Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukubwa wa Yanga uendane na vitendo Afrika

Mgunda Na Yanga Ukubwa wa Yanga uendane na vitendo Afrika

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga ni miongoni mwa timu kubwa na kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Tanzania inajivunia rekodi kibao, ikiwemo kuongoza kwa mataji ya Ligi Kuu yapatayo 28.

Ukubwa wao kwenye ligi hautoshi kujivunia bado wanapaswa kufanya kitu tofauti na kile kilichozoeleka ili waendelee kuitwa wao ni wakubwa.

Ukubwa wao unatakiwa uonekane kwenye mashindano makubwa ngazi ya Afrika baada ya kufanikiwa kuikamata ligi, kinyume na hapo bado wao hawawezi kutamba na kujiona ni wakubwa wakati hawaonekani wakifanya kitu kikubwa.

Unapozungumzia mashindano makubwa yanayotambulika ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo ni muhimu kwao kufanya juhudi zao kuonesha ukubwa wao. Tayari walikosea kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakashindwa kuingia hatua ya makundi baada ya kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Nyumbani wakilazimishwa sare ya bao 1-1 na ugenini wakifungwa bao 1-0. Pamoja na ukubwa wa timu hiyo, lakini bado haijafanya mambo makubwa Afrika kwani wameshindwa kabisa kutamba barani Afrika.

NAFASI

Jambo la kushukuru kwao hawajatolewa kwenye mashindano wameangukia Kombe la Shirikisho na sasa wana nafasi ya mwisho kuhakikisha wanadhihirisha ukubwa wao kwa kufanya vizuri ili kusonga hatua ya makundi.

Wanatarajia kucheza na Club Africain ya Tunisia. Ni timu nzuri, lakini sio ya kutisha kama Yanga itaamua kujipanga inaweza kufanya vizuri. Ni wazi kwamba mashabiki wao wanatamani kuona timu yao ikifuzu makundi kwa sababu mara ya mwisho kuingia hatua hiyo ilikuwa mwaka 1998.

Ni miaka mingi kwa timu kama hiyo inayojivunia mafanikio ya ndani kushindwa kutamba kimataifa.

Yanga ina nafasi ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo ikiwa itawaheshimu wapinzani wao na kuhakikisha inatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri kabla ya kwenda kumaliza mechi ugenini.

IJIFUNZE

Yanga inaweza kujifunza kwa watani zake wa jadi Simba ambao kwa miaka ya karibuni wameonesha umahiri wao kwa kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa. Miaka ya nyuma Simba ilikuwa inafanya vibaya katika mechi za ugenini ikifungwa mabao mengi, lakini kadiri miaka ilivyosogea walijifunza kwa kufuta uteja huo.

Leo Simba ikishiriki michuano ya kimataifa viongozi wake hujipanga na sasa na wamekuwa ni tishio barani Afrika. Namna wanavyojipanga dhidi ya wapinzani wameonesha wao ni wakubwa na wamedhamiria kufanya kitu.

Kwa mwenendo wa Simba ipo siku watachukua ubingwa wa Afrika. Hivyo, hata Yanga wasione aibu kujifunza kwa wenzao na kuona wanafanya nini hadi wanafanikiwa.

Kuna mtazamo hasi watu wamekuwa nao kuwa mpinzani wako atakusaidiaje, lakini inawezekana kujua tu wanafanya nini hadi wanafanikiwa na wao wafanye kwa manufaa yao.

CLUB AFRICAIN

Ni miongoni mwa klabu chache kongwe barani Afrika iliyoanzishwa miaka 102 ikijulikana kwa jina maarufu kama Al Club kabla ya kubadilishwa jina. Ndio timu ya pili kwa ukubwa na kwa mafanikio nchini Tunisia nyuma ya Esperance Sportive de Tunis iliyoanzishwa mwaka 1919.

Ndio klabu ya kwanza kushinda Kombe la CAFCL kwa kipindi hicho iliitwa African Champions League. Katika mafanikio ya ligi ya ndani inashika nafasi ya pili ikiwa na jumla ya mataji 39 huku Esperance ikiwa na mataji 53.

Kwenye Ligi Kuu ya Tunisia imetwaa jumla ya mataji 13. Timu hiyo imewahi kuwa mabingwa wa ligi ya mabingwa barani Afrika katika msimu wa mwaka 1991 ikimfunga SC Villa ya nchini Uganda kwa jumla ya mabao 7-2.

Mechi zilichezwa mbili nyumbani na ugenini ilikuwa sare ya bao 1-1 na nyumbani kwao walishinda mabao 6-1. Kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho timu hiyo ilimtoa Kipanga ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 7-0.

Mchezo wa kwanza uliochezwa Zanzibar walitoka suluhu na ule wa marudiano wakashinda idadi hiyo ya mabao wakiwa kwao. Timu hii inaonekana ni hatari hasa ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani hufanya kila namna kuhakikisha inapata matokeo mazuri.

YANGA IFANYE NINI

Yanga inapaswa kuhakikisha mipango ya nyumbani inawekwa vizuri kumaliza mechi nyumbani. Mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Novemba 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga ihakikishe inashinda mabao kuanzia mawili, matatu na hata manne ili wakienda ugenini wajipange kukabiliana na fitna za Waarabu. Hawapaswi kuruhusu bao la mgeni kama walivyofanya kwa Al Hilal kwa sababu wakifanya hivyo wanawapa nafasi ya kujiamini zaidi na kuwavurugia mipango.

Inawezekana kabisa viongozi wa klabu hiyo walishaona kuna kitu walikosea wasikubali kurudia makosa, wakifanya hivyo, basi watakuwa wamejiondoa wenyewe kwenye mashindano.

Pia, kuwaandaa wachezaji kisaikolojia wanapokuwa nyumbani wafanye nini na wanapoenda ugenini zile fitina wafanyeje kuzikwepa na kwa uhakika watavuka. Waarabu wamekuwa na fitna hasa wanapokuwa kwao ndio maana Club Africain wanapokuwa ugenini wanaonekana kabisa kutafuta sare ili kwenda kwao kumaliza kazi.

Yanga ina kila sababu ya kushinda ili kulinda ukubwa wao kwa kuwa wana kikosi kizuri ni mbinu tu zinahitajika kuwazidi wapinzani za ndani na nje ya uwanja.

NJE YA UWANJA

Mbali na uwanjani, Yanga pia inatakiwa ijiimarishe nje ya uwanja kwa kujenga miundombinu bora ya uwanja wao kama zilivyo timu kubwa za Afrika.

Yanga wanashindwa hata na timu kama Azam, iliyoanzishwa miaka michache iliyopita, lakini tayari wana uwanja wao ambao wanaweza hata kuutumia katika mashindano ya kimataifa.

Columnist: www.tanzaniaweb.live