Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Umeyaona matokeo ya timu zetu Afrika?

Simba Vs Horoya Guinea Mtego Umeyaona matokeo ya timu zetu Afrika?

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita tulikuwa na taarifa ya ligi yetu kushika nafasi ya tano Afrika. Ukichukua kigezo cha mafanikio kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika bado Tanzania hatustahili hata kuwemo ndani ya 10 bora. Ukichukua kigezo cha michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, bado sisi si lolote, si chochote.

Kifupi bado tuko nyuma sana kwenye mpira wa bara letu. Umeyaona matokeo ya timu zetu Afrika? Kila mtu anaona aibu. Simba wanaona aibu. Yanga wanaona aibu. Tunaweza kuwa na mashabiki wengi. Tunaweza kuwa imara kwenye mitandao ya kijamii, lakini bado hatuko sawa kwenye mapambano ya uwanjani.

Timu zetu bado zinafungwa mabao yakeyale. Timu zetu bado kushinda ugenini ni kama twiga kuzaa farasi. Ni kweli Simba imewahi kushinda ugenini Nigeria, DR Congo na Sudan, lakini hakuna mwendelezo. Imebaki kuwa historia. Ni kweli Yanga imewahi kushinda ugenini Tunisia lakini hakuna mwendelezo.

Ni kama ushindi wa timu ugenini kubahatisha zaidi. Umeyaona matokeo ya timu zetu ugenini? Ni huzuni tupu kwa kweli. Wanachowaza ni maisha yao binafsi tu. Timu zetu zote mbili zimefungwa kirahisi sana wikiendi iliyopita.

Ukitazama aina ya mabao timu zetu zinayofungwa yote ni yaleyale. Simba ikifungwa bao la kichwa, Yanga itafungwa mpira wa kutenga. Ni mabao yaleyale. Yanga ikifungwa kwa faulo, Simba itafungwa kwa kona. Mabao ni ya aina moja kila siku. Ni kweli tunafungwa mabao ya aina moja kwa sababu mabeki wetu ni wafupi? Jibu ni hapana.

Dunia imewahi kuwa na wachezaji wafupi, lakini walikuwa bora sana kwenye mipira ya vichwa. Unamkumbuka Fabio Cannavaro wa Italia? Alikuwa mfupi lakini fundi sana kwenye mipira ya juu. Ulibahatika kumuona Diego Maradona? Alikuwa mtu mfupi lakini fundi sana wa mipra ya juu.

Alikuwa anaupiga mwingi sana enzi zake. Urefu au ufupi sio sababu ya moja kwa moja inayomfanya mtu kuwa mahiri kucheza mipira ya juu. Ni kweli kimo kirefu kinaweza kuwa na faida kubwa, lakini sio mara zote. Wapo watu wengi warefu, lakini hawana msaada kabisa kwenye mipira ya juu. Kuwa fundi wa mipira hiyo sio lazima uwe mrefu.

Unaziona timu zetu zikipata alama zote tisa za hatua ya makundi zikiwa uwanja wa nyumbani? Kiukweli sina uhakika. Simba imepoteza mechi kule Guinea kirahisi sana. Sio aina ya mechi ambayo Mnyama alistahili kupoteza. Ukitazama mechi ya Yanga kule Tunisia baada ya dakika 20 za kwanza ungesema leo mtu anakwenda kupigwa bao tano, kakini haikuwa hivyo.

Monastir sio timu kali sana. Ni watu wanaoshika nafasi ya nne kwa ubora nchini Tunisia. Mechi kama hizi kwenye michuano mikubwa kama hii Simba na Yanga walipaswa kurudi na alama mkononi nyumbani. Kama sio ushindi, basi walau hata sare.

Umeyaona matokeo ya timu zetu Afrika? Ni huzuni tupu. Tulipaswa kupata alama ugenini. Yanga imefungwa kirahisi sana pale Tunisia. Simba imepoteza nafasi nyingi sana pale Guinea.

Kama mechi hizi zingekuta timu zetu zipo kwenye viwango bora. Kuna alama za ugenini zingekuja nyumbani. Yanga ina deni kubwa sana kwa mashabiki. Haina historia ya kufanya makubwa kwenye michuano yotote Afrika, lakini nadhani wakati wa kuweka historia mpya ni sasa.

Hiki ndicho kipindi cha kuandikisha rekodi mpya. Simba walau wamekuwa na historia nzuri kidogo licha ya kushindwa kutwaa kombe lolote. Tuna kazi kubwa sana kama taifa kwa timu zetu kushinda mechi zote za Benjamin Mkapa.

Timu zetu zimefungwa kirahisi sana ugenini. Zinaonyesha dalili pia kuwa zinaweza kufungwa kwa mtindo uleule nyumbani.

Kwa usajili walioufanya Yanga wanalo deni kubwa kwa mashabiki wao, lakini kuleta historia mpya klabuni. Unapokuwa na wachezaji kama Yannick Bangala, Aziz KI, Bernard Morrison na Fiston Mayele, watu wanatazamia makubwa kutoka kwako.

Yanga wana timu iliyojengeka kwa misimu mitatu sasa. Ilipaswa kuleta utofauti kimataifa. Simba haina timu bora sana kama misimu minne ya nyuma, lakini unapopangwa na timu kama Horoya unapaswa kuona kandanda safi la Mnyama.

Tunapaswa kuona kina John Bocco wanafunga mabao. Simba imepoteza nafasi nyingi sana pale Guinea. Ni makosa makubwa sana kushindwa kuzigeuza nafasi zile kuwa mabao.

John Bocco ni mchezaji bora sana wa safu ya ushambuliaji nchini, lakini hakuwa na siku nzuri. Nafasi kama zile wakipata wenzetu hakuna masihara. Watu wanatupia mpira kambani. Watu wanatupia mpira nyavuni.

Bado tuna safari ndefu. Ni vigumu sana kusema timu zetu kama zitapata alama zote tisa za mechi tatu za nyumbani. Simba siwaamini. Yanga siwaamini. Wote ni walewale tu.

Yanga wamefungwa kirahisi ndani ya dakika 16 tu za kwanza. Simba wamepoteza nafasi nyingi sana za wazi. Kama makosa haya yatajirudia usishangae timu kufungwa kwa Mkapa. Kama mwendo ndio huu, hakuna wa kupata alama tisa nyumbani.

Matokeo ya timu zetu ugenini, hayaakisi kabisa ile nafasi ya tano kwa ubora Afrika tuliyoambiwa kwenye utafiti wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS). Mpira wetu bado sana japo kuna hatua kadhaa nje ya uwanja tumezipiga kwenda mbele.

Columnist: Mwanaspoti