Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usajili wa Akpan Simba na kilio cha Mzamiru

Victor Akpan Ff Victor Akpan, anatajwa kumalizana na Simba SC

Wed, 29 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna wakati asili ya maisha yanashindwa kutenda haki kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa na juhudi kubwa kwenye kazi za maisha yao. Yupo ambaye anaweza kufanya kazi ya kawaida akapata heshima kubwa kutoka ndani ya taasisi fulani lakini pia yupo mwingine anaweza kuwa na mchango mkubwa lakini heshima yake ikawa ya kawaida.

Soka letu sasa lipo kwenye kipindi cha usajili ingawa dirisha rasmi bado halijafunguliwa,kila timu inapiga hesabu za jinsi gani waweze kuwa na msimu bora ujao baada ya kuangalia wapi wamepungukiwa katika msimu huu.

Simba ambao wamepoteza mataji yote waliyokuwa wanayatetea msimu huu nao ni moja ya timu ambayo inapiga hesabu hizo za kuboresha timu yao.

USAJILI WA AKPAN

Simba inahusishwa na usajili wa kiungo wa Coastal Union Victor Akpan ambaye ni raia wa Nigeria, mbio hizi zilikolea sana siku tatu zilizopita wakitajwa kugombania saini ya kiungo huyo na klabu ya Azam FC.

STAA GHALI KWELI?

Inawezekana Akpan akiwa mmoja wa wachezaji bora waliofanya vizuri katika eneo la kiungo cha Coastal lakini kitu ambacho kimewashtua wengi ni kauli za baadhi ya wadau Coastal Union kwamba usajili wa kiungo huyo mkabaji ni Sh100milioni.

Kiasi hicho ambacho inaelezwa Simba wako njiani kukitoa, ingawa ni siri ni sh 100 milioni, lakini mbali na hapo namba hizo zimezidi kuwa kubwa kiasi cha kushtua. Swali ambalo wengi tumekuwa tukijiuliza hii ni thamani halisi ambayo inastahili au kuna mambo mengine nyuma ya pazia kutoka kwa wahusika wanaosimamia hizi sajili?

Akpan ni kiungo mzuri ambaye ameipa thamani yake Coastal lakini kwa Simba ambayo inafikiria kucheza Nusu Fainali ya Kombe la Afrika, walitakiwa kupima sawasawa juu ya aina ya viungo wake ambao walikuwemo katika misimu hii miwili katika eneo la Mnigeria huyu kisha kujiuliza wanafanya maamuzi sahihi?

Kama majibu yatakuwa sahihi kwao basi tunaweza kuwaruhusu kuendelea na hesabu hizo lakini mwisho wa siku wao viongozi ndio wa mwisho kulaumiwa.

THAMANI YAKE DHIDI YA MZAMIRU

Wakati mjadala huu ukiendelea wa usajili wa Akpan, hapohapo Simba kuna kiungo mwingine anahitaji kuongezewa mkataba, Mzamiru Yassin. Za ndani kabisa ni kwamba thamani yake ni Sh40Milioni. Mtu mmoja mfupi asiye na maisha ya makeke nje ya uwanja na hata ndani ya uwanja, yupo pale Msimbazi kwa muda sana akishuhudia msururu wa majina ya kigeni yakiingia na kutoka.

Mzamiru taarifa zinasema bado hajaongeza mkataba ndani ya klabu hiyo na kitu kikubwa ni kiasi cha fedha anachotaka kiongezwe kutokana na ubora wa kazi yake ndani ya muda ambao amedumu Simba.

Huyu ndiye kiungo ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa inayojificha katika macho ya wanaoangalia mpira juu juu akipewa mpaka jina la ‘kiungo punda’ kutokana na utumishi wake wa kukaba bila kuthaminiwa.

Sio rahisi hata ungekuwa wewe unayesoma makala hii kukubaliana na maisha ya kazi kubwa unayofanya kisha ukapewa fedha kiduchu.

Sakata la Mzamiru linanikumbusha kiungo mmoja wa zamani wa Real Madrid Claudio Makelele ambaye alikuwa na kazi kubwa uwanjani lakini fedha anayolipwa ilikuwa ndogo akizidiwa hata na wachezaji baadhi wanaokaa benchi wakati huo.

Makelele baadaye alishindwa kukubaliana na Madrid kisha akaamua kuyakimbilia maisha yenye thamani kwake akitimkia Chelsea ambayo ilitambua nguvu yake.

Simba haipaswi kusubiri mfano huu wa Makelele utumike kwa Mzamiru ambaye kazi hiyo bora imekuwa akiifanya hata katika timu ya taifa Taifa Stars.

Simba wakumbuke tu katika takwimu bora kabisa kutolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) dhidi ya Mzamiru kiungo huyu punda alikimbia umbali wa kilometa 11.06 akicheza dhidi ya timu ngumu kabisa Afrika Algeria, akiwa ndiye mchezaji aliyekimbia umbali mrefu zaidi kuliko wote.

Thamani kama hii anayokupa Mzamiru unaipata wapi kwingine zaidi ya kutakiwa kuheshimu namba kama hizi. Simba inapaswa kumpa Mzamiru na mastaa wengine wazawa wenye uwezo heshima na thamani wanayostahili.

Columnist: Mwanaspoti