Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Unyanyapaa ni `kifo’ upo hospitalini, jamii, nyumbani

Mon, 15 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

USIKU wa kuamkia Aprili 19, 2020 umeandika historia katika maisha ya Hemed Mwanansali, mwalimu wa Shule ya Msingi Tandahimba mkoani Mtwara, kwani ndiyo siku alipoanza kuziona dalili za maambukizo ya corona zilizoanza kwa maumivu makali ya kichwa na taya la kulia.

Anapata dalili hizo siku 15 baada ya kurejea Tandahimba akitokea Dar es Salaam na kwamba aliondoka Dar Aprili 4, 2020 baada ya kukamilisha mambo aliyokuwa anayafuatilia.

Leo Mwanansali aliyeathirika na COVID -19 ameshapona na kujiunga na familia yake baada ya kutengwa nao kwa siku 21 za kuwekwa karantini.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni wilayani humo, Mwanansali anasema kuumwa corona ni tatizo kubwa lakini kilichomtesa zaidi ni kupambana na unyanyapaa kuliko hata ugonjwa wenyewe.

“Nilipata tatizo hili usiku wa kuamkia Aprili 19. Kihistoria nina matatizo ya kiafya yaliyonipata miaka minne iliyopita ninaumwa kichwa na taya la kulia, halafu maumivu yakiisha sikio la kulia linatoa maji ,” anasimulia Mwanansali.

Anasema ugonjwa huo humpata kila baada ya mwezi mmoja au mitatu na kwamba anajitibu kwa dawa za miti kwa kuchemsha na kunywa maji ya maganda ya mbuyu na mlonge.

ALIVYOPATA CORONA

Akieleza jinsi alivyokutwa na maambukizo Mwanansali anasema usiku wa kuamkia Aprili 19 alipata maumivu makali ya kichwa na taya na kudhani ni ugonjwa unaomsumbua mara kwa mara.

“Maumivu hayakuisha hadi asubuhi, Niliamua kwenda hospitali kupimwa.Nilipofika hospitali pale getini wameweka utaratibu wa kupima joto la mwili. Nilipimwa na kukutwa na nyuzi 36.5 ambalo ni joto la kawaida. Kisha nikaenda kumwona daktari, nikamweleza ninavyojisikia na nikaomba kupima malaria.

“Lakini daktari alishtuka akasema mbona ni dalili za corona? Ghafla nikamwona daktari amepata mshtuko na kunipa barakoa nivae. Aliniuliza kama nilisafiri siku za karibuni. Nikamjibu nimerudi kutoka Dar es Salaam tangu Aprili 4 ambao ni muda mrefu,” anasema.

Anasimulia kuwa daktari alikwenda kushauriana na wenzake kuhusu hali yake na ghafla kukawa na taharuki hospitalini hapo ambapo madaktari walifanya vikao kumjadili.

“Nilitarajia madaktari na wahudumu wa afya wangenitia moyo, lakini mimi ndiyo nilikuwa nawatia moyo kwani walikuwa kwenye taharuki. Nilishtukia habari zangu zimeanza kuenea hospitali hapo na mitaani. Baadhi ya madaktari hawa walinishangaza kutangaza habari za mgonjwa,” anasema.

Anasema wakati muda unazidi kwenda alikuwa akitafakari endapo atapimwa na kukutwa na maambukizo ya COVID-19 itakuwaje, kwani ni mwalimu maarufu aliyefundisha shule kadhaa wilayani humo. Baada ya kuwaomba madaktari hao kumpima malaria kushindikana, anawaambia wafanye wanachotaka.

KUTENGWA

“Walinitenga kwenye chumba maalum, wakati wanaendelea na maandalizi mengine, hata hivyo sikupewa huduma yoyote tangu nilipofika saa 2 asubuhi. Nilikuja kuhudumiwa saa 10 alasiri kwa kupimwa malaria. Majibu yalionyesha kuwa sikuwa na malaria. Hata hivyo nilikuwa na njaa kwani sikula tangu asubuhi.”

Mwalimu huyo anasema tangu wakati huo alitengwa kwenye chumba chake akisubiri kupimwa corona.

“Siku iliyofuata nilichukuliwa kipimo cha corona. Baada ya siku kadhaa majibu yalikuja. Kabla hata sijapewa majibu hayo nikasikia fununu kutoka kwa rafiki zangu kuwa majibu yanaonekana nina maambukizo. Kweli daktari alikuja siku hiyo na kuniambia nimekutwa na virusi,” anasema Mwanansali.

Baada ya hapo anasema alihamishiwa kwenye kituo cha karantini kilichopo mji wa Nanyamba kilometa 10 kutoka Tandahimba na akaendelea kutumia dawa za miti kwa kunywa mara tatu kwa siku, lakini hakupewa dawa yoyote kutoka hospitalini.

“Nilikaa kwa siku 21 kwenye karantini na hali yangu iliendelea kuimarika. Madaktari walikuja kunitembelea na wakati mwingine ilikuwa mpaka niwaite. Muda mwingi nilikuwa nikifanya mazoezi,” anasema walimu huyo.

UNYANYAPAA

Mwalimu Mwanansali anasimulia alichoakutana nacho wakati wa kuumwa kilimuumiza, kukithiri kwa unyanyapaa tangu kwa wahudumu wa afya na jamii nzima. Pia anasema awali hakukuwa na maandalizi ya kutosha kuhudumia wagonjwa hadi alipobainika.

Akielezea zaidi anasema hakukuwa na maandalizi na aliyoyaona katika kipindi chote hicho, yalifanywa baada kushukiwa kuwa ana ugonjwa huo.

“Hakukuwa na maandalizi ya kutosha hadi mimi nabainika kuwa na maambukizo. Waliandaa chumba nikiwa pale, walikuwa wakifyeka eneo na maandalizi mengine, ndiyo maana nilichelewa kuhudumiwa tangu asubuhi nilipofika hadi jioni,” anasema mwalimu huyo.

“Nilichojifunza ni kwamba, nilipambana na unyanyapaa zaidi kuliko corona yenyewe. Unyanyapaa kutoka kwa wahudumu wa afya na jamii kwa jumla. Kwa mfano mke wa rafiki yangu aliposikia nimeambukizwa corona alimuuliza mumuwe kwa nini anakuwa na urafiki na mimi. Nilichojifunza ni kuishinda hofu ambayo ndiyo tatizo kubwa linalowasumbua wengi,” anaongeza.

Aidha, anashauri wahudumu wa afya wapewe mafunzo ya kutosha ili wapunguze unyanyapaa kwa wagonjwa.

“Wahudumu wa afya wanapaswa kupewa ushauri wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa corona na kuwatia moyo kuliko kuwanyanyapaa. Mimi ni mgonjwa wa kwanza hapa Tandahimba, lakini inavyoonekana hakutakuwa na mwingine kwa sababu watu wanaogopa unyanyapaa. mtu atakohoa atajitibu mwenyewe huko huko kuliko kwenda hospitali,” anaeeleza.

MAONI YA VIONGOZI

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tandahimba, Athumani Suleiman, anakanusha kuwapo kwa unyanyapaa katika hospitali ya hiyo akisema kilichotokea ni hali ya taharuki tu.

“Si kweli kwamba mgonjwa alinyanyapaliwa, kwa sababu alipokwenda pale alipokelewa kama mgonjwa wa kawaida. Kwa kuwa huu ugonjwa ni mpya kulikuwa hali ya taharuki na kumekuwa na hofu kiasi kwamba hata mtu akikohoa watu wanadhani ni corona,” anasema Suleiman.

Akizungumzia juhudi zilizochukuliwa na Halmashauri hiyo kupambana na ugonjwa huo, Sulaiman amesema wilaya hiyo ilifanya maandalizi mapema ikiwa pamoja na kuunda kamati ya kuratibu ugonjwa huo na vituo vilivyoandaliwa kwa ajili ya kupokelea wagonjwa.

“Tulianzisha kamati kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Afya na tunakutana kila Jumatano kutathmini hali ya maambukizo ilivyo. Kamati hiyo inahusisha madiwani, viongozi wa dini na wa kata,” anasema Suleiman.

Anaongeza kuwa halmashauri hiyo imetumia mapato yake ya ndani kununua vifaa vya kuwakinga na maambukizo wahudumu wa afya na wagonjwa wanaofika katika hospitali na vituo vya afya.

Columnist: www.tanzaniaweb.live