Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Umuhimu wa Fair Play na ushabiki ubora kwenye soka

IMG 4294 Saido.jpeg Saido Ntibazonkiza

Sat, 24 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika tuzo za TFF kwa msimu wa 2022-2023, kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza, alishinda tuzo ya Fair Play akiwapikunyota wenzake wa Msimbazi, Pape Osmane Sakho na Jean Baleke.

Saido alishinda tuzo kutokana na kitendo cha kumzuia ugomvi wa Baleke na Fiston Mayele kwenye pambano la Simba na Yanga ambalo liliisha kwam Yanga kulala mabao 2-0.

Pia kwa wanaokumbuka Januari mwaka jana kwenye tuzo maarufu za Ufaransa za Ballon d’Or na ile ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) zilizotolewa Zurich, kuna tuzo maalum ilitolewa ya Fair Play.

Tuzo hiyo ya FIFA ya Fair Play 2021, ilienda kwa timu ya taifa ya Denmark na madaktari wake kutokana na jitihada za kuokoa maisha ya Christian Eriksen alipoanguka ghafla na kuzimia wakati wa Fainali za Euro 2020.

Ni kweli neno Fair Play ndilo ambalo limezoeleka katika vinywa vya watu wengi hapa nchini ikiwamo wanahabari, ila kwa lugha rahisi ya kiswahili tafsiri ya neno hili ni Uungwana wa kimchezo.

Mashabiki wa Denmark nao waliibuka washindi wa tuzo ya 'Mashabiki Bora' kwa mwaka 2021 kutokana na kitendo cha kiungwana na kuunga mkono walioonyesha wakati kiungo huyo akipewa huduma.

Vitendo hivi viwili vilikuwa na mchango mkubwa katika uokozi wa maisha ya Kiungo wa Denmark Eriksen ambaye alikuwa katika hali ya hatari uwanjani. Uponywaji wake umesaidia nyota huyo kuendelea na soka na msimu huu kila mtu ameshuhudia alivyoupigwa mwingi ndani ya Manchester United iliyobeba Kombe la Ligi (Carabao Cup) na kumaliza nafasi ya tatu ya Ligi Kuu ya England.

Ushabiki bora wa kuunga mkono mchezaji huyo kuletewa huduma haraka na madaktari wa timu ambao walikuwa na wepesi wa hali ya juu waliingia na kumpa huduma za awali za dharula.

Soka ni mchezo mkubwa duniani ambao unaingiza mamilioni ya fedha huku ikibeba hisia kali za mashabiki ambao siku zote hutaka timu zao zishinde na kubeba ubingwa.

Pamoja na hayo yote linapokuja suala la uhai wa mtu au afya ya mtu hapo ndipo uungwana na ushabiki bora unahitajika, vinginevyo mchezo huu ungekosa utu kwa majeruhi au wanaopata matatizo ya kiafya.

Mchezaji muungwana humjali mpinzani wake na mwezake pale anapopata tatizo la ajali la kimchezo au apomfanyia faulu. Kufanya hivyo ndiyo kunaleta faraja na kumweka katika hisia nzuri mjeruhiwa.

Ushabiki bora ni pale mshabiki anapotambua kuwa pamoja na uwepo wa upinzani mkali wa mchezo lakini bado anawajibu wa kujali na kutoa msaada pale inapotokea mchezaji au yoyote yule anapoumia au kuumwa au kuwa na tishio la uhai.

UMUHIMU WAKE

Fair Play ni kitu kipana katika michezo ambacho kimebeba uthamani wa mambo mengi ambayo si tu kwa michezo bali hata mambo ya kimaisha ya kila siku.

Ushindani wenye uungwana katika michezo unabeba heshima, utu, urafiki, umoja, hamasa ya timu, heshima kwa kanuni na sheria za michezo zilizoandikwa na zile zisizoandikwa kama vile uaminifu, mshikamano, uvumilivu, kujali, ubora na furaha.

Hivyo hapa tunapata picha kuwa mambo mengi haya ndiyo yanajenga msingi mkuu wa fair play katika michezo hatimaye michezo inakuwa si uadui bali ni burudani.

Tafiti kadhaa zimawahi ktafiti na kuja na majibu kuwa uungwana wa kimchezo au maarufu zaidi kama Fair Play ni moja ya nyenzo muhimu ya kupunguza majeraha yasiyo ya lazima michezoni.

Moja ya tafiti hizo ni ile iliyofanyika 2018 ni ile iliyofanywa na taasisi ya Sport Medicine Psychology Laboratory ya nchi Marekani ambayo ilijikita kutafiti fair play na upunguzaji kasi ya majeraha ya kimichezo kwa wanamichezo vijana kwa kuhamasisha tabia za kiungwana.

Nyenzo ya Fair Play ndiyo inamfanya mchezaji wa upinzani kuutoa mpira nje au kusimamisha mpira ili mpinzani au mwenzake apate huduma ya kwanza.

Mfano mzuri wa uungwana mchezoni umewahi kuonyeshwa katika soka kwa vitendo Desemba 2000 na mchezaji wa West Ham, Paolo Di Canio dhidi ya Everton katika mchezo wa Ligi Kuu (EPL).

Katika mchezo huo kipa wa Everton, Paul Gerrard alipiga mbizi ili kupokonya mpira lakini aliumia wakati alipokuwa akifanya hivyo hatimaye mchezaji wa West Ham Utd, aliunasa na kutoa pasi.

Di Canio ambaye alikuwa katika nafasi nzuri alipokea pasi hiyo akiwa yeye na lango likiwa wazi kwani kipa alikuwa hayuko eneo hilo akigaragara kwa maumivu ya jeraha.

Wengi walitarajia kuwa angelifunga lakini hakufanya hivyo, badala yake aliutoa mpira nje ili kutoa nafasi watoa huduma ya kwanza waje uwanjani ili kumpa kipa huyo huduma.

Tukio hili lilikuwa ni moja ya matukio ya juu ya kiungwana katika soka, tukio hili liliishilia kwa Di Canio kupata tuzo ya FIFA Fair Play Award mwaka uliofuata 2001.

Vile vile hata inapotokea mchezaji hakuweza kurudi uwanjani basi huweza kupata faraja kutokana na vitendo vya kiungwana ambavyo huonyeshwa na mpinzani wake na wachezaji wenzake.

Ukiacha uungwana, ushabiki bora nao una mchango wake kwani kitendo cha mashabiki kuonyesha kumjali na kumuunga mkono mchezaji aliyejeruhiwa humpa faraja na kumpa tiba ya kiakili.

Endapo ingelikuwa mashabiki wanamzomea na kumpa maneno makali mchezaji majeruhi ina maana ingeliweza kuwapa mpasuko wa kihisia hatimaye mtikisiko wa kiakili ikiwamo kupata msongo wa mawazo.

Mchezaji majeruhi anapokuwa amejeruhiwa na huku anapata matatizo ya kiakili kama msongo wa mawazo ina maana kuwa anakuwa amebeba jeraha la kimwili na kiakili.

Vitu hivi vikiwepo mwilini tayari inakuwa mwili hauna afya njema na matokeo yake anaweza kuchangia mwili kuwa dhaifu na kutokupona kwa wakati.

Tukio la kuzimia kwa Erikson na kupewa faraja na uungwaji mkono na mashabiki wakati anapatiwa huduma ni ishara kuwa hata mashabiki wenye hisia kali wanatambua kuwa uhai wa mtu ni zaidi ya vyote.

Tumeshudia mashabiki mbalimbali duniani wakitumia muda mwingi katika kuta za mitandao ya kijamii kuwapa maneno ya faraja wachezaji waliopata majeraha mabaya na kutolewa uwanjani.

Mfano mzuri ni siku za karibu mchezaji wa zamani wa klabu ya Manchester City aliyetua klabu ya Barcelona msimu huu ambaye amelazimika kuachana na soka kutokana na hali ya afya ya moyo.

Mamia ya wachezaji, mashabiki, makocha na wadau wa soka waliungana pamoja kumpa faraja mchezaji huyu kwa kumuandikia maneno mazuri ya kumfariji katika kuta za mtandao wake wa kijamii.

Na vitendo hivi vinafanywa si tu kwa mashabiki wa mchezaji huyo bali pia na wale ambao ni wapinzani wao, hii inaonyesha mshikamano wa kiungwana wa mashabiki kwa wachezaji wanaopata majeraha.

Uungwana wa kimichezo yaani fair Play na ushabiki bora vitabaki kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya michezo kuliko timu kushinda au kuchukua ubingwa.

Columnist: Mwanaspoti