Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Unalijua jina lingine la Augustine Okrah?

Okraaaaah Augustine Unalijua jina lingine la Augustine Okrah?

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Augustine Okrah. Okrah Magic. Okrah fundi. Okrah spidi. Hivi ndivyo wachezaji wakubwa wanavyoishi kwenye soka la Tanzania. Hata kama una siku mbili, unaweza kuwa na majina ya kukutukuza hata 10. Hivi ndivyo mashabiki wa soka Tanzania wanavyowaenzi wachezaji wanaowapenda.

Ukiona mchezaji yuko Tanzania na anaitwa kwa jina aliloitwa na wazazi wake, mtazame vizuri labda ni Mwanariadha. Mtazame vizuri labda ni Mwanamitindo. Mpira wa Tanzania ni kama muziki wa Hip Hop, majigambo yametawala.

Okrah ni mmoja wa wachezaji waliokamilika zaidi pale kwenye kikosi cha Simba. Ana uwezo wa kukupa mabao, ana uwezo wa kukupa spidi, ni fundi hasa wa boli. Mara chache sana tunapata wa wachezaji aina ya Okrah kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika.

Mara nyingi wachezaji wa kutoka Ghana, Nigeria, Cameroon wanaokuja nchini huwa tayari ni wavunja kuni, tayari mwendo wameumaliza. Watu waliomaliza muda wao uwanjani na wanakuja kwetu kupumzika.

Hata Okrah amekuja kwa kuchelewa lakini bado boli analijua. Amekuja kwa kuchelewa lakini ufundi bado umetawala kichwa na miguu yake. Kama kuna jina jipya ambalo mashabiki wa Simba wanapaswa kumpa Mghana wao, ni Okrah mchoyo. Okrah mbinafsi. Hakuna namna haya yanapaswa kuwa sehemu ya majina yake. Nimetazama Kariakoo Dabi wikiendi iliyopita na Okrah alikuwa mmoja wa watu waliokuwa na siku nzuri sana ofisini. Ndiye mfungaji wa bao pekee la Simba. Ndiye mchezaji ambaye kimsingi alipaswa kuwamaliza Yanga mapema tu. Mchezo wa soka ni mchezo wa nafasi na muda.

Lazima uwe na wachezaji wenye uwezo mkubwa sana wa kucheza na nafasi na muda. Wakati unatakiwa kutoa pasi, ukikokota unaharibu. Wakati unatakiwa kupiga langoni, ukimpiga mtu tobo unaharibu. Ndiyo mchezo wa soka unavyotaka. Kila kitu lazima kifanyike kwa wakati wake. Kama Okrah angepunguza uchoyo, huenda Yanga angefungwa kwa Mkapa.

Kama Okrah angepunguza ubinafsi, angetengeneza nafasi nyingi sana za kufunga juzi kwa Mkapa. Wachezaji nao ni binadamu kuna muda sio kila kitu watakifanya kwa usahihi.

Simba kwenye idara yao ya ushambuliaji, waliwategemea watu wanne. Pape Ousmane Sakho, Moses Phiri na Okrah na mwamba wa Lusaka. Hawa ndio Simba wa Juma Mgunda. Kwa bahati mbaya, bado Sakho anajitafuta. Kwa bahati mbaya, Moses Phiri anategemea zaidi utengenezewa nafasi.

Chama na Okrah ndiyo wapishi wakuu wa nafasi kwa Simba. Ndiyo maana bao la Simba, lilipikwa kwenye miguu mitakatifu ya Chama. Fundi wa boli. Okrah akipunguza mambo mengi uwanjani, Simba watanufaika sana na uwepo wake uwanjani kwa sababu sio tu ubunifu, Okrah ana kasi pia kuliko hata Chama.

Hakukuwa na sababu yoyote ya Okrah kuvua jezi baada ya kufunga bao la mapema. Unapata kadi ya njano ya mapema bila sababu yoyote ya msingi. Okrah anapaswa kuacha kujifikiria yeye tu. Anapaswa kuifikiria zaidi timu kuliko yeye binafsi. Kama angepunguza uchoyo, huenda Yanga angefia kwa Mkapa.

Ni msimu wa tatu sasa unakwenda Simba wanapata tabu kwenye ligi kumfunga Yanga. Ushindi pekee Simba wameupata ni kwenye mechi za FA tu. Walimfunga Yanga 1-0 pale Kigoma na kutwaa ubingwa. Walimfunga Yanga 4ñ1 pale kwa Mkapa na kumwachia maumivu makali, zote ni mechi za FA.

Mechi za ligi mara ya mwisho Simba kushinda, Ramadani Kabwili bado alikuwa kipa wa Yanga. Simba hivi karibuni wametamba sana nyumbani dhidi ya Al Ahly, Kaizer Chiefs lakini hawajafurukuta dhidi ya Yanga. Katika mechi sita za ligi, Simba haijashinda hata mechi moja. Kuna mahali kitu hakipo sawa. Ushindi wa Simba kwa Yanga siku hizi ni sare. Hakuna jipya zaidi ya hilo. Kocha Mgunda anapaswa kumbadilisha kidogo Okrah, anapaswa kumwandaa kidogo kiakili. Akiacha ubinafsi atakuwa msaada mkubwa sana kwa Simba, akiacha ubinafsi, Phiri atafunga sana msimu huu.

Ni mara chache sana tunapata wachezaji wazuri kutoka Ghana. Ni mara chache sana tunapata wachezaji wazuri kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika.

Wachezaji wa ukanda huu, wanawaza zaidi Ulaya kuliko kucheza Afrika, nyumbani huwa wanarejea wanapokaribia kustaafu, nyumbani huwa wanarejea baada ya kuumaliza mwendo.

Timu inaonekana inabadilika kila kukicha chini ya Mgunda. Uzoefu wa wachezaji wakubwa unaonekana, boli linatembea chini ya Mgunda, kama kocha anamfanya Okrah kuacha uchoyo, Simba watasogea. Kama Okrah atakubali kuwa mpishi wa Phiri, kuna mabao mengi sana yanakuja. Bado namwona Chama akirejea kwenye ubora, pasi rula zimeendelea kutolewa, bado ameendelea kuwa kiungo mbunifu na mtulivu zaidi nchini.

Wakitengeneza muunganiko mzuri na Okrah, Simba itakuwa salama sana chini ya Mgunda. Ubinafsi ukitawala, mabao ya Phiri yatakauta, bado naendelea kuamini Okrah mchoyo angebadilika na kuwa Okrah Magic, bila shaka yoyote matokeo yangekuwa tofauti.

Mechi kubwa wakati mwingine huamuliwa na wachezaji wakubwa, Okrah ni mchezaji mkubwa, hakuja Simba kwa bahati mbaya, ni mechi ya kwanza ya Dabi kwa Mgunda bila yoyote haya sio matokeo mabaya.

Anapaswa kumrejesha Sakho kwenye kiwango chake bora, anapaswa kumsaidia pia Okrah kuacha uchoyo ili kuifanya Simba kuwa imara zaidi Kimataifa na kwenye kusaka taji la Ligi kuu. Unalijua jina lingine la Okrah? Usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Nani unadhani alistahili kuwa mchezaji bora wa Dabi?

Columnist: Mwanaspoti