Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukweli kuhusu mkaa 

9d194c7977afb2a33033e531f7bb56e7 Ukweli kuhusu mkaa 

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“KAMA kuna mtu hapa hajawahi kutumia mkaa anyooshe mkono.”

Hilo ni swali lililoulizwa siku moja na Meneja wa Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoFCorEST), Charles Leonard, wakati akianza kuwasilisha mada yake kuhusu mradi huo.

Walioulizwa ni washiriki wa semina kuhusu mambo muhimu yahusuyo Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) na Usimamizi wa Pamoja wa Misitu (JFM) uliohusisha pia waandishi wa habari waandamizi na wahariri zaidi ya 40.

Leonard alisubiri kwa takribani nusu dakika, lakini hakuna aliyenyoosha mkono juu kukubali kwamba katika maisha yake hajawahi kutumia nishati ya mkaa kwa ajili ya kupikia, kuchomea nyama au mahindi.

Akauliza swali lingine: “Ni nani ameacha kutumia mkaa isipokuwa sasa anategemea nishati mbadala pekee?” Hakuna tena aliyenyoosha mkono.

Akauliza tena swali la tatu: “Ni nani kati yenu hawezi tena kutumia nishati ya mkaa maishani mwake?” Kama ilivyokuwa kwenye maswali mawili ya awali, hakuna mwanasemina aliyenyoosha mkono.

Kupikia mkaa kunaweza kukoma mwaka huu?

Meneja huyo wa mradi kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), alisema ukimya uliojitokeza kwa kutopatikana mtu ambaye ameacha kabisa kutumia nishati ya mkaa kwa ajili ya kupikia, unadhihirisha hali halisi ilivyo nchini mwetu.

Hivi karibuni, katika warsha na ziara ya mafunzo iliyofanyika mkoani Morogoro ikihusisha maofisa mawasilino kutoka taasisi mbalimbali za serikali pamoja na waandishi wa habari, Meneja huyo pia alisema kupitia takwimu zilizopo, bado asilimia 96 ya kaya nchini zinategemea nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na kwamba asilimia 91 ya kaya katika jiji la Dar es Salaam zinategemea pia mkaa.

“Hili linaonesha pia kwamba kukataza matumizi ya mkaa mijini haiwezekani angalau katika wakati tulio nao sasa. Sana sana itakuwa inaongeza bei ya mkaa tu kwa walaji,” anasema.

Anasema kwamba kutokana na ukweli huo, zaidi ya tani milioni 2.3 za mkaa zinatumika kwa mwaka hapa nchini na kwamba mchango wa sekta ya mkaa kwenye uchumi wa nchi ni takribani Sh trilioni 2.2. Anasema hakuna zao lolote la biashara nchini linalingana na mkaa katika kuingiza pesa.

Hata hivyo, anasema kwamba kutokana na kutokuwa na sera makini katika sekta hiyo ya mkaa ili kuwa na uzalishaji mkaa endelevu, mapato yanayopotea kwa mwaka ni takribani Sh bilioni 220.

Kwa mujibu wa Leonard, ingawa matumzi ya mkaa bado hayakwepeki, mkaa mwingi unaotumiwa na wananchi unazalishwa kiholela na kwa njia ambazo sio endelevu, hali inayochangia uharibifu mkubwa wa misitu.

Leonard anasema ingawa kinachozungumzwa sana na watunga sera kwa sasa ni nchi yetu kujielekeza katika uzalishaji wa nishati mbadala ya kupikia, hususani mkaa mbadala, gesi na umeme, bado ni jambo ambalo litatuchukua miongo kadhaa kulifikia.

“Nitoe mfano. Imani iliyopo ni kwamba wakazi wengi wa Dar es Salaam wana kipato cha wastani. Jiji hilo pia halina shida ya umeme wala mitungi ya gesi, lakini ndilo linaloongoza nchini kwa kutumia mkaa mwingi,” anasema.

Nini kifanyike?

Washiriki wa warsha walitembelea kijiji kimoja kati ya 35 vinavyotekeleza progamu ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu na kushangaa kuona jinsi wanakijiji wanavyotunza misitu huku wakizalisha mbao na mkaa kwa njia endelevu na kukiwezesha kijiji kikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo bila kuchangisha wananchi.

Kijiji walichotembelea ni Kitunduweta kilichoko Wilaya ya Kilosa, Morogoro, ambako Mtendaji wa kijiji hicho, Thomas Lukoo alisema kijiji kilianza kutekeleza Usimamizi Shirikishi wa misitu mwaka 2016 kupitia mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa nchini (TTCS) ambao ulishamaliza muda wake.

Alisema kabla ya mradi, kijiji hakikuwa na mapato yoyote lakini baada ya mradi wamekuwa wakipata wastani wa Sh milioni 28 kwa mwaka.

Akasema pesa hizo zimewawezesha kujenga darasa na kukarabati madarasa mawili, kujenga nyumba ya mwalimu mkuu, kujenga choo cha kisasa na kununua madawati. Pia alisema wamemudu kulipia bima za afya kwa kaya zote 378 kijijini hapo.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na asilimia 40 ya mapato yao kwani asilimia 60 inakwenda kwenye ulinzi wa msitu wa kijiji.

Alifafanua kwamba mradi umesaidia kuleta elimu kubwa ya uhifadhi na ulinzi wa msitu kiasi kwamba uvunaji holela ni kama umeisha kwani wananchi ni walinzi madhubuti baada ya kuona faida ya msitu wao.

Wachoma mkaa walieleza wanavyonufaika baada ya kutoka kwenye uchomaji wa kujificha ficha uliokuwa unaharibu misitu hadi uchomaji rasmi na endelevu unaowapa faida kubwa wao na kijiji.

Kulangwa Ganda alisema hutengeneza faida ya zaidi ya sh 400,000 kila mwezi kutokana na mkaa ambapo kila tanuri hutumia gharama ya wastani wa Sh. 150,000 kuwalipa watu wa kumsaidia na kwamba kama biashara ni nzuri huchoma wastani wa matanuri mawili kwa mwezi.

"Miongoni mwa mafanikio ambayo nimepata kutokana na kuchoma mkaa ni kusomesha watoto wangu na pia nimefungua duka," alisema.

Kwa nini unaitwa mkaa endelevu?

Kijiji kinachofanya USMJ kwanza hupima eneo lote la kijiji na kisha kuwa na matumizi bora ya ardhi, hatua inayowezesha kutenga eneo la msitu, eneo la mifugo, makazi na huduma za jamii.

Katika msitu hutengwa asilimia 10 hadi 15 tu ya eneo ambalo ndilo huachwa kwa ajili ya kuzalisha mkaa kwa miaka yote na eneo lilolobaki haliguswi.

Ndani ya eneo hilo, vitalu vya mita 50 kwa 50 hutengwa na kama kitalu A kitavunwa leo, kitalu B kinarukwa na kuja kuvunwa baada ya miaka 12 huku kilichovunwa leo kikirejelewa baada ya miaka 24, wakati kimerejea kuwa msitu.

Ndani ya kitaku kinachovunwa, miti mdogo, miti ya mbao, miti yenye makazi ya viumbe hai kama nyuki au wanyama wadogo haiguswi.

Programu inatekelezwa kwenye maeneo yenye misitu ya miombo kwa sababu ina uwezo wa kuchipua na hivyo hata ukataji wa mti huacha shina ili litoe machipukizi ambayo baada ya miaka 24 huwa mti mkubwa unaofaa kuvunwa tena.

Wachoma mkaa hupata vibali kutoka kwenye kamati ya maliasili ya kijiji ambayo hubaki na asilimia 60 ya mapato kwa ajili ya ulinzi na doria za mara kwa mara kwenye msitu wa kijiji.

Washiriki wa warsha walisema nini?

Baada ya ziara ya mafunzo na mada zilizowasilishwa, washiriki wa warsha walikiri kwamba kama Usimamizi Shirikishi wa Misitu utafanyika nchi nzima, miti italindwa, vijiji, halmashauri hadi serikali kuu itapata mapato yanayopotea bure.

Kwamba zile Sh bilioni 220 zinazopotea kila mwaka sasa zitaingia kwenye mikono salama na kuleta maendeleo.

Bashiri Salumu, Ofisa habari wa Wizara ya Kilimo, alielezea kukoshwa na aliyoyaona Kitunduweta likiwemo suala la kijiji kulipia kaya zote 378 bima ya afya iliyoboreshwa.

Lakini alionekana kusita kuamini kama ilivyoelezwa kwenye mada kwamba kilimo, hasa cha kuhamahama, ndicho kinaongoza kwa kumaliza misitu kwa mujibu wa tafiti zilizo na siyo mkaa.

Leonard alimhakikishia kwamba kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na TFCG miaka ya karibuni, asilimia 89 ya ufyekaji misitu inatokana na kilimo.

Alisema ingawa misitu ina faida nyingi lukuki kwa mwanadamu kama vile kulinda vyanzo vya maji, kuvuta mvua, kunyonya hewa ukaa na kusaidia kupunguza tatizo la mabadiliko ya tabianchi watu wanapohifadhi misitu ya asili haionekani kama ni shughuli ya maendeleo bali wakifyeka misitu inaonekana mtu amefanya maendeleo!

“Utasikia watu wanasema, ‘hajaendeleza eneo lake, ameliacha tu kama pori’,” alisema akionya namna nchi itakavyogeuka jangwa kama uharibifu wa misitu utaendelea kama ilivyo sasa.

Alisema hakuna anayepinga kupanua kilimo nchini kutokana na ongezeko la watu lakini kinachotakiwa ni kuendesha kilimo hifadhi ambacho kinafanya mtu kulima eneo dogo na kupata mavuno mengi.

Kawa Kafuru kitoka NEMC alisema: “Nimejifunza mengi na kama ofisa wa NEMC itanisaidia kutoa elimu ya namna ya kutunza misitu bila kuathiri mazingira ya kijiji kama nilivyoona kule Kitunduweta.

“Kimsingi tumeona USMJ ni kitu kizuri kwa kuwa kinamgusa mtanzania. Unatunza mazingira na kuyaboresha na hata Waswahili wanasema mchawi mpe mwanao akulelelee. Wananchi wanapewa msitu wanaulea na hiyo. Kimsingi ni njia nzuri ya kutunza msitu ni kushirikisha jamii.”

Robert Hokororo, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais alisema amejifunza kwamba watu wasikate miti, lakini amegundua yanayofanyika kwenye vijiji vinavyofanya uvunaji endelevu, miti inavunwa na kutunzwa.

“Nimejifunza kwamba kumbe miti inaweza ikalindwa huku ikileta faida.”

Fredrick Kibano, Ofisa Habari Tamisemi alisema: “Nitapiga debe angalau asilimia kadhaa ya mafungu iende kwenye USMJ. Pia nitapigania ili maofisa habari wawe wanashirikishwa kwenye miradi kama hii.”

Issa Kibuga kutoka Idaya ya Habari na Mawasiliano, Halmashauri ya Kilolo alisema: “Nimejifunza kwamba wananchi wakishirikishwa katika kuvuna misitu yao wanaweza kutunza vyema misitu. Wakati tunapita na gari niligundua kwamba kama misitu ingekuwa hailindwi tusingekuwa tunaona kiasi hicho kikubwa cha miti ambayo haijakatwa.”

Columnist: www.habarileo.co.tz