Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Upendeleo kwa waamuzi - 4

Waamuzi Zz.jpeg Upendeleo kwa waamuzi - 4

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jana katika mfululizo wa Ripoti Maalumu kuhusu waamuzi wa soka nchini, tuliona namna wanavyolipwa, madeni wanayobeba na jinsi wanavyobanwa kwenye kukumbushia malimbikizo yao.

Pia iliwekwa bayana namna waamuzi wanavyokumbana na changamoto nyingi ikiwamo ya kupimwa na makamisaa na kupewa alama zinazoweza kuwabeba au kuwaangusha.

Leo tunaendelea na kipengele hicho kabla ya kugeukia juu ya tuhuma za kuwepo kwa upendeleo kwa baadhi ya waamuzi na kupewa mechi mfululizo sambamba na madai ya kuhusishwa na rushwa. Je kuna ukweli katika madai hayo? Endelea nayo upate majibu.

Referees Facilitator ndio hao wanakwenda kuwanoa 'match commissioner' wakikuandikia 'ziro' ujue biashara yako imekwisha. Hivi msimu mzima (2018/19) ligi haikuwa na mdhamini, hamkujiuliza waamuzi walikuwa wanapata wapi pesa za kujikimu? Mambo ni mengi muda mchache kaeni kwa kutulia, hii ligi kuna watu wananeemeka. Waamuzi tunabebeshwa tu mzigo.

UPO UPENDELEO?

Umewahi kujiuliza kuna nini hata waamuzi wanakuwa ni walewale? Nini kimejificha nyuma ya pazia kwa hawa waamuzi? Rekodi zinaonyesha katika misimu mitano wamekuwa wakitembea na timu kongwe za Simba na Yanga mara nyingi zaidi.

Ramadhan Kayoko, Ahmed Arajiga na Heri Sasii ni baadhi ya waamuzi wanaojirudia kila mara kwenye mechi zinazohusu timu hizo kongwe za soka katika misimu mitano iliyopita.

MSIMU HUU

Katika michezo minane ya kwanza ya Yanga msimu huu (wakati makala hii ikiandaliwa), Heri Sasii ndiye aliyekuwa kinara akichezesha michezo mitatu na ikishinda yote ambapo alianza dhidi ya Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting na ule wa KMC uliopigwa Oktoba 26.

Kwa upande wa Ramadhan Kayoko alichezesha michezo miwili ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania na Simba huku Ahmed Arajiga kutoka Manyara, Raphael Ikambi (Morogoro) na Florentina Zablon wa Dodoma wakichezesha mechi moja kila mmoja wao.

Kwa Simba mwamuzi anayeongoza kuichezesha ni Kayoko ambaye katika michezo minane ya kwanza msimu huu, aliichezesha minne akianza na dhidi ya KMC, Dodoma Jiji, Yanga na Azam FC huku Ahmed Arajiga akichezesha miwili dhidi ya Geita Gold na Tanzania Prisons.

Hance Mabena (Tanga) alichezesha dhidi ya Kagera Sugar huku Tatu Malogo pia wa Tanga akichezesha mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.

MISIMU ILIYOPITA

Katika misimu iliyopita na sasa hakuna mabadiliko sana kwenye uteuzi wa waamuzi kwenye michezo mikubwa kwani mara kwa mara wamekuwa wakijirudia wale wale ambao wamekuwa wakionekana mbele ya hadhira.

Waamuzi Jonesia Rukyaa (Kagera), Emmanuel Mwandembwa (Arusha), Herry Sasii (Dar es Salaam), Ramadhan Kayoko (Dar es Salaam) na Ahmed Arajiga kutoka Manyara ni miongoni mwa waliochezesha nusu ya michezo yote ya vigogo nchini.

Mbali na hao wengine ambao wamepata nafasi ya kuchezesha mara moja moja ni Nassoro Mwinchui (Pwani), Abel William (Arusha), Raphael Ikambi (Morogoro), Hance Mabena (Tanga), Martin Saanya (Morogoro), Abdallah Mwinyimkuu (Singida), Gilbert Mrina (Kilimanjaro), Ahmada Simba (Kagera) na Joachim Akamba wa Mbeya.

Mmoja wa waamuzi wa kati nchini anasema sababu kubwa ambayo imekuwa ikiwafanya waamuzi wachache kusimamia michezo ya klabu kubwa hizo kongwe kwanza ni ubora wao, ingawa pia amekiri kuwepo na dosari katika uteuzi wa wahusika hao.

Anasema mchakato huo huleta ukakasi mkubwa kuanzia katika mazoezi ya kupima ubora wa waamuzi ambapo hutokea waamuzi licha ya kuonekana uwezo wao ni sawa na wengine lakini bado baadaye hupewa majukumu hayo.

"Unajua nchi yetu hii tunaijua, sikatai kwamba mwamuzi wa kusimamia mechi kama hizi lazima rekodi zake zimbebe kwa kuchezesha vyema, unaweza kujiuliza kwanini waamuzi wa pembeni hawamlalamikii Komba (Aloyce) kwa kuwa wanamuona ubora anao hata kama atakuwa na makosa machache," alisema mwamuzi huyo.

"Hivyohivyo unaweza kujiuliza kwanini sisi waamuzi wa kati hatumlalamikii dogo Kayoko (Ramadhan) unamuona kwamba sasa hivi ameimarika lakini waangalie wengine kwanza wamekuwa na makosa hatarishi yanayojirudia lakini bado wanapewa hizo mechi.

"Angalieni pia hata hizi adhabu zinazotoka wale waamuzi wao hupewa adhabu kwa ugumu sana lakini makosa hayohayo ndio wanahukumiwa vibaya wengine, utaona hapo shida ilipo."

Mwamuzi mwingine wa pembeni kutoka jiji la Dar es Salaam alisema hakuna usawa katika kupeana nafasi za kuchezesha mechi hizo kubwa na akaenda mbali zaidi akidai yapo mazingira ya wenzao kuishi vizuri na wakubwa wanaoongoza mpira na waamuzi.

"Kila mwamuzi anapoingia kwenye taaluma hii anatamani kuchezesha hizi mechi kubwa, mimi naona kwanza tunaangushwa na mafunzo yenyewe, sioni kama wote wanaochezesha hizi mechi wamefaulu vizuri, shida ni kwmaba na ninyi waandishi mnakuja tu uwanjani lakini mngekuwa mnakuja kuona tunavyoandaliwa.

"Jingine ukweli ni kwamba kila mwamuzi anatamani kuwa sehemu ya kuamua hizi mechi kubwa lakini shida inakuja ni jinsi gani utakuwa unapatana na wakubwa wenye uamuzi, ndio maana unaona hata adhabu zetu pia zinatofautiana, sisi tunahukumiwa kwa makali zaidi na wewngine utaona jinsi adhabu inavyozunguka."

Sambamba na huyo, mwingine alidai: "Kila mwamuzi ndoto yake ni kuchezesha timu kubwa kwa hapa kwetu ni Simba na Yanga, timu ambazo zimefanikiwa kujizolea umaarufu mkubwa nje na ndani kutokana na kuwa na mashabiki wengi.

“Kupotea kwa waamuzi pia kunatokana na kukatishwa tamaa na wasimamizi wao ambao wanashindwa kuwaamini na kushindwa kuwapa nafasi ya kuchezesha mechi za ndoto yao, wanajiona hawakui wanaishia chini, wanaamua kujiengua na kufanya mambo mengine.”

Anasema ukubwa wa mechi ya Simba na Yanga unakuza na kumshusha mwamuzi kutokana na namna mwamuzi anavyoweza kumudu kutokana na presha kubwa ya mchezo wenyewe na ndio maana waamuzi wengi wachanga wanatamani kukua lakini sio rahisi kwao kupata nafasi hiyo.

Columnist: Mwanaspoti