Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usalama wa wananchi EAC uwe kipaumbele

EAC EAC Usalama wa wananchi EAC uwe kipaumbele

Tue, 11 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

Iko mbioni kuipokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa nchi mwanachama ikiwa ya saba.

Nchi ambazo tayari ni wanachama ni, Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Hizi ni nchi ambazo kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa wanachama wa EAC, ni jirani.

Hali hii imekuwapo muda mrefu kiasi kwamba, baadhi ya makabila yaliyo katika nchi moja, hupatikana katika nchi nyingine, kwa mfano, Wamasai wanapatikana Tanzania lakini hata Kenya wapo.

Hii ni kusema kuwa, nchi hizi na nyingine majirani ambazo hazijawa wala hazijafikiria au kufikiriwa kuwa wanachama wa AEC, ni majirani wanaopaswa kushirikiana kwa mambo mengi yakiwamo ya usalama na kuzuia uhalifu mbalimbali.

Huu ni pamoja na umiliki, utumiaji na biashara haramu ya silaha, ugaidi, bishara ya binadamu na hata kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya na wizi ukiwamo wa mifugo.

Kwa msingi huo, nchi zote ziweke bidii kuelimisha na kuhamasisha wananchi wao kuonana kama ndugu wa damu na hivyo kuwa aibu kubwa kwa mwananchi wa nchi moja kufanyiwa unyama, kuteswa na hata kuonewa katika nchi nyingine.

Hili libebwe kama ajenda ya jamii nzima kufichua uhalifu na wahalifu kabla hata hawajafika wala kutekeleza uhalifu katika nchi nyingine.

Matukio yanayosikika mara kwa mra ya baadhi ya watu wa nchi moja mwanachama wa EAC kukutwa nchi nyingine wakifanya au kutaka kufanya uhalifu, yawe aibu katika nchi wanachama wa EAC na jirani zao.

Kwa msingi huo, nchi zote zikatae kwa dhati kulea uhalifu unaovuka mipaka kwani ndio husababisha wahalifu wakiwamo magaidi kufanikiwa kufanya uhalifu katika nchi nyingine na kujificha katika nchi nyingine.

Wananchi pia wasikubali mali za wizi kama mifugo kuingia au kutoka nchini mwao na hivyo kuungana na kushirikiana na vyombo vya usalama vya nchi husika kudhibiti uhalifu kama huo.

Iwe aibu kwa mwananchi wa nchi mwanachama wa EAC kufanya au kufanyiwa unyama na wananchi au chombo chochote cha umma katika nchi nyingine mwanachama.

Nionavyo mimi, tukizingatia hayo, tutadhibiti wizi, mauaji, mapigano, magendo, ugaidi na chuki miongoni mwa raia wa nchi wanachama kwani hazina tija badala yake, kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili kuimarisha amani na shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Kukiwa na uhakika zaidi wa usalama na amani katika nchi hizi, uzalishaji mali na shughuli nyingine za kijamii zitafanyika kwa tija zaidi, lakini kinyume chake, kila mmoja ajue kuwa kama jirani yako si salama, nawe si salama.

Ninasema: “Usalama wananchi EAC uwe kipaumbele.”

Columnist: www.habarileo.co.tz