Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukame hat trick...Ni ubora wa mabeki au udhaifu wa mastraika

Hat Pic Ukame hat trick...Ni ubora wa mabeki au udhaifu wa mastraika

Tue, 31 May 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-2022 imesaliwa na mechi za raundi tano tu kabla ya kufikia tamati, huku Yanga ikiwa hatua chache kabla ya kutawazwa kuwa mabingwa.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 64, baada ya mechi 26, ikifuatiwa na watetezi, Simba inayoshika nafasi ya pili na alama zao 51 baadaya mechi 25.

Licha ya ligi kuelekea ukingoni huwezi kuamini kuwa, hadi sasa ligi ikiwa imechezwa mechi 206 na kushuhudiwa jumla ya mabao 401 yakitinga wavuni, yakiwamo 97 yaliyofungwa na nyota wa kigeni 36, lakini kukiwa kuna hat-trick moja tu.

Hat trick hiyo pekee kwa msimu huu kwa sasa iliwekwa kimiani na nyota wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma wakati timu hiyo ya maafande ikiizamisha Namungo kwa mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Novemba 27, 2021 mjini Sumbawanga, Rukwa.

Kuwepo kwa uhaba wa hat trick ndani ya msimu huu unazua maswali kwa wadau, wakihoji ni umakini mdogo na udhaifu wa washambuliaji wa klabu 16 za ligi hiyo au ni ubora na uimara wa mabeki wa timu hizo ama ni umahiri wa makipa wa timu shiriki?

Maswali hayo yanakuja kutokana na takwimu za misimu mitatu iliyopita ya ligi hiyo ikishuhudiwa zaidi ya hat trick moja zikifungwa katika msimu mmoja.

Misimu miwili iliyopita ya ligi hiyo iliandikwa rekodi tamu na ya aina yake ya kushuhudiwa zikipigwa hat trick nyingi, kitu ambacho hakikuwahi kutokea zaidi ya misimu 20 iliyopita ya ligi hiyo ya Bara iliyoasisiwa mwaka 1965.

Katika msimu huo timu shiriki zikiwa 20 zilipigwa hat trick nane, huku ikishuhudiwa, Obrey Chirwa aliyekuwa Azam akipiga mara mbili akifikia rekodi za Amissi Tambwe na Emmanuel Okwi waliyoiweka nyuma. Mwanaspoti linakuletea hat trick 18 zilizopigwa ndani ya misimu minne ya Ligi Kuu Bara ikiwa moja ya msimu huu na utabiri unaoweza kutokea kwa mechi zilizosalia za kumalizia msimu kama kunaweza kufungwa nyingine au ndo hesabu zimeshafungwa!

MSIMU WA 2018-2019

Katika msimu huu ambao kila timu ilicheza jumla ya mechi 38, uliandika rekodi ya kufungwa hat trick nyingi baada ya misimu kadhaa kupita ikishuhudiwa hat trick chache zilifungwa katika Ligi Kuu Bara.

Msimu huu zilifungwa hat trick sita ambazo zilizinduliwa rasmi na Mrundi, Pascal Kitenge aliyekuwa akikipiga Chama la Wana, Stand United enzi hizo kabla ya kushuka daraja.

Mshambuliaji huyo alifunga kwenye pambano kali lililoisha kwa sare ya mabao 3-3 kati ya Chama la Wana na Yanga, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Baada ya Kitenge alifuata Emmanuel Okwi aliyekuwa Simba aliyetupia mabao matatu wakati timu yake ikiizamisha Ruvu Shooting kwa mabao 5-0 jijini Dar es Salaam kabla ya Salim Aiyee aliyekuwa Mwadui kutupia mabao matatu wakati Wachimba Almasi wa Mwadui kuizamisha Kagera Sugar kwa mabao 4-0.

Nahodha wa Ruvu Shooting, Fully Maganga naye hakubaki nyuma alitupia mabao matatu wakati timu yake ikiizamisha Mwadui kwa mabao 6-2 katika mechi iliyopigwa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani kabla ya Okwi kurudia tena kupiga hat trick wakati Simba ikiizamisha Coastal Union kwa mabao 8-1 jijini Dar es Salaam.

Mchezaji wa mwisho kukamilisha hat trick kwa msimu huo alikuwa ni Meddie Kagere pia wa Simba aliyefunga katika mechi hiyo ya Coastal na kumfanya amalize msimu huo uliokuwa wa kwanza kwake kama kinara wa mabao wa msimu akifunga mabao 23.

MSIMU WA 2019-2020

Katika msimu huu ambao timu shiriki zilikuwa 20 pia, ulioandika rekodi ya kupigwa hat trick nyingi (nane), huku Ditram Nchimbi aliyekuwa Polisi Tanzania kuwa wa kwanza katika pambano la kibabe la timu yake dhidi ya Yanga lililoisha kwa sare ya mabao 3-3.

Hat trick hiyo ndiye iliyompa ulaji mshambuliaji huyo kusajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la msimu huo na kujikuta akishindwa kutamba kabla ya kutemwa na kukimbilia Geita Gold ambako pia hana maajabu tena.

Daruwesh Saliboko enzi hizo akikipiga Lipuli alifuatia akipiga hat trick wakati timu yake ikiizamisha waliokuwa vibonde wa msimu Singida United kwa mabao 5-1 kabla ya Obrey Chirwa akiwa Azam kufunga hat trick wakati wakiizamisha Alliance kwa 5-0.

Naye Kelvin Sabato aliyekuwa Kagera Sugar naye alifunga hat trick dhidi ya Singida United walipoizamisha kwa mabao 3-0, kisha kufuatiwa na David Richard aliyekuwa akikipiga Alliance walipoizamisha Mwadui kwa mabao 4-1.

Meddie Kagere aliyekuwa akitetea kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora, alifunga hat trick yake wakati Simba ikiizamisha Singida United kwa mabao 8-0, yeye akitupia manne katika mechi ya upande mmja iliyopigwa Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji Atupele Green wakati huo akiwa Biashara United, alikuwa nyota wa saba kufunga hat trick msimu huo wakati timu yake ikiishindilia KMC kwa mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Karume, mjini Musoma, Mara kabla ya mchezaji huyo kuhama kwenda Kagera Sugar, kisha Geita na kurudi tena Biashara aliyopo sasa.

Chirwa alikamilisha hat trick za msimu huo, ikiwa ya pili kwake wakati Azam ikiizamisha Singida United kwa mabao 7-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex na mshambuliaji huyo kutoka Zambia alitupia kimiani mabao manne.

MSIMU ULIOPITA

Katika msimu uliopita uliokuwa na timu 18 na kufanya kila timu kucheza mechi 34 msimu mzima, hakukuwa na hat trick nyingi kama misimu miwili nyuma yake, kwani zilifungwa tatu, Adam Adam aliyekuwa JKT Tanzania ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga wakati timu yake ikiizamisha Mwadui mabao 6-1.

Baada ya uzinduzi huo kupitia mechi hiyo iliypopigwa Oktoiba 25, 2020 kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, mjini Mwadui mkoani Shinyanga, Nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ alifuata kwenye mechi baina ya timu yake na Coastal Union iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mabao 7-0, huku Coastal wakiwa wenyeji wakihamishia mechi zao jijini humo baada ya Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kufungiwa kwa muda na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kutokithi mahitaji. Mshambuliaji aliyehitimisha hat trick ya msimu huo alikuwa Juma Liuzio ‘Ndanda’ wa Mbeya City ali mhhnnnyefunga mara tatu wakati timu yake ikiizamisha Coastal Union kwa mabao 4-0 katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

UKAME ZAIDI

Msimu huu, timu zikiwa zimepungua na kufikia 16 tu, umeonekana kuwa na ukame zaidi wa hat trick kwani tangu Jeremiah Juma ‘JJ’ kutupia kwenye mchezo uliopigwa Novemba 27, mwaka jana wakati Tanzania Prisons ikiizamisha Namungo kwa mabao 3-1 haijafungwa tena hadi sasa.

Licha ya ligi kusaliwa na mechi 41 kabla ya kufungwa kwa msimu huu wa 2021-2022, kuna dalili ndogo ya kuongezeka kwa hat trick kutokana ligi ilivyo ngumu. Licha ya kuonekana timu nyingi zoefu za ligi hiyo kuyumba, lakini huwezi kuamini kuwa ndani ya msimu huu, hakuna timu iliyopata ushindi zaidi ya mabao manne kulinganisha na misimu mitatu iliyopita ambapo timu zilipigwa hadi mabao manane. Tusubiri tuone!

Columnist: Mwanaspoti