Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ushirika una nafasi kubwa kuwakomboa wanawake

4ad782379a94663ce4ed459a647142db Ushirika una nafasi kubwa kuwakomboa wanawake

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWANAMKE ndio msingi wa malezi ya jamii zetu na hii ni kutokana na majukumu na uwezo walionao katika kulea, kutunza familia na jamii zinazowazunguka. Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke na katika kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia, dunia jana iliadhimisha siku ya Wawanawake.

Wanawake wengi wameonekana katika harakati mbalimbali za kujikwamua kiuchumi, wamekuwa wakijiunga na vikundi vinavyowaunganisha kwa lengo la kupata mitaji, masoko au uendeshaji wa miradi mbalimbali kama vile kilimo, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika Ushirika wanawake wana fursa ya kuwa wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika wa nyanja mbalimbali kutokana na ukweli kwamba ushirika ni sekta mtambuka yenye wigo mpana kiuchumi.

Maeneo mengi ya nchi yana ushirika wa aina mbalimbali ikiwemo Kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ufugaji, Nyumba na nyingine, zote hizi zikiwezesha kutoa fursa nyingi kwa mwanamke kuchagua na kushiriki kulingana na nafasi, eneo, uwezo na maamuzi binafsi.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dk Benson Ndiege anabainisha kuwa Wanawake wanaweza kunufaika na fursa za Ushirika kwa kujiunga pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja katika kutafuta na kutumia fursa zinazowazunguka katika nyanja mbalimbali.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Dk Ndiege anatolea mfano Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) ambavyo vinapatikana maeneo mengi hapa nchini akisema wanawake wanaweza kutumia vyama hivi kutokana na upatikanaji wake kuwa rahisi, na kuwa masharti na vigezo nafuu vinavyoweza kuwasaidia wanawake wengi kuanzisha biashara, mashamba, ujenzi na masuala mengi yenye kuongeza tija na maendeleo.

Akizungumzia masuala ya ufugaji na wanawake, Meneja wa Chama cha Ushirika wa Wafugaji Ng’ombe Wilaya ya Korogwe (UWAKO), Zamuata Ismail, anasema chama hicho kina wanachama wanawake ambao wanaendesha shughuli za ufugaji na ukusanyaji maziwa.

“Uwako inawaunganisha wafugaji hao na wanunuzi mbalimbali kwa uhakika wa soko la maziwa. Tumekuwa tukipata wanunuzi wa maziwa wanatoka ndani na nje ya Wilaya ya Korogwe," anasema Zamuata

Anaongeza: “Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wanawake na mabinti hususani wanaomaliza masomo yao katika ngazi ya elimu kujishughulisha na ufugaji katika maeneo yao na pia kujiunga na vyama vya ushirika ili kupata uhakika mitaji, masoko na ushindani wa bei.”

Anasema ushirika ni nyenzo muhimu inayowezesha kutosheleza na kufikia mahitaji makubwa ya masoko ambayo inaweza kuwa changamoto kwa mfugaji mmoja mmoja.

“Wanawake wenzangu tusifikiri kuwa shughuli za ufugaji ni za wanaume pekee yake, tuingie kwenye ufugaji hasa wa ng’ombe wa maziwa kwani ufugaji ni zaidi ya biashara. Ukiweza kupata maziwa na uhakika wa soko kupitia ushirika kama ilivyo hapa Uwaki kwa kweli tutafanikiwa kupunguza na hatimaye kuondokana na umaskini.”

Naye Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Ushirika wa Mkonge Magunga Amcos wilayani Korogwe, Asha Hiza anasema kuchaguliwa kwake kuwa mjumbe wa bodi ni baada ya kujishughulisha na kilimo cha mkonge kwa kipindi kirefu.

“Pamoja na kujishughulisha na kilimo bado anaweza kutekeleza majukumu yangukama mama wa familia. Kilimo hiki kimeniwezesha kusomesha watoto, kununua kiwanja na hivi sasa anajenga nyumba ya kisasa wilayani Korogwe.”

Akitolea mfano kuhusu mauzo ya hivi karibuni, Asha anasema kuwa mkonge umekuwa ukiuzwa kwa takribani kiasi cha Sh milioni 3.5 kwa tani moja, bei ambayo inawatia moyo wakulima kulima na kuuza kupitia ushirika ukilinganisha na awali walipokuwa wakiuza kwa wanunuzi na kampuni binafsi ambao walikuwa wakinunua kwa bei ndogo isiyo na tija.

“Niwatie moyo wanawake kuanza kulima mkonge si lazima uwe na fedha nyingi unaweza ukaanza ekari moja mwaka huu na ukawa unaongeza kulima ekari zaidi kulingana na uwezo wako, kina mama tuingie kwenye kilimo cha mkonge kinalipa tena kinalipa haswa.”

Naye Meneja wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha kinachohudumia Wanawake wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera (Kawosa), Goliath Elias anasema katika jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi hususani wa maeneo ya vijijini, chama hicho kilianzisha programu ya kuwalipia karo za shule watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

“Baadaye tulibadili utaratibu na kuanza kuwatafuta mama wa watoto hao ambao walifundishwa ujasiriamali wa aina mbalimbali na hatimaye kuanza kuwakopesha lengo likiwa ni kuweza kuwainua kiuchumi wao hivyo kumudu kuendesha maisha yao na ya familia zao.”

Naye mmiliki wa shule ya awali ya Cherish Daycare and Nursery, Ela Fute anasema mkopo aliouchukua UDOM Saccos ulimwezesha kujenga madarasa, kununua gari kwa ajili ya watoto pamoja na kujenga nyumba yake ya makazi.

“Saccos imenisaidia sana, kwani awali sikuwa na madarasa nilianzia shule yangu na darasa mmoja nikiwa nimeanza na mtoto mmoja, nashukuru watoto wameongezeka na nimefanikiwa kuongezavyumba vya madarasa.”

Aidha, Dk Ndiege anaongeza kusema kuwa: Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 itaendelea kutekeleza jukumu la kusimamia na kuhamasisha makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo wanawake, Vijana na wenye Ulemavu kujiunga na kunufaika na fursa za Ushirika ili kujikwamua na kujiendeleza kiuchumi.

Columnist: www.habarileo.co.tz