Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uhalali wa mshahara wa Aziz Ki dhidi ya Fei Toto

Aziz Ki Kwa Mkapa Uhalali wa mshahara wa Aziz Ki dhidi ya Fei Toto

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Limeanza kuwa gumzo kubwa kuhusu malipo ya mshahara wa mastaa wa kigeni dhidi ya mastaa wetu. Inaonekana mastaa wetu wanalipwa kiduchu kuliko mastaa wa kigeni. Yanga imeanza kukumbana na wimbi hilo kwa sasa.

Imeonekana kwamba staa wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ analipwa pesa kiduchu kuliko mastaa wa kigeni klabuni hapo huku wengi akiwa amewazidi kiwango na mchango mkubwa klabuni. Muda si mrefu Yanga wataingia katika tatizo jingine.

Inadaiwa kwamba mlinzi wao mwingine imara, Dickson Job naye anaweza kuingia katika mkumbo huo huo wa kutaka malipo makubwa kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa kigeni klabuni hapo. Nadhani klabu nyingi kubwa zitaingia katika matatizo na mastaa wao.

Kuna mambo mawili hapa. Kwanini mastaa wetu hawalipwi kiasi kikubwa cha pesa kuliko wageni? Jambo la kwanza ni ukweli kwamba wanakosa wasimamizi wazuri wakati wanapopinda mgongo kusaini mikataba ya awali au mikataba mipya katika klabu zao. Hili nimelizungumza mara nyingi.

Na hata watu wanaowasimamia wanakosa hoja za msingi za kuhalalisha malipo makubwa kwa mastaa wetu. Hawa wageni wana wawakilishi wazuri lakini pia wanajua kutengeneza wasifu wao kwa ajili ya kuhalalisha kiasi kikubwa cha mshahara.

Wachezaji wazawa huwa wanakurupuka kutaka malipo mazuri wakati msimu unaendelea. Kwa mfano, mchezaji akiwa anacheza vizuri kuliko wageni anahisi anadhulumiwa. Anasahau kwamba alikaa mezani na kujadili malipo yake ya mshahara.

Wenzetu huwa wanatengeneza uhalali wa malipo hayo wakati wa mazungumzo. Kitakachokuja kutokea uwanjani ni suala la kumuachia Mwenyezi Mungu. Na ni kweli. Wengine huwa wanafanya vizuri lakini wengine mambo yanakwenda kombo. Mbona hata kwa wazawa kuna wakati jambo hilo linatokea?

Turudi katika mfano halisi wa Azizi Ki dhidi ya Fei Toto. Wakala au Meneja wa Aziz Ki lazima alikuja na wasifu mzuri wa mchezaji wake. Na inawezekana pia anaweza kuwa Aziz Ki mwenyewe aliyetengeneza wasifu wake mzuri ambao unahalalisha malipo mazuri.

Aziz Ki alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita. Aziz Ki pia anacheza panga pangua katika kikosi cha timu ya taifa ya Burkina Faso. Itazame nafasi ya Burkina Faso katika viwango vya Fifa kisha itazame Taifa Stars. Wao wanashika nafasi ya 50 wakati Taifa Stars inashika nafasi ya 130.

Kiungo anayecheza katika kikosi cha timu ya taifa inayoshika nafasi ya 50 anaweza kupiga kelele dhidi ya kiungo anayecheza katika kikosi cha timu ya taifa inayoshika nafasi ya 130. Inategemea tu na ujanja wa wakala wake katika meza ya mazungumzo.

Lakini hapo hapo jiulize. Yanga walimuona wapi Fei Toto na walimuona wapi Aziz Ki? Yanga walimuona Feisal wakati anacheza klabu ya JKU ya Zanzibar. Wakampata kama hisani kutoka klabu ya Singida United ambayo mmiliki wake ni shabiki wa Yanga.

Lakini kumbuka kwamba Yanga walimuona Aziz Ki akiwa anacheza katika klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast na klabu hiyo ilikuwa inacheza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Nafasi ya kumpata Aziz ilipaswa kuwagharimu pesa nyingi na kumshawishi kiasi kikubwa cha mshahara kuwashinda wakubwa wengine ambao walikuwa wanawania saini yake.

Kifupi ni kwamba mazingira ya kumpata Aziz Ki yalikuwa magumu kwa Yanga kuliko kwa Fei Toto. Jambo hili linawafanya wachezaji wa kigeni kulipwa pesa nyingi wakati mwingine kuliko wazawa. Unaweza kumdharau Jesus Moloko lakini wakati Yanga wanapambana kuipata saini yake walikuwa pia wamejiongeza kutokana na wasifu wake.

Ndani ya msimu mchezo wa mpira unaweza kuleta viwango tofauti lakini wachezaji hawa wanajipatia mishahara tofauti kutokana na mazungumzo yao katika meza lakini pia wasifu wao ambao umewaleta katika klabu zao.

Sio rahisi sana kumpata mshambuliaji kama Moses Phiri ambaye unaweza kuiona ofa yake ya kutakiwa na klabu za Afrika Kusini wakati unawania saini yake. Ni tofauti na Yusuph Mhilu wakati unaiwania saini yake.

Ni kweli kwamba wanaweza kuingia uwanjani na Mhilu akafanikiwa kucheza vizuri zaidi klabuni. Hata hivyo wakati wanaingia klabuni walikuwa na wasifu tofauti. Wachezaji wa kizawa lazima wajue namna ya kutengeneza wasifu wao.

Mabosi wa hizi klabu huwa wanatishika na wasifu. Leo hata kama Simon Msuva au Mbwana Samatta wakirudi kucheza soka letu la ndani nadhani watakuwa wachezaji wanaolipwa zaidi kwa wachezaji wa ndani au hata wa nje. Wametengeneza wasifu wakubwa ambao unasomekana kirahisi kwa mabosi wetu wa soka.

Nadhani hata mabosi wetu wa soka kwa sasa hawafikirii kuwa na wachezaji kama Samatta au Msuva kwa sababu wanahisi hawawezi kuwamudu. Mfano ni wazi kwamba kwa sasa Samatta ana wasifu mkubwa kuliko Aziz Ki.

Kitu kingine ambacho kinaweza kusababisha wachezaji wetu wa ndani wapate malipo makubwa ni kuzipata mafanikio klabu hizi na kisha kutakiwa na klabu mbalimbali za nje. Kwa mfano, inawezekana Fei ana bahati tu kutakiwa na Azam au Simba. kama angekuwa hatakiwi na klabu yoyote kati ya hizo si ajabu Yanga wasingeteseka kutaka kumboreshea maslahi yake.

Nawakumbusha tu mchezaji kama Fiston Mayele alikuja nchini huku akiwa mfungaji bora namba mbili katika Ligi Kuu ya Congo. Lakini pia alikuwa katika kikosi cha AS Vita ambacho kilifika katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Unampata wapi mchezaji mwenye wasifu kama huo katika soka letu?

Wachezaji wetu wanapaswa kufanya mambo mawili. Kutafuta mawakala au mameneja wenye uwezo mkubwa wa mazungumzo ambao wataweza kujenga hoja za kuhalalisha malipo mazuri kwao. Lakini pia wanapaswa kujenga wasifu mkubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa mfano, bado naamini kwamba Aishi Manula anastahili kulipwa mshahara mkubwa kama ilivyo kwa makipa wengi wa ndani ya bara la Afrika. unampata wapi kipa mwenye wasifu kama yeye kwa urahisi? Rekodi yake na Simba katika soka la ndani na la kimataifa inajieleza wazi.

Columnist: Mwanaspoti