Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Unauza bunduki, kununua fimbo

Bunduki Pic Wachezaji wa Kikosi cha Taifa Stars

Sat, 10 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Tumetolewa CHAN, tujipange.Wikendi iliyopita Taifa Stars ilitolewa na Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa kufuzu kwa mashindano ya Afrika wanaocheza kwenye ligi za ndani ya nchi zao (CHAN) kwa jumla ya mabao 4-0.

Ambacho hakijaingia akilini mwangu ni mabadiliko ya kocha wa taifa pale alipoondolewa Kim Poulsen baada ya kupoteza pambano la kwanza Dar es Salaam kwa 0-1. Nisichoelewa ni kama kocha mpya aliajiriwa kwenda kubadili matokeo katika mechi ya Kampala au ilikuwa ni matukio pacha (coincidence).

Kama benchi jipya la ufundi lilikuwa maalumu kwa ajili ya mechi ya marudiano, basi hiyo ilikuwa ni upatu wa hali ya juu. Ni kuuza bunduki ili kununua fimbo.

Ameondolewa kocha aliyekaa na timu kwa muda mrefu. Na si hilo tu, pia amewalea na anawajua baadhi ya wachezaji wakiwa katika timu za vijana na badala yake anaajiriwa kocha ambaye hapa nchini ni mgeni na ana majukumu ya klabu na anapewa msaidizi ambaye karibuni hakuwa kwenye ufundishaji wa timu inayocheza ligi na pia kocha wa makipa ambaye miezi miwili iliyopita alikuwa anacheza kwenye ligi na bado hajastaafu kama mchezaji.

Chini ya juma moja anatakiwa kupindua matokeo na kweli anayapindua kwa kufungwa 3-0. Ukiachilia mbali masuala ya kiufundi, muda ulikuwa ni mfupi mno kwa benchi jipya la ufundi. Hapa mwajiriwa aliomba kazi au mwajiri alimfuata mwajiriwa?

‘Eni wei’, makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe na mwajiri ndiye ana siri ya anachokipata kwa kuajiri na kufukuza. Taifa Stars ilipoteza mchezo wa marejeano kabla hata haujachezwa. Ndiyo hivyo, Stars imetolewa tujipange kwa changamoto zinazofuata.

MWAKINYO AMEJITAHIDI, ILA DUNIA HAIJAFIKA MWISHO

Pambano la ngumi la kimataifa kati ya Bondia Mwingereza Liam Smith na Mtanzania Hassan Mwakinyo lililofanyika katika Ukumbi wa M&S kwenye Jiji la Liverpool, Uingereza lilifika mwisho katika raundi ya nne kwa Mtanzania kupoteza kwa Knock Out. Hata hivyo, kumekuwa na maneno - kwanza kutoka kwa bondia mwenyewe akieleza chanzo cha kupoteza na baadaye wafuatiliaji hapa nchini na hata nje kila mmoja akisema lake.

Namna pambano lilivyohitimishwa ghafla huku Mwakinyo akifanya vizuri, ilimshangaza siyo tu mpinzani wake bali pia mwamuzi Victor Roughlin.

Watanzania mara nyingi tunafanya juhudi kubwa kutafuta maelezo jambo linapokwenda kinyume kuliko hata juhudi iliyokuwepo kushughulikia jambo lenyewe. Uzuri wa miaka hii teknolojia imewezesha kila mtu kuona anavyoona na kutafsiri kwa kadri ya uelewa wake. Yote kwa yote kila kinachoendelea kinaweza kumfaidisha au kumtia hasara Mwakinyo.

Sina hakika na udhamini wake wa vifaa na hata promota wake, lakini ninachokijua kampuni zinahitaji wanamichezo walio na menejimenti sahihi siyo tu kiufundi, bali pia upande wa mahusiano (PR).

Ikiwa mchezaji ataingia kwenye mtego wa wachambuzi na wenye chuki naye anaweza kujikuta anapoteza nafasi kama mwanamichezo wa kulipwa (professional) na pia anaweza kushindwa kukaribisha udhamini ambao ungemsaidia kusonga mbele na kujipatia kipato.

Yaliyotokea yametokea, Mwakinyo aweke fikra zake kwenye pambano lijalo na kuchukua somo tu kutoka pambano la Liverpool. Yeye bado ni bondia mwenye mafanikio nchini. Pambano la Liverpool lilikuwa lazima liwe na matokeo hata angekuwa Muhammad Ali, Mike Tyson au Mayweather.

Huu sio wakati wa kusema koti hili au kanzu hii ilinipwaya. Maneno awaachie wanaolipwa kwa kuzungumza huku yeye akijifua zaidi.

HONGERA BODI YA LIGI, LAKINI WAAMUZI

Ligi Kuu Bara imeanza kama ilivyopangwa. Hakujasikika malalamiko mengi kuhusu maandalizi yaliyofanywa na na Bodi ya Ligi (TPLB) kuelekea msimu mpya wa 2022/23. Hata hivyo, mwanzo mzuri wa ligi unatiwa dosari na waamuzi. Msingi wa utendaji kazi mzuri wa mwamuzi ni kuzielewa na kuzitafsiri vyema sheria 17 kama zilivyoandaliwa na Bodi ya Soka (IFAB) na kutolewa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Pia, mwamuzi anatakiwa kuwa na utimamu wa mwili na akili. Hapo kwenye akili kunahitaji zaidi kujiamini (confidence). Mwamuzi anapotoa adhabu isiyo ya kweli au faida isiyostahili kwa kufanya kinachoitwa mtaani ‘kubalansi mchezo’ huo unakuwa udhaifu mkubwa unaotokana na kutojiamini (lack of confidence).

Kosa halifanyiwi fidia na kosa. Shime Bodi ya Ligi na vyombo vinavyohusika na waamuzi waketisheni chini waamuzi bila kuwawekea shinikizo na kuwaeleza kuwa wao ndio wanaweza kufanikisha msimu wa ligi au kuharibu kazi nzuri iliyopangwa.

AZAM IMEONA NJIA?

Tofauti na kaka zake wakubwa, binti yangu mdogo ni mpenzi wa timu ya Azam. Msimu uliopita aliniuliza “daddy mbona kila siku zinacheza Yanga na Simba, mbona Azam haichezi?” Alikuwa akimaanisha kwamba timu zinazoonekana zaidi na mechi zake kuangaliwa na wengi ni Yanga na Simba.

Ukweli nilikosa jibu. Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Azam FC uliofanyika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam ulishuhudia juzi, Jumanne Azam ikiwapa kipimo tosha Yanga kuhusu kutetea ubingwa na pia ushiriki wao kimataifa.

Azam imewekeza katika timu na klabu kwa ujumla, lakini imekuwa haifanyi vizuri hata dhidi ya timu zinazoishi kwa kuungaunga. Msimu huu Azam FC, chini ya Mkurugenzi Yusuf Bakhressa ambaye ni wakala wa zamani wa wachezaji anayetambuliwa na Fifa, imefanya usajili wa wachezaji wenye wasifu na uwezo mkubwa kama walivyoonekana kwenye pambano la Jumanne.

Kama haitoshi Azam ilikuwa naye jukwaani kocha mwenye kuujua mpira wa Afrika bila shaka wakijua majukumu ya CAF yaliyoko mbele yao. Azam FC imeona njia? Bado ni mapema. Lakini kama ikicheza hivi mpaka mwisho wa msimu na ikaendelea kufanya vizuri kila msimu basi itajikuta imepata wafuasi hasa wa kizazi kipya.

Timu hutengeneza mashabiki kwa kucheza vizuri na kushinda mara nyingi na kuchukua mataji mengi. Mashabiki ni mtaji namba moja kwa klabu ya michezo.

LINI ZANZIBAR ITACHEZA MPIRA WA FIFA?

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ameongea kuhusu Zanzibar kufaidika na misaada ya maendeleo kutoka FIFA.

Chama cha Mpira Zanzibar kinaweza kuwa miongoni mwa wanachama ambao uanachama wao katika Shirikisho la Mpira Afrika ulidumu kwa muda mfupi.

Zanzibar ilipata uanachama wa CAF Machi 2017 na kunyan’ganywa Julai, mwaka huo. Uanachama wa CAF ilikuwa ni kigezo cha kuomba uanachama wa FIFA na Zanzibar ilikuwa imeshaandika tayari barua.

Nasema ilinyang’anywa kwa sababu ilipata uanachama kupitia kikao cha juu kabisa cha CAF - yaani mkutano mkuu na kunyang’anywa katika kikao cha kamati ya utendaji. Mabailiko katika ibara ya 4 ya katiba ya CAF ya Machi 2021 yameweka ugumu kwa Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa CAF au FIFA.

Hayo yametokea lakini Zanzibar bado inacheza mpira na inatoa vipaji vya hali ya juu ingawa kiukweli ni kama hautambuliwi na FIFA kwa sababu FIFA haifanyi kazi ya moja kwa moja inayohusu maendeleo ya mpira Zanzibar. FIFA na CAF zinaitambua Tanzania kama nchi.

Ni kweli kwamba Zanzibar imewahi kufaidika na misaada ya FIFA kama vile ujenzi wa nyasi bandia katika Uwanja wa Gombani, mafunzo ya makocha na waamuzi lakini vyote hivi vimepatikana kupitia mgongo wa TFF ambayo mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa usajili wake yanaishia Tanzania Bara.

Ili kuhakikisha maendeleo ya mpira yanakuwa sawia nchi nzima, ni muhimu kwa TFF na ZFF kutafuta maeneo ya ushirikiano na ikiwezekana kufanya kazi kimuungano kama inavyofanya kazi Kamati ya Olimpiki (TOC). Michezo Zanzibar ikikua itakuwa na tija kwa maendeleo ya michezo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Columnist: Mwanaspoti