Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ulingo wa Siasa: Shughuli ndio kwanza imeanza

Rais Samia X Zitto Shughuli ndio kwanza imeanza

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Shughuli ndiyo imeanza. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kuanza mchakato wa kurekebisha sheria pamoja na mipango ya kuukwamua mchakato wa Katiba.

Mikutano ya hadhara ilizuiliwa Juni mwaka 2016 na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kwa kile alichoeleza ni kuwapa wananchi muda wa kufanya kazi badala ya kupoteza muda kwenye mikutano hiyo ya vyama vya siasa.

Pia, mchakato wa kupata Katiba mpya ulikwama mwaka 2014 baada ya Bunge Maalumu la Katiba (BMK) kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo hata hivyo haikuwa na maridhiano kwa sababu wapinzani walitoka kwenye Bunge hilo na hivyo kuamuliwa na CCM na wajumbe wa kundi la 201.

Mabadiliko ya sheria na kanuni pia yalikuwa ni muhimu ili kuwezesha mikutano ya hadhara kufanyika kikamilifu lakini pia kuusimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambao umekuwa ukipiganiwa na vyama vya siasa na wanaharakati wengine.

Juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini na kuwaeleza ameruhusu mikutano ya hadhara kufanyika huku marekebisho ya Katiba yakiendelea na akijiandaa kuunda kamati maalumu ya kupitia maoni ya wadau kuhusu mchakato wa Katiba.

“Tunauanza mwaka tukitoa mikutano ya hadhara kuendelea, marekebisho ya sheria kadhaa yanaendelea yatakayohusisha vyama vya siasa na tunakwenda kuukwamua mchakato wa Katiba Mpya,” alisema Rais Samia.

Mikutano ya hadhara

Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Samia alitangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni zilizopo.

“Uwepo wangu leo (jana) hapa mahali, nimekuja kufanya ruhusa ya mikutano hii, nimekuja kutangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,” alisema.

Aliongeza “wajibu wenu ni kufuata sheria na kanuni zinavyotaka, lakini tufanye siasa za kistaarabu za kupevuka, kujenga na sio kubomoa au kurudi nyuma.

Rais Samia alisema ndani ya CCM wanaamini katika kukosolewa au kujikosoa na kwa sababu ndiyo walioiweka Serikali, ametoa ruhusa ya kukosolewa kwa kuambiwa changamoto ilipo ili akaifanyie kazi. Hata hivyo, alihimiza ukosoaji wenye staha na siyo wa kutukanana.

“Tusiende kutukana sio mila zetu tena katika majukwaa, sio mila zetu… wala desturi za Watanzania kusema wewe Samia huna adabu, miguu yako imekwenda upande, kichwa kama mbuzi yananipata, Samia Suluhu anaweza kuwa na moyo wa ustahimilivu kama alionao kwa sababu yananipata, lakini shabiki wangu ‘chawa’ anaweza asistahimili na anaweza akavaana na chawa wa aliyetukana, balaa litaanzia hapo. Basi tusiende kuchokozana, nendeni isemeni Serikali, ikosoeni na tunapokosea kwenye haki za binadamu semeni, tutarekebisha,” alisema Rais Samia.

Ilivyozuiliwa

Vyama vya siasa vilifurahia mikutano ya hadhara wakati wa utawala wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, hata hivyo Juni 2016, Rais Magufuli ambaye sasa ni marehemu alipiga marufuku huku akiagiza wabunge na madiwani waifanye katika maeneo yao.

Zuio hilo la mikutano licha ya kwamba linakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake, lilivunja pia Sheria ya Vyama vya Siasa.

Tayari Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akiwa katika ziara kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, alishatangaza kuanza mikutano ya hadhara kuanzia kesho.

Juzi aliyekuwa Meya wa Ubungo kupitia Chadema, Boniface Jacob ambaye mwaka 2020 aligombea ubunge wa Ubungo alionyesha barua aliyoipeleka ofisi ya mkuu wa polisi wa Wilaya Ubungo kutoa taarifa ya kufanya mkutano wa hadhara utakaofanyika Jumamosi hii, Kimara Mwisho.

Akizungumzia kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Rainery Songea, alisema hatua hiyo ni mwelekeo mzuri kwa duru za kisiasa na alichokifanya Rais Samia ni kuondoa zuio ambalo halikuwa halali kisheria.

“Alichokifanya ni kuturudisha katika mstari kwamba sheria inasemaje ni jambo la kupongezwa kwa sababu aliona kuna makosa yamefanyika. Changamoto iliyopo je kuna nia njema? Kwa sababu kabla ya kufanya mkutano unatakiwa kutoa taarifa polisi, huko nyuma walikuwa wanazuia je hali hii imebadilika?

“Kama dhamira hii itakuwa hadi kwenye vyombo vya dola basi itakuwa ni jambo jema, kwa sababu kazi ya siasa ni pamoja na kuongeza wanachama sasa kuwazuia wasifanye mikutano sio sawa, lakini nampongeza kwa jambo hili pamoja na kamati ya maridhiano imefanya kazi kubwa,” alisema Songea.

Kuukwamua mchakato wa Katiba

Akizungumzia mchakato wa Katiba mpya, Rais Samia alisema ni jambo ambalo amelichukua na atakwenda kuunda kamati maalumu ambayo itakuwa na jukumu la kuangalia namna bora ya kuukwamua mchakato huo.

Rais Samia alisema Serikali yake imedhamiria kuukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba mpya kwa namna watakavyokubaliana kwa siku za usoni.

“Tupo tayari kuukwamua ili tuanze sasa kwa kamati kadhaa kufanya kazi kadhaa za kuangalia mambo kadhaa. Tumekuwa tukiumiza vichwa, wengine wanasema tuanze na kamati ya Jaji Joseph Warioba na wengine Katiba Pendekezwa ya Bunge Maalumu la Katiba.

“Ile ilikuwa mwaka 2014, sasa ni miaka nane, kuna mambo kadhaa yameshabadilika, sasa kuna haja ya kuangalia hali halisi ya sasa hivi ikoje, je, yaliyomo mle mangapi yanatufaa na yapi hayatufai, tunakwendaje? alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa inawezekana Katiba ya Jaji Warioba na Katiba Pendekezwa zikawa siyo vyanzo vizuri vya kuanzia mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa sasa, lakini wanaweza wakaanza kwa Katiba ya sasa kwa kuangalia mazuri au kushauri yapi yarekebishwe kwa kuchukua vipande kutoka katika Katiba hizo mbili.

Rais Samia aliwahakikishia viongozi hao wa vyama vya siasa kwamba muda si mrefu wataanza na kamati itakayoshauri namna ya kuliendea jambo hilo. Alisema kamati hiyo itajumuisha Watanzania kutoka sekta na nyanja zote.

“Tutakuwa na vyama vya siasa, asasi za kijamii, Watanzania walioko katika jumuiya za kimataifa, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, ili waje na kitu cha Watanzania sio vyama vya siasa. Faraja ninayowapa kwamba madai yenu ya muda mrefu yanakwenda kukwamuliwa na kufanyiwa kazi.

Mkuu huyo wa nchi alisisitiza kamati hiyo, itafanya kazi kwa kufuata hadidu za rejea watakazopewa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao.

“Tunataka wakati mchakato huu unaendelea nchi iwe tulivu ikiendesha shughuli zake za maendeleo, sio vuguvugu litakalokwenda kusimamisha kila kitu kwa kuangalia Katiba. Watanzania hawatashiba, ikiingia njaa wakulima mtanipigia kelele au tusipojenga na kuboresha vituo vya afya, mtapiga kelele.

“Kazi za maendeleo lazima ziendelee lakini mchakato nao uanze ili kuelekea katika marekebisho ya Katiba ya Tanzania,” alisema Rais Samia ambaye katika Bunge Maalumu la Katiba alikuwa mwenyekiti mwenza.

Maoni ya wadau

Mkuu wa Idara ya Haki, Amani na Uadilifu wa Uumbaji katika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Kasala Camillius alisema siasa ni sehemu ya himaya ya Mungu, ndiyo maana si ajabau kwa kiongozi yeyote akiwa anamaliza kiapo chake anasema eeh ‘Mungu nisaidie’.

Alisema Katiba ni waraka rasmi wa kimaadili wa Taifa, pia hakuna andiko katika kuendesha nchi zaidi ya Katiba. Alisema huwezi kutenganisha masuala ya uchaguzi, mabadiliko ya sheria, mikutano na yote yanayohusu uendeshaji huwezi kulizungumzia nje ya Katiba.

“Yote yaliyotajwa na Rais Samia ikiwemo mikutano huwezi kutenganisha na mchakato wa Katiba, hatuwezi kuleta mabadiliko bila kubadili Katiba. Tunaposema Katiba si ya wanasiasa bali ya watu wote na Katiba tuliyochangia mwaka 2014 si nyingine ni Rasimu ya Warioba iliyohusisha makundi yote.

“Kama sauti ya watu ni sauti ya Mungu, Rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba inaakisi sauti ya Mungu kwani ni sauti ya Watanzania.Siasa ni sehemu ya himaya ya Mungu, kwa hiyo viongozi wasikilize sauti ya Mungu ambayo ipo katika Rasimu ya Warioba yote aliyoyazungumza Rais Samia,” alisema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Rainery Songea alipongeza hatua hiyo, akisema italeta mageuzi makubwa hasa katika masuala ya uchaguzi na michakato yake hasa Tume Huru na sheria za uchaguzi. Alisema jambo likafanyika vizuri tutengeneza Tanzania bora.

“Suala la Katiba Mpya ni jambo jema na hatuna haja ya kuanza upya, bali turudi hatua moja nyuma tulipoishia kwa sasa hivi kuna mambo mengi yamebadilika kama wameanza maridhiano wanaweza wakajadili na hili namna ya kwenda mbele,” alisema Songea.

Columnist: Mwananchi