Kwa kutazama maendeleo ya klabu zetu uwanjani, Mohamed Dewji maarufu kama MO, anapaswa kuwa Role Model wa matajiri wote wanaowekeza kwenye mpira wetu. Simba bado haijapata mafanikio makubwa kwenye michuano ya CAF lakini kuna hatua wanapiga kila siku. Simba bado hawajatwaa ubingwa wa Afrika lakini kuna mahali wameshasogea. Bado Simba haina uwezo wa kusajili wachezaji wakubwa kama Al Ahly na Mamelod Sundowns, lakini kuna mahali wamesogea.
Watu kama kina Clatous Chota Chama isingekuwa rahisi kuwapata. MO pia ni rafiki mkubwa wa vyombo vya habari. Hana tatizo kabisa kama ilivyo kwa matajiri wengine nchini. Ametembelea vyombo vyetu vya habari karibu vyote. Ni mara chache sana unampata tajiri wa aina hii.
Simba chini ya MO Dewji kama mwekezaji, inapaswa kuwa mfano mzuri kwa klabu zetu nyingine. Tunatamani kumsikia GSM mwenyewe. MO ni rafiki mkubwa wa media zetu. Kama hatuwezi kumsifia, basi tumheshimu.
Ni matajiri wachache sana wanakubali kuhojiwa. Wengi tungetamani kufanya mahojiano na Rostam Aziz lakini, huwezi kumpata kirahisi. Hawezi kukubali kwa sababu chochote anachotamka kina ‘impact’ kubwa sana kwa jamii, Serikali na hata biashara zake binafsi. Wengi tungependa kumhoji Mzee Saidi Salim Bakhresa lakini, hawezi kukupa fursa hiyo. Mtu kama MO ambaye amekuwa rafiki wa media tunambeza kweli? This is very unfair!
Kwa wapenzi wa Simba SC ndiyo usiseme kabisa. Pengine MO ndiyo tajiri anayeongoza kwa kwenda uwanjani na kuvaa Jezi. Pengine MO ndiyo tajiri nchini anayejiachia mbele ya timu yake kuliko mwingine yeyote. MO hastahili kubezwa.
Mchezo wa soka kwa sehemu kubwa unaonekana ndiyo starehe ya watu wa tabaka la chini. Ukiona mtu kama MO anajishusha hadi chini, usimbeze. Ameamua tu kuwa mnyenyekevu. Ukiona MO anakubali kufanya interview, ni jambo la kufurahia na hasa kwa sisi watu wa media.
Wengi tungetamani kusikia Mzee Bakhresa anasema nini juu ya Azam FC na soka la Tanzania. Wengi tungetamani kusikia GSM anasema nini juu ya Yanga ijayo na soka la Tanzania lakini, tunaishia kuwasikia wasaidizi wao tu. MO amekuwa rafiki mkubwa sana wa media kwa matajiri wa zama hizi za soka letu lakini ndiyo kwanza tunaishia kumtukana tu mtandaoni! Tunamwona anatafuta KIKI! Tunamwona anataka Trending! Tunamwona anataka sifa!
MO kama mwanadamu, atakuwa na mapungufu yake kama ilivyo kwako wewe na kwangu mimi, lakini kuhusu media, huyu mtu anatupa heshima kubwa sana. Kutozungumza na media kwa matajiri wengine wa mpira wetu, sio sifa. Sio jambo la kuonekana mashujaa. Ni kutunyima habari. Ni kutunyima maarifa.
Matajiri ambao hawazungumzi na media hawapaswi kusifiwa kama wengi wanavyodhani. Tunahitaji watu kama MO kwenye mpira wetu. Tunatamani kumsikia Mzee Bakhresa mwenyewe. Tunatamani kumsikia GSM mwenyewe. MO ni rafiki mkubwa wa media zetu. Kama hatuwezi kumsifia, basi tumuheshimu.