Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukishangaa ya Mandonga utakutana na ya Azam FC

Azam Last Training Azam FC wakijifua

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unajikuta namna ambavyo unamshangaa bondia Karim Mandonga namna anavyojitamba katika mchezo wa ndondi. Mdomo mwingi lakini kila siku tunamshuhudia akilamba sakafu. Wote tunajikuta tunacheka. Muda si mrefu tutajikuta tukimchoka.

Inanikumbusha timu inayoitwa Azam. Timu ya kitajiri. Kama ilivyo kwa Mandonga, Azam ni timu yenye majigambo kabla ya msimu kuanza. Na msimu huu walionekana kujiandaa kuwa na msimu bora pengine kuliko msimu wowote waliokuwa nao miaka ya karibuni.

Walianzia wapi? Walipofanikiwa fitina yao ya muda mrefu ya kumnasa Fei Toto. Baada ya vurugu za muda mrefu kati ya Fei na klabu yake ya zamani Yanga mwishowe tukajua kwamba kumbe nyuma yake walikuwa wamesimama rafiki zetu wa Azam. Yanga walipoagizwa na Mheshimiwa Rais wamalizane na Fei ghafla Azam wakaibuka mezani kumchukua mchezaji wao.

Wachambuzi na mashabiki wakaanza kuipanga safu ya kiungo ya Azam huku wakimaliza maneno. Kwamba hapa kutakuwa na James Akaminko pale kutakuwa na Sos Bajana halafu mbele yao atakuwepo Fei. Tukaulizwa, kutakuwa na safu ya kiungo kama hii katika Ligi Kuu Bara na michuano mbalimbali ya timu za Tanzania?

Azam wakaenda kujifungia Tunisia. Kilichotokea huko hatufahamu sana zaidi ya matokeo mabaya ya Pre Season. Hata hivyo, ilikuwa vema kuweka akiba ya maneno kwa sababu walicheza na timu bora ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ambayo ina maendeleo makubwa ya soka.

Baadaye wakarudi kucheza Tanga katika michuano ya ajabu ya Ngao ya Jamii ambayo ilishirikisha timu nne. Tangu lini Ngao ya Jamii ikashirikisha timu nne? Mechi yao ya kwanza dhidi ya Yanga walikimbizwa kwa dakika zote 90. Haikujulikana timu ipi ilikuwa imeweka kambi Tunisia na ipi ilikuwa imeweka kambi Kigamboni.

Muda mwingi waliishia kucheza rafu. Awali, walionekana kama timu ambayo baada ya kuwachukua kina Fei na Yannick Bangala labda wangefanikiwa kuziba pengo lililokuwapo msimu uliopita. Haijawezekana. Yanga na Azam vilikuwa vitu viwili tofauti.

Na sasa imewadia michuano ya kimataifa. Azam walitazamiwa kufika mbali lakini wameondolewa katika michuano na timu dhaifu ya Bahir Dar Kanema kutoka Ethiopia. Ndio ni timu dhaifu kama utalinganisha uwekezaji mkubwa unaofanywa na Simba, Yanga na Azam kwa sasa. Hauwezi kusema umecheza na timu ngumu kutoka Ethiopia, Djibouti au Eritrea kwa sasa.

Kule Azam alifungwa 2-1 na marudiano wakashinda kama hivyo. Mechi ilikwenda katika matuta na Azam imetolewa katika staili ile ile ya Mandonga. Kila mtu amebaki mdomo wazi. Nini shida ya Azam? Ukweli ni kwamba hatujui. Kila mtu amewahi kutoa mawazo yake lakini sijaona wazo ambalo halijawahi kufanyiwa kazi pale Azam. Hata hivyo, timu bado haiendi.

Mabilioni ya pesa yameendelea kuzama pale Azam lakini hakuna kinachobadilika. Watendaji wamewahi kubadilishwa mara kadhaa lakini Azam imeendelea kuwa ile ile. Wachezaji mastaa wamebadilishwa Azam lakini Azam imeendelea kuwa ile ile. Makocha wamebadilishwa Azam lakini Azam imeendelea kuwa ile ile.

Azam iliwahi kuleta menejimenti kutoka Hispania lakini Azam imeendelea kuwa ile ile. Hili la juzi limewatia uchungu hata watu wa Simba na Yanga ambao huwa hawaichukii Azam pindi linapokuja suala la michezo ya kimataifa. Imesikitisha sana na imezidi kuibua swali lile lile, shida ya Azam ni nini?

Hawa Bahir wangecheza na Simba na Yanga si ajabu wangefungwa Adis Ababa na Temeke. Nilitazama pia pambano la KMKM dhidi ya St George. Sawa, Wazenji walifungwa lakini nilipotazama kiwango cha St George niligundua kwamba timu za Ethiopia, Djibouti na Eritrea sisi sio saizi yao tena.

Kwa uwekezaji wetu tunapaswa kuzifunga. Na hata kwa viwango uwanjani pia tunapaswa kuziondosha katika mashindano mapema tu. Katika uwanja wao huo huo, Yanga waliionyesha Azam kinachopaswa kufanyika Chamazi. Kesho yao waliwadunda Wahabeshi wengine kipigo kizito cha mabao 5-1. Haya ndio matokeo ambayo Azam walistahili kuyapata nyumbani na ugenini.

Sijui familia ya Mzee Bakhresa itakuwa inafikiria nini kwa sasa lakini ukweli ni kwamba timu inawaangusha. Wakati mwingine unatamani hii familia wangeinunua timu kama Simba hivi. Kinachotokea kwa Azam ni kwamba timu inakosa upambanaji kwa sababu sio timu ya wananchi.

Waingereza wanaita passion. Azam ndio timu ambayo inaweza kufungwa kizembe lakini usisikie kelele zozote kutoka kwa wananchi. Kama juzi ingekuwa imetolewa Simba au Yanga basi nchi ingezizima. Lakini kwa Azam inakuwa shwari. Hakuna presha kubwa kwa wachezaji wala viongozi. Maisha yanaendelea.

Kama Simba au Yanga mmoja angetolewa vile leo tungekuwa tunazungumzia basi la wachezaji kupigwa mawe. Tungezungumzia kocha kupigwa kofi na shabiki. Tungezungumzia majigambo hadi bungeni. Lakini kwa Azam hakuna presha hii. Mara ngapi hata marefa wanaionea Azam kwa sababu hawaogopi kuionea?

Lakini hata matajiri wa Azam wapo mahali salama zaidi. Ukiwa Ghalib Mohammed au Mohammed Dewji pindi unapoona mashabiki wanalia kwa sababu timu imefungwa unajua kwamba unawajibika moja kwa moja na kichapo. Unahisi mzigo ni wako. Lakini umewahi kumuona shabiki wa Azam akilia?

Unapomuona shabiki ana furaha iliyopitiliza unajua kuwa unahusika moja kwa moja na furaha hiyo. Ni tofauti na Azam. Haishangazi kuona kwamba kunakuwa hakuna presha kwa kila anayehusika na timu. Timu sio ya wananchi. Wachezaji wapo salama, benchi la ufundi lipo salama na matajiri wapo salama.

Aishi Manula aliwahi kufungwa mabao ya mbali akiwa katika lango la Azam lakini siku alipofungwa bao la mbali na Mapinduzi Balama katika pambano la watani wa jadi ilikuwa kama vile ameua mtu. Hizi ndio Simba na Yanga ninazozifahamu. Mechi ijayo mchezaji lazima uwe na presha ya kufanya vizuri zaidi.

Kama pesa naambiwa kwamba wachezaji wa Azam waliahidiwa pesa ndefu katika pambano la Ethiopia na hili la juzi. Hata hivyo, wameshindwa kuzichukua. Wakati mwingine pesa sio kila kitu, unahitaji kupigwa presha ya kitu kingine ili upate matokeo.

Columnist: Mwanaspoti