Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usicheze ukiwa na maumivu ya viungo

Kelvin De Bruyne Bayern Injury 1140x640 Usicheze ukiwa na maumivu ya viungo

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi mbalimbali duniani zimeisha, wiki iliyopita mwishoni kulikuwa na mechi kadhaa za kimataifa ikiwamo zile za kunyang’anyiro cha kupata nafasi ya mashindano ya mataifa ya Afrika.

Ukiacha hayo tuliona pia hapa Tanzania juzi siku ya Jumanne katika mechi ya hisani iliyohusisha timu Samatta na timu Kiba iliyopigwa katika Uwanja wa Azam Complex.

Mechi hii ilikuwa ni muhimu katika kada ya afya ya jamii kwani ilikuwa na lengo la kuchangia pesa kwa ajili ya kusaidia watoto njiti, ilikuwa na mchanganyiko wa wachezaji mbalimbali wa hapa nchini.

Wachezaji wengi walikuwa wametoka katika majukumu ya klabu na ya timu ya Taifa lakini walionekana wakicheza mechi hii wakiwa na furaha huku pia wakionyesha uungwana wa hali ya juu.

Pamoja na mechi hii kuwa ni ya hisani lakini wachache walionekana walipomaliza kama vile wanachechemea, hii ni kawaida katika soka kwani soka inahusisha kutumia nguvu wakati wakucheza.

Ni kawaida kwa mwanasoka kwa hiyari yake akawa na majeraha yanayoleta maumivu lakini akaamua kucheza hivyo hvyo, na zaidi anaweza akatumia dawa za maumivu na kucheza.

Dawa hizi huwaondolea maumivu kwa muda tu lakini si kuponya jeraha au kupunguza ukubwa wa jeraha. Leo nitawapa ufahamu wa mambo mawili muhimu kwa wachezaji yaani madhara ya kucheza na maumivu na utumiaji wa dawa za maumivu kiholela.

Usicheze na maumivu kwa sababu hizi

Kucheza mchezo ukiwa na maumivu ni jambo ambalo sio sahihi kiafya kwani kunaongeza ukubwa wa tatizo. Jeraha linapotoneswa mara kwa mara ni chanzo cha kujijeruhi upya na hivyo kuchelewa kupona. Maumivu kwa mwanamichezo aliye majeruhi ni ishara kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Maumivu yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati na makali. Yanaweza kuwa ni majeraha ya mfupa, misuli, mishipa ya fahamu na tishu nyingine za mwilini.

Panapotokea jeraha mwili hujibu mapigo kwa kutuma askari mwili kwa ajili ya kukarabati neneo hilo. Mlipuko wa kinga ya mwili ndio chanzo cha mtu kuhisi maumivu, kufa ganzi, kuvimba, kupata joto na kubadilika rangi ya ngozi. Hali hii ndio kitabibu huitwa inflammation.

Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi hudhani kuwa maumivu yanapopungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza. Pasipo kufahamu kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Mara nyingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo huwapo kwa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa. Unapobainika na wataalam wa tiba za michezo kuwa una majeraha ya mfupa na nyuzi ngumu za tendon na ligamenti, fahamu kuwa itachukua muda kupona kabisa na kurudi mchezoni.

Mwanamichezo anahitajika kujifahamu na kujidhibiti binafsi na maumivu yake ikiwamo kujua yanachokozwa na mambo gani, je yanaanzaje wakati wakuanza, katikati au mwishoni baada ya mazoezi/mchezo?

Vema pia kufahamu kuwa maumivu yanauma unapominywa au yanakuwepo tu yenyewe, je yanasambaa au yanaibukia sehemu nyingine. Kila tabia ya maumivu ya mwili hutoa picha ya chanzo chake na ukubwa wake.

Wataalam wa tiba za afya za michezo huweza kugundua na kutibu maumivu, kuyatathimini madhara yake kiujumla na huku wakitambua mjongeo wa mwili ambao unaweza kuchochea tatizo hilo kuendana na jeraha lilipo katika mwili.

Baadhi ya makocha, viongozi na mashabiki ndio wanakawaida ya kushinikiza wachezaji walio na majeruhi na maumivu kuwapa dawa za maumivu.

Ikumbukwe kuchoma sindano na kunywa dawa za maumivu zinakwenda kuondoa maumivu na kukupa utulivu kwa muda tu na si kukarabati jeraha na kuliponyesha kabisa.

Hata pale anapopona mfupa, msuli au tishu zilizojeruhiwa kwa mara nyingine, hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa kwani tishu hizo zinapungua uimara kuweza kuhimili michezo na mazoezi.

Ni vizuri kuepuka kumchezesha mchezaji au kucheza akiwa na maumivu au majeruhi. Vizuri kuzingatia ushauri wa madaktari wa timu na wataalam wengine wa afya.

Kutumia dawa holela za maumivu ni hatari

Wanamichezo wengi hupatwa na majeraha mbalimbali wakati wa kucheza ikiwamo kuchanika misuli, michubuko, kuvilia damu, kuteguka viungo na kuvunjika mifupa ya mwili.

Majeraha ya michezo yanaweza kuzuilika lakini ni kawaida kutokea unapocheza. Unaweza usipate majeraha kwa ajali au faulo wakati wa kucheza lakini ukapata majeraha mwilini kutokana na kufanyishwa mazoezi magumu kupita kiasi.

Majeraha ni kawaida kuambatana na maumivu ambayo huwa ni kama kero na yakizidi huwa ni mateso. Hali hii ndiyo huwapa ushawishi wa kutumia dawa za maumivu bila maelekezo ya madaktari.

Ni sahihi kutumia dawa hizo unapokuwa na maumivu kiasi na huku unahitaji kucheza kama huongezi ukubwa wa jeraha, lakini huwa sio sahihi inapotokea na kujengeka kuwa ni mazoea kila wakati.

Jambo la msingi kabla ya kutumia dawa zozote vizuri kumwona mtaalam wa afya aliye jirani nawe au mjulishe daktari wa timu kuwa una maumivu yeye ndiye atakayeamua.

Dawa za maumivu ziko za aina nyingi na kila moja au kila jamii ya dawa hizo huwa na kazi tofauti. Zipo zakukabiliana na madogo mpaka ya kati na zipo za maumivu ya kati mpaka makali.

Vile vile dawa hizi huwa na maeneo maalum ya mwilini inapokwenda kufanya kazi. Zipo ambazo ni maalum kwa ajili maumivu ya kichwa tu, tumbo, misuli ya pembezoni mwa mwili na mishipa ya fahamu.

Hutokea wachezaji wakapata uraibu wa kutumia dawa za maumivu kutokana na kutumia mara kwa mara kiholela. Hufanya hivyo wakidhani ndiyo wanatibu jeraha kumbe ni kukata maumivu tu lakini tatizo lenyewe haliponi kwa dawa hizo

Tabia hii huwakumbuka sana wachezaji wenye maumivu sugu ya viungo vya mwili. Pasipo kujua kuwa kadiri unavyosababisha uungaji wa jeraha kuchelewa na ndivyo pia huchukua siku nyingi kuwa imara kwa asilimia 100%.

Dawa nyingi za maumivu zimechanganywa changanywa kitaalamu na nyingi zinakuwa na majina ya kibiashara.

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa matumizi ya kiholela ya dawa za maumivu hazina faida yoyote kwa mchezaji akiwa na maumivu na kuhitaji kucheza mechi.

Kazi inayofanya ni kukata maumivu wakati tatizo liko palepale, hivyo kucheza huku unatumia dawa jeraha nalo huongezeka ukubwa au kujeruhiwa tena matokeo yake kuchukua muda kuunga na kupona.

Chukua hii

Wanasoka ni vizuri kushikamana na ushauri wa wataalam wa afya na kuepuka kucheza na maumivu pamoja na matumizi holela wa dawa za maumivu.

Columnist: Mwanaspoti