Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Una malalamiko? Yatume Haki za Binadamu kupitia mtandao

Fdf89e841bb177ead003c88495f588cb Una malalamiko? Yatume Haki za Binadamu kupitia mtandao

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UNA malalamiko yoyote yanayohusiana na utekelezaji au utendaji wa watu wanaoshikilia ofisi katika utumishi wa Serikali, mamlaka za umma au vyombo vya umma, ikijumuisha taasisi binafsi na watu binafsi ambapo malalamiko hayo yanahusu matumizi mabaya ya madaraka?

Je, una malalamiko kuhusu huduma za upendeleo kwa mtu yeyote, ikiwa ni mlalamikaji au mtu mwingine katika kutekeleza kazi zao za kiserikali au umma?

Je, una malalamiko kuhusu masuala ya ardhi, kunyanyaswa kazini, kudhulumiwa haki zako mbalimbali kama mtoto, mzee, mwanamke na zinginezo?

Kama ndivyo, hii ni habari njema kwako kwamba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeanzisha utaratibu wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa njia ya mtandao na simu.

Kwamba, sasa unaweza kupeleka malalamiko yako kwenye Tume hii kupitia simu ya kawaida, simumtelezo (simu janja) au mtandao wa kompyuta na kufanyiwa kazi na hivyo kupunguza gharama na muda ambao ungetumika kwa kulazimika kwenda ofisini.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu anasema, Tume hiyo imeamua kuimarisha ufanisi wa utoaji huduma kwa kuboresha mfumo wa upokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa kumwezesha mlalamikaji kuwasilisha na kufuatilia malalamiko yake kupitia mtandao.

“Hivi sasa mwananchi anaweza kuwasilisha, kufuatilia malalamiko, kutoa taarifa za matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa msingi ya utawala bora kupitia tovuti, simu ya kiganjani au simu janja,” anasema.

Ili kuboresha mfumo wa upokeaji wa malalamiko ya wananchi kwa kutumia mitandao, Tume kupitia mradi wa miaka mitatu iliangalia uhusiano wa biashara na haki za binadamu.

Mradi huo una lengo la kuimarisha ufuatiliaji, utafiti na kuibua midahalo juu ya biashara na haki za binadamu na kuongeza uwezo wa kitaifa kutoa ulinzi wa makundi maalumu yaliyopo hatarini kupata madhara ya haki kutokana na shughuli za kibiashara nchini Tanzania.

Tume imefanya mikutano katika mikoa minane Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ya kuhamasisha wananchi na wawekezaji katika viwanda kwa kutumia njia ya mtandao kuwasilisha malalamiko yao. Njia hii imepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi.

Jaji Mwaimu anasema, njia hizo za kutumia mtandao katika kuwasilisha malalamiko ni nyepesi na hazina gharama kwa mlalamikaji kwa sababu halazimiki kufika katika ofisi za Tume au kufuatilia mrejesho kuhusu malalamiko yake.

“Pia mlalamikaji anaweza kuwasilisha au kufuatilia malalamiko yake kwa muda wowote na mahali popote alipo,” anasema.

Mwananchi anayo fursa ya kuwasilisha au kufuatilia malalamiko yake kupitia tovuti ya Tume ambayo ni www.chrgg.go.tz na kushusha ukurasa hadi kufika katikati, upande wa kushoto ambapo ataona jedwali lenye safu tatu.

Katika jedwali hilo, ataona safu ya kuwasilisha malalamiko, kufuatilia na takwimu za malalamiko. Hivyo, mwananchi atachagua safu ya kuwasilisha malalamiko ambayo ina vipengele 12 ikiwemo kichwa cha malalamiko yake, muhtasari wa malalamiko, jina kamili, jinsi, anuani ya barua pepe, namba ya simu, namba ya kitambulisho cha NIDA (kama ipo), mkoa anaotoka, wilaya, kata na anuani ya posta na hatimaye atabonyeza kitufe cha wasilisha.

Jaji Mwaimu anasema, mwananchi anaweza kuambatanisha vielelezo vinavyohusiana na malalamiko kwa kuchagua faili na kuweka kiambatanisho hicho. Kupitia anuani ya barua pepe aliyoandika, atapata ujumbe unaomfahamisha namba aliyopewa na Tume baada ya kupokea malalamiko yake.

Mwananchi atatumia namba hiyo kufuatilia malalamiko yake. Hivyo, ni muhimu kutunza namba hiyo ili kuepuka usumbufu wakati wa kufuatilia malalamo yake.

Jinsi ya kufuatilia malalamiko kupitia tovuti, mwananchi anatakiwa kuchagua safu ya fuatilia malalamiko kwa kuingiza namba ya malalamiko aliyotumiwa, kisha anachagua alama ya kutafuta. Hatimaye atapata mrejesho kuhusu malalamiko yake kupitia anuani yake ya barua pepe.

Kuhusu kuwasilisha malalamiko kupitia simu ya kiganjani, mwananchi anatakiwa kupiga namba *152*00#; kisha atachagua namba 9 inayohusu sheria na haki, kisha anachagua namba 1 inayohusu haki za binadamu, kisha anachagua namba moja kuwasilisha malalamiko na atafuata maelekezo.

Jinsi ya kufuatilia malalamiko kwa kutumia simu ya kiganjani, anapiga kama alivyopiga wakati akichagua kutuma malalamiko, kisha anachagua namba 2 kufuatilia malalamiko halafu anafuata maelekezo. Akitaka kusitisha muamala anachagua sitisha (cancel).

Mwananchi pia anaweza kutumia njia ya tatu ya kuwasilisha ua kufuatilia malalamiko kwa kupitia simu janja (mobile app) ambapo anatakiwa kuwa na simu janja (smart phone). Katika simu yake, anaingia kwenye play store au App Store. Anatafuta Haki App, kisha anaipakua maadamu programu hiyo (app) itakuwa na nembo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

“Baada ya kupata Haki App kwenye simu yako, unafuata maelekezo ya kuwasilisha malalamiko. Unajaza taarifa sahihi, hasa anuani ya barua pepe ili uweze kutumiwa namba ya kufuatilia malalamiko yako,” anasema.

Mwaimu anasema, mwananchi atafuatilia malalamiko yake kupitia Haki App kwenye simu yake, yakiwemo ya uvunjwaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na mwenendo wa mtu yeyote au taasisi yoyote katika kutekeleza madaraka au utekelezaji unaokiuka madaraka.

“Matumizi au matendo ya watu wenye madaraka katika utumishi wa serikali kuu, serikali za mitaa yaani halmashauri za wilaya, miji, manispaa, vijiji na kata, mashirika au kampuni za umma, vyombo binafsi na watu binafsi kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, kutotenda haki na kuonea,” anasema.

Tume haishughulikii malalamiko yaliyoletwa na mtu mmoja, kikundi cha watu au taasisi ambayo yamecheleweshwa kwa zaidi ya miaka miwili, hata hivyo inaweza kufuatilia au kuchunguza malalamiko hayo kama itaona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

“Tume haifutilii kama mlalamikaji anayo nafasi ya kuelekeza au kupeleka katika vyombo vingine vyenye mamlaka kisheria na kama malalamiko yanatolewa kwa nia mbaya, bila sababu ya msingi na kwa njia ya kukomoa au malalamiko yapo nje ya mamlaka ya Tume,” anasema.

“Kama malalamiko yametumwa katika mamlaka nyingine na kunakiliwa Tume. Hata hivyo Tume inaweza kuendelea kufuatilia au kuchunguza malalamiko hayo iwapo itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo,” anasema.

Pia Tume imeweka utaratibu wa kutochunguza malalamiko ambayo yanashughulikiwa au yameshughulikiwa na mahakama au chombo kingine chenye asili ya kimahakama kama vile Baraza la Usuluhishi na makazi.

Pia haitachunguza malalamiko yanayohusu uhusiano au ushirikiano kati ya Serikali na Serikali ya nchi yoyote ya nje au shirika la kimtaifa au malalamiko yanayohusu madaraka ya Rais ya kutoa msamaha wa wafungwa au watu wengine wowote.

Pia Tume haitachunguza malalamiko ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Rais wa Zanzibar ameagiza vinginevyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Katiba ya Zanzibar pamoja na malalamiko ya madai yanayotokana na mikataba binafsi, madai ya kawaida kama ya kuvunja ndoa au mirathi.

Pamoja na njia mbalimbali za kutumia tovuti, simu za viganjani na simumtlezo (janja) mwananchi pia anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa kuandika barua kwa kuweka ndani yake jina, anuani, namba ya simu na anuani ya barua pepe na anuani ya mlalamikiwa kwa mwenyekiti wa Tume Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam, Mwanza na Wete-Pemba ili Tume iweze kuendeleza mawasiliano na mlalamikaji au mlalamikiwa.

Lakini pia mwananchi anayelalamika anaweza kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Tume zilizopo katika mikoa ya Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam, Lindi, Mwanza na Wete-Pemba.

Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Tume, Manyiri Isack anasema, tangu uhamasishaji ufanyike kwa wananchi kwa kutumia mitandao kuwasilisha malalamiko yao kuanza Januari 8 mwaka hadi hadi

Isack anasema mwitikio wa wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa Tume ni mkubwa hususani kwa kutumia simu ya kiganjani baada ya uhamasihaji kufanyika katika mikoa minane nchini..

Naye Mratibu wa Uboreshaji, Ufuatiliaji, Utafiti na mazungumzo kuhusu Biashara na Haki za Binadamu, Jovina Muchunguzi anasema katika mradi huo wa miaka mitatu uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) wamepata mwitikio mkubwa wa wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa tume kupitia mtandao.

Columnist: www.habarileo.co.tz