Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukocha utazima 'kiu' ya ajabu ya Juma Kaseja?

Kaseja Coach Ukocha utazima 'kiu' ya ajabu ya Juma Kaseja?

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Inatokea mara chache katika mchezo wa soka. Kocha wa makipa wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ bado hajastaafu soka na anawinda timu ya kuchezea. Zamani kulikuwa na nafasi maarufu ya kocha mchezaji lakini huwa inatokea kwa makocha ambao ni wachezaji wa ndani.

Mapema wiki iliyopita Juma Kaseja alikuwa amegoma kustaafu soka baada ya kuachwa na klabu yake ya KMC. Halafu wiki hiyo hiyo alichaguliwa kuwa kocha wa makipa wa timu ya taifa ambayo ilisafiri kwenda kucheza Uganda dhidi ya Uganda Cranes michuano ya Chan.

Wakati huu, Juma anasaka timu kama mchezaji, lakini yupo katika benchi la ufundi la Taifa Stars kama kocha wa makipa. Majuzi wakati akihojiwa na Redio ya Wasafi aliweka wazi anasubiri timu ambayo itataka huduma zake kwa sababu anajiona bado yupo fiti.

Huyu ndiye Kaseja ninayemfahamu. Kuamkia wiki hii sijajua msimamo wake kama amenogewa na kazi yake mpya au bado anatamani kuendelea na kazi yake ya zamani. Hata hivyo, natabiri kwamba bado anatamani kuendelea na kazi yake ya zamani.

Hata wakati akiwafua Aishi Manula, Abdultwalib Mshery na Beno Kakolanya kuelekea katika mechi dhidi ya Uganda, nadhani Juma alikuwa anaona anastahili zaidi kuwania nafasi yake na makipa hao na sio kuwa kocha wao.

Kuna baadhi ya wachezaji walicheza na Juma zamani kama Suleiman Matola na Boniface Pawassa kwa sasa wanaonekana tayari ni makocha wa muda mrefu. Walishasahau mambo ya uchezaji lakini Kaseja bado yupo langoni tu na ana hamu kweli kweli.

Kwa nini Juma yupo kama alivyo? Kitu cha kwanza ni kwamba yupo fiti. Inawezekana sio kama alivyokuwa awali lakini Juma anapenda mazoezi. Bila ya kufanya mazoezi hasikii raha. Yupo tayari aondoke nyumbani na mipira yake miwili aende mitaani akafanye mazoezi na vijana. Ni mchezaji tofauti kidogo na wengine.

Kama tungekuwa na wachezaji wengi wa ndani wenye tabia kama ya Juma si ajabu wangefika mbali. Kaseja huwa hana likizo, wikiendi wala mapumziko. Sawa kwa sasa kuna mambo mengi yamepungua kutoka kwake lakini kwa tabia za wachezaji wetu, hata makipa, ni nadra kucheza kwa muda mrefu kama yeye alivyofanya.

Mtandao wa Wikipedia unaonyesha Kaseja ana umri wa miaka 37 lakini hata kama ukisema amedanganya umri, basi hilo litakuwa jambo la kustaajabisha na atakuwa ameingia katika orodha ya wachezaji wachache sana waliocheza hadi miaka 40. Mmojawapo ni Madaraka Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio’.

Inawezekana Kaseja hayupo katika uwezo wa baadhi ya makipa wa Ligi Kuu wa sasa kama vile Manula lakini katika soka letu ni kwamba anacheza katika kiwango cha juu. Kiwango cha Ligi Kuu. Kuna tofauti kubwa ya kucheza Ligi Kuu na kucheza soka la madaraja mengine au soka la kujifurahisha.

Kitu kingine ambacho inawezekana kinamzuia Kaseja kustaafu ni ukweli kwamba kuna viwango vya makipa wengi wa Ligi Kuu ambao wanamtamanisha ajione bado yuko bora. Sio siri, katika zama hizi makipa wetu hawana ubora mkubwa.

Labda ingekuwa zama za zamani za akina Riffat Saidi, Mohamed Mwameja, Steven Nemes, Paul Rwechungura, Madata Lubigisa, Ali Bushiri na wengineo, huenda Kaseja angejiona amechuja na angeamua kupumzika.

Kwa hali ilivyo sasa Juma anaendelea kutamani kucheza. Chukulia mfano jinsi KMC walivyomkutanisha na kipa wa kimataifa wa Kenya, Farouk Shikalo waliyemchukua kutoka Yanga. Shikalo ana umri wa miaka 25 tu lakini alikuwa na makosa mengi kuliko Kaseja. Matokeo yake kocha akajikuta akiwapanga kwa kupokezana. Ilipaswa Shikalo achukue nafasi yake jumla na Juma awe msaidizi lakini kiwango chake kilikuwa kinatia mashaka.

Wakati mwingine makipa kama Juma wanakuwepo kikosini kama makipa wa akiba kutokana na umri wao kusogea. Wapo akina Lee Grant au Willy Caballero ambao walicheza wakiwa na umri mkubwa kama makipa wa akiba zaidi. Hata hivyo, ushindani mdogo kutoka kwa makipa unamfanya Juma ahisi anaweza kucheza katika kiwango cha juu kwa muda mrefu.

Kitu kingine ambacho inawezekana kinamtamanisha Juma ni aina ya wachezaji wetu wa ndani. Mshambuliaji gani amempa shida tangu atue katika timu za kawaida? Sawa huwa anafungwa lakini sidhani kama amepata mikikimikiki ya kutosha ya kumstaafisha.

Kama angekuwa anacheza timu kubwa kama Simba na Yanga nadhani ndio angekuwa likizo zaidi. kiwango cha timu nyingine kinapaswa kumstaafisha Kaseja. Kama anajiona yupo fiti kuendelea kucheza basi ni kwa vile anatembea na takwimu zake mkononi.

Majuzi wakati akihojiwa na waandishi wa habari alikuwa ana takwimu zake za msimu uliopita ambazo alidai ukizilinganisha na za makipa wengi bado takwimu zake zinabakia kuwa bora. Akiwa langoni katika mechi ambazo alikuwa amecheza amepoteza mechi chache kuliko alizoshinda.

Sijui kama Kaseja atapata timu lakini nadhani pia kuna wepesi wa yeye kupata timu kwa sababu kuna klabu nyingi ambazo zinamuona yeye ni bora kuliko makipa wengi vijana. Haishangazi kuona baada ya kuondoka Simba na Yanga alipata fursa ya kuzurura Kagera Sugar, Mbeya City na KMC.

Lakini kama akiamua kuachana na soka letu na akaanza maisha mapya ya ukocha bado Juma anatuachia funzo katika soka letu. Ni Gwiji. Miaka aliyosimama langoni ni ishara tosha kwamba alikuwa mchezaji mwenye nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja. Vijana wengi inabidi wamsake alipo ili awape siri ya mafanikio yake. Sio kitu rahisi kucheza misimu 20 ya Ligi Kuu. Katika suala la kumfuata, haijalishi wewe unacheza nafasi gani.

Columnist: Mwanaspoti