Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ushiriki wa watu kuhusu uamuzi wenye kuathiri mazingira yao

Eddcd36579dab8037f4cb87f81467e4a Ushiriki wa watu kuhusu uamuzi wenye kuathiri mazingira yao

Wed, 23 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

USIMAMIZI endelevu wa mazingira, pamoja na mambo mengine, unaweka msisitizo mkubwa kwenye ushiriki wa watu katika ngazi zote za uamuzi hasa yanayoweza kuathiri mazingira yao kwa namna moja au zaidi.

Msingi wa ushiriki wa watu umejengwa juu ya dhana ya kuwa watu ndio chanzo cha mamlaka yote ya serikali kama ielezavyo ibara ya 8(1), (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Ushiriki wa watu ni zaidi ya kuzungumza na kusikilizwa. Ushiriki wa watu ni maingiliano kati ya watu na serikali. Ushiriki wa watu ni maingiliano yanayowapa watu nafasi ya kuibua masuala, kuainisha vipaumbele, kupendekeza mpango kazi, kuonesha suluhisho na pia kupendekeza namna bora ya matumizi ya rasilimali na uwajibikaji katika kutekeleza maamuzi.

Mwanasheria kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Clay Mwaifwani, anasema kuwa ushiriki wa watu hauiondoi serikali kwenye nafasi yake kama wafanya uamuzi, la hasha!

Ila anasema unaileta serikali karibu na watu na kuwapa watu umiliki wa uamuzi na mabadiliko. Ushiriki wa watu huongeza uhalali na kukubalika kwa serikali na mipango yake ya maendeleo kwa watu. Hii ni kwa sababu watu walifanyika kiini cha uamuzi wa serikali tangu awali.

Vivyo hivyo kwenye usimamizi wa mazingira, serikali inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa na kusimamiwa kwa namna inayowezesha kufanyika kwa shughuli za uzalishaji leo bila kuathiri uwezo wa mazingira hayohayo kuzalisha kwa ajili ya vizazi vya kesho na kesho kutwa.

Katika kufanya uamuzi wowote unaoweza kuathiri mazingira, serikali inao wajibu wa kuhakikisha kuwa watu wanashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kufikiwa kwa uamuzi huo.

Kanuni ya 10 ya Tamko la Rio la Mazingira na Maendeleo la mwaka 1992 inaeleza kuwa masuala yote ya mazingira yatatekelezwa kwa ufanisi na yatakuwa yenye matokeo chanya iwapo yatatekelezwa kwa kuzingatia ushiriki wa kila mmoja.

Kanuni hiyo inaenda mbele kwa kueleza kuwa ushiriki wa watu unakamilika na kuwa ushiriki kamili iwapo watu wote wanaweza kupata taarifa zote muhimu zihusuzo mazingira.

Tamko la Rio la Mazingira na Maendeleo la Mwaka 1992 limefanywa kuwa msingi wa sheria za usimamizi wa mazingira na uhifadhi wa rasilimali za maliasili sehemu nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 (Sheria Namba 20 ya Mwaka 2004) chini ya kifungu cha 178 inaeleza kuwa watu wote watakuwa na haki ya kupewa taarifa kwa wakati kuhusiana na mpango wowote wa kiutawala unaoweza kuathiri mazingira yao na pia watakuwa na haki ya kushiriki katika mchakato huo wa uamuzi.

Sheria hiyo inaenda mbele kwa kutaja baadhi ya mambo ambayo watu watakuwa na nafasi ya kushiriki katika ngazi zote za uamuzi na mambo hayo ni pamoja na maandalizi/utungwaji wa sera za mazingira, mikakati, mipango, sheria na kanuni zinazosimamia uhifadhi wa mazingira.

Ushiriki wa watu kwenye usimamizi wa mazingira na maliasili unaweza kufanywa kwa ufanisi zaidi katika ngazi za chini za utawala kama vile ngazi za serikali za mitaa ama serikali za vijiji. Mikutano ya serikali ya vijiji ama mitaa ni jukwaa sahihi katika kuhakikisha watu wanashiriki kikamilifu kwenye usimamizi wa mazingira na maliasili.

Ushiriki wa watu kwenye usimamizi wa mazingira na maliasili unasimamiwa na sheria, kama ilivyoelezwa kwenye aya zilizopita. Kuwapo kwa sheria yenye kueleza juu ya utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuwezesha ushiriki wa watu ni jambo moja ilihali ushiriki kamilifu wa watu ni jambo jingine linalohitaji mjadala mpana pia.

Mwanasheria mwingine kutoka LEAT, Baraka Thomas anasema kuwa ushiriki wa watu kwenye usimamizi wa mazingira hauishii kwenye sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 pekee bali unaenda mbali na kuhusisha sheria zote zinazohusu usimamizi wa raslimali za maliasili.

Misitu ni rasilimali mojawapo kati ya rasilimali nyingi zinazosimamiwa na kulindwa na sheria za Tanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (Sura ya pili ya Sheria za Tanzania, toleo la mwaka 2005) chini ya ibara ya 145, inaanzisha mamlaka ya serikali za mitaa na ibara ya 146 ya katiba hiyo inaeleza wazi kuwa madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka ya serikali za mitaa ni kupeleka madaraka kwa watu.

Rasilimali misitu, kwa misitu iliyoko vijijini kwa maana ya kuwepo kwenye ardhi ya ardhi ya kijiji, inasimamiwa na vijiji husika na mamlaka ya juu ya uongozi wa kijiji ni mkutano mkuu wa kijiji. Licha ya ukweli kuwa wanakijiji ndio walinzi wa misitu bado maamuzi ya kuvuna au kutovuna rasilimali misitu hufanywa na ofisa misitu wa wilaya.

Mfumo wa utendaji wa namna hiyo unawapa watu haki ya kushiriki katika usimamizi wa mazingira na rasilimali za maliasili kwa mkono mmoja na kuipora haki hiyo kwa mkono mwingine. Mbali na kutoa haki na kupora, sheria bado zina mianya mingi inayowanyima watu haki ya kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mazingira na raslimali zao.

Mfano wa mianya hiyo ni utungwaji wa sheria kwa hati ya dharura. Hati ya dharura ni jambo halali kabisa lililowekwa kwa mujibu wa sheria na litafaa iwapo litatumika kwenye mambo ya dharura.

Mambo mbalimbali yanayofanyika wakati wa utungwaji wa sheria kwa hati ya dharura huwanyima watu nafasi ya kushiriki kikamilifu katika utungwaji wa sheria hivyo kwenda kinyume na dhana ya ushirikishwaji kama watu.

Mfano wa sheria zilizotungwa kwa hati ya dharura ni sheria ya Umiliki wa Milele wa Utajiri wa Taifa na Rasilimali za Maliasili ya Mwaka 2017 (Sheria namba 5 ya Mwaka 2017).

Kwa kutunga sheria kwa hati ya dharura watu wanakosa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuamua hatma ya mazingira na rasilimali za maliasili na pia wawakilishi wao wanakosa nafasi ya kufanya mijadala mipana na kurudi majimboni kufanya mikutano na watu na kuchukua maoni yao na kuyapeleka bungeni.

Mbali na watu kukosa nafasi ya kufanya uamuzi wa uvunaji wa rasilimali na pia kukosa nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye utungwaji wa sheria zinazotungwa kwa hati ya dharura, bado kuna changamoto nyingine nyingi zinazowakosesha watu nafasi ya ushiriki na moja wapo ni kukosekana kwa mindombinu wezeshi ili kutimiza matakwa ya kisheria juu ya ushirikishwaji.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 chini ya kifungu cha 178(5), (a) inaeleza kuwa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira litakuwa na wajibu wa kuandaa midahalo mbalimbali ili kupata maoni ya watu.

Swali la msingi ni je, kuna mazingira rafiki ya kuwezesha midahalo nchi nzima ilihali sheria zenye kuhifadhi mazingira na maliasili zinatungwa kwa hati ya dharura?

Sheria inaeleza wazi watu watakuwa na haki ya kupata taarifa mapema juu ya nia ya kuandaa sera ama kutunga sheria, lengo la kuweka wazi nia hiyo ni kuwapa watu muda wa kutafakari na pia kuandaa maoni yao.

Sheria inawapa watu haki ya kupata taarifa sahihi zihusuzo mazingira. Swali ni je, muda wa kutafakari nia ya serikali na kupitia taarifa muhimu uko wapi ilihali sheria inaenda bungeni kwa hati ya dharura?

Mbali na maswali hayo, swali kubwa zaidi linalohitaji kujibiwa na pengine majibu ya swali hilo yatatosha kujibu na maswali ya awali ni je tunatunga sheria zenye kusimamia mambo muhimu kwa taifa kwa hati ya dharura kwa haraka ipi?

Usimamizi bora wa mazingira unaweza kuumaliza ule wimbo wa kutokomeza ujinga, maradhi na umasikini hata hivyo yote yatawezekana iwapo usimamizi huo utafanyika kwa maslahi ya watu na namna bora ya kuyafikia maslahi ya watu ni kuwapa watu umiliki wa mchakato yaani ushiriki unaohama toka kwenye maandishi ya sheria na kuwa dhahiri kwa kuandaliwa mazingira rafiki ya utekelezwaji.

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inaamini kuwa ustawi wa kesho na kesho kutwa wa taifa letu upo kwenye usimamizi dumivu wa mazingira na raslimali za maliasili. LEAT inapigia chapuo ushiriki wa watu katika kufanya maamuzi yanayoweza kuathiri mazingira yao pamoja na raslimali za maliasili zinazowazunguka.

Ushiriki wa watu sharti uwe ushiriki kamilifu wenye kuwapa watu na wawakilishi wao muda wa kutosha kutafakari, kuandaa hoja zao, kutoa maoni yao kwenye mijadala na midahalo mbalimbali na pia kuipa serikali nafasi ya kupokea maoni, kuainisha maoni yapi itayafanyia kazi na maoni yapi haitayafanyia kazi na sababu za kutoyafanyia kazi ni zipi.

Mtu mmoja amewahi kusema weledi wa taifa utapimwa kwa namna taifa linavyoyasimamia mazingira yake. Wote tunao wajibu wa kuyatunza mazingira yetu, hata hivyo wajibu huo utatekelezeka iwapo namna bora ya kuyatunza mazingira ni matokeo ya mchakato wa pamoja. Tushirikishane.

Columnist: habarileo.co.tz