufaa mengi kwa wananchi, serikali na misitu hivyo wataendelea kusaidia eneo hilo kwa miaka ijayo.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

Columnist: habarileo.co.tz