Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uhakiki kaya masikini uzingatie vigezo

C27d09494eca88117d57a664fdd24cdc Uhakiki kaya masikini uzingatie vigezo

Fri, 24 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HIVI karibuni Rais John Magufuli alizundua kipindi cha pili awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na kusimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Katika uzinduzi huo Rais Magufuli alisifu wazo la kuwepo kwa mpango huo lililoanza kutekelezwa mwaka 2000 na kwamba Maisha ya kaya nyingi yameboreka na wengi wameondoka kutoka umaskini wa kukithiri na kuwa na hali bora.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga,siku chache zilizopita wilayani Bariadi mkoani Simiyu, alifungua mafunzo kwa wawezeshaji na wakuu wa Idara ili kusaidia utekelezaji wa ufanisi wakati wa kusimamia uhakiki wa kaya masikini ili zitambulike na kuingia kwenye mpango wa kusaidiwa.

Katika rai yake aliwataka wasimamizi hao kuzingatia uadilifu na nidhamu ili kuhakikisha walengwa halisi ndio wanaingia kwenye mpango huo wa kuzinusuru kaya masikini na wasikubali kupindisha lengo na kuingiza wananchi wasio na sifa.

Jambo muhimu alilosisitza Mwamanga ni kuhakiki taarifa za wanufaika wa miradi hiyo na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu jambo hilo ili fursa hiyo itumike tu kwa wahitaji ili kupunguza umaskini wa kaya hizo na kuinua uchumi.

Kauli hiyo ni njema na inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kwa kushiriki na kutoa taarifa za watu wanaotumia fursa hiyo kujinufaisha, kwani wapo baadhi ya wachache wanaoweza kunufaika isivyo halali na hivyo kuwanyima wahitaji wa kweli fursa hiyo.

Tangu mwaka 2000 ulipoanzishwa mpango huo wa kuzinusuru kaya hizo zaidi ya shilingi trilioni 4.109 zimetumika katika awamu zote huku miradi 52,979 na kaya 2,500,000 zikinufaika. Baada ya kuanzishwa kwa mpango huo, awamu ya kwanza ilikuwa mwaka 2000-2005 na ulitumia Sh bilioni 72 katika halmashauri za wilaya 40 Tanzania Bara na 10 Zanzibar na miradi 1,704.

Awamu ya pili ilikuwa mwaka 2005-2013 na ilitumia Sh bilioni 430 katika halmashauri 126 Bara na 10 Zanzibar huku miradi 12,347 ilitekelezwa. Awamu ya Tatu kipindi cha kwanza kilianza mwaka 2013 hadi Desemba 2019 ikihusisha kaya milioni 1.1, miradi 8,928 katika halmashauri 159 Bara na 11 Zanzibar na Sh trilioni 1.5 zilitumika.

Awamu ya pili iliyozinduliwa mapema mwaka huu imeanza 2020 hadi 2023, ikilenga kutumia Sh trilioni 2.031 katika halmashauri 185 Bara na 11, Zanzibar huku kaya milioni 1.4 zikitarajiwa kufikiwa na miradi 30,000.

Miongoni mwa mafanikio katika utekelezaji huo ni kubuni miradi mbalimbali ikiwemo ya ufugaji ngómbe wa maziwa,mbuzi, kuku nguruwe miradi ya kilimo, biashara na miradi mingine iliyobadilisha Maisha ya wanakaya hao.

Aidha pia ajira na fursa za masomo zilipatikana ambapo wanafunzi walionufaika na Tasaf wakiwemo 277 walijiunga na vyuo vikuu mbalimbali jambo ambalo ni la kupongezwa na lenye tija kwa taifa.

Hayo ni baadhi tu na manufaa mengi ya Tasaf yanayopatikana kwa wanufaika, hivyo ni vyema basi kuendelea kusisitiza Pamoja na uzuri wa jambo lenyewe na faida inayoonekana, umakini na uhakiki wa kuzitambua kaya hizo uzingatie vigezo ili kuepusha kuachwa kwa wahitaji wa kweli.

Columnist: habarileo.co.tz