Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uchumi wa soko jamii unaweza kulinda uchumi wa kati Tanzania

Ad8dccade4ececd3c87691ae5ea56fef Uchumi wa soko jamii unaweza kulinda uchumi wa kati Tanzania

Tue, 21 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HIVI karibuni Benki ya Dunia (WB) imeorodhesha Tanzania chini ya Uongozi wa Rais John Magufuli kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati, ikiwa ni miaka mitano kabla ya malengo ya maendeleo ya taifa kufi kia kiwango hicho mwaka 2025.

Rais Magufuli anawapongeza Watanzania akisema: ‘’Huu ni ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya, tulipanga kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, lakini tumefanikiwa...’’

Rais Magufuli anasifiwa kimataifa kwa kupambana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa Tanzania hasa kwa kusisitiza ‘kuchapa kazi’ kwa juhudi na maarifa, kudhibiti matumizi na kukabiliana na ufujaji wa fedha sambamba na kuhimiza uadilifu katika utumishi, uongozi bora na usimamizi bora na wa kutosha wa rasilimali za nchi.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba anasema, ili nchi itangazwe kuwa ya uchumi wa kati, Benki ya Dunia hutazama pato la taifa kwa mfano, kupitia jumla ya utajiri wa rasilimali na ule wa kifedha na kugawanya na idadi ya watu wa Tanzania.

“Mataifa yenye kipato cha kati ya Dola 1,006 hadi Dola 3,955 kwa mtu mmoja, hutajwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati, lakini yaliyo na uchumi mdogo…” anasema.

MAANA YA UCHUMI WA KATI KWA TANZANIA

Wachambuzi wanasema kuingia kwa Tanzania katika uchumi wa kipato cha kati, ni ishara wazi kuwa Tanzania inaimarika kiuchumi.

“Hii ni ishara kuwa, siasa za Tanzania zinaenda sambamba na ukuaji wa uchumi wa taifa na sifa hiyo italisaidia taifa kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni itakayoimarisha zaidi kiuchumi,” anasema Kibamba.

Anaongeza: “Watanzania wanapaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi ili kuboresha uchumi.”

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abasi anasema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyoibua ajira kwa Watanzania wengi ni kati ya vitu vilivyoivutia Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kufikia hatua hiyo.

Anasema takwimu za kipato cha waliopata ajira ni miongoni mwa maeneo yaliyochukuliwa na benki hiyo kuthibitisha kwamba, pato la Watanzania limeongezeka, pamoja na ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji wa megawati 2500 kama mojawapo ya mambo yaliyosababisha kuimarika kwa uchumi wa taifa hilo.

Mradi huo umeibua zaidi ya ajira 3500. Tanzania inafika katika uchumi wa kati ikiwa imepitia katika maboresho mbalimbali ya kiuchumi tangu ipate uhuru ikiwamo kuanzishwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967 lililolenga kuweka uchumi mikononi mwa umma na pia, imepitia katika hali ya soko huria.

Kitabu kiitwacho: ‘Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii Kwa Tanzania; Kuelekea Maendeleo ya Uchumi Jumuishi na Endelevu” cha Machi 2019 kinasema, Azimio la Arusha lililenga kuleta matumaini ya usawa, umma kumiliki na kuendesha njia za uzalishaji mali huku lengo kuu likiwa ni kufikisha mahitaji na huduma za jamii katika maeneo ya vijijini kwa urahisi zaidi.

Kitabu hicho kiliandaliwa kwa msaada wa shirika la Konrad- Adenauer- Stiftung kikihusisha wataalamu wa uchumi na wasomi mbalimbali nchini akiwamo Profesa wa Uchumi; Mtafiti na Mshauri wa Uchumi na Biashara katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi.

Wengine miongoni mwa waandalizi ni Dk Pd Charles Kitima ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo mstaafu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT) na sasa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Ntui Pontian ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika SAUT na Mwezeshaji wa mafunzo ya biashara yanayojumuisha Uhasibu wa Fedha, Utoaji wa Taarifa za Fedha, Usimamizi wa Fedha na Usimamizi wa Fedha Kimataifa.

Kinasema popote duniani, mfumo wa uchumi wa soko huria una hatari ya kusababisha ongezeko la umaskini kwa kuwa siyo jumuishi kwa watu wote hivyo, unaweza kusababisha watu wachache au kampuni chache kunyonyonya wengine kupitia namna wanavyoendesha biashara zao.

Wataalamu na wasomi hao na wenzao wameandika katika kitabu hicho: “Lengo la soko huria lilikuwa kuleta bei halisia ya soko na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa.”

Kinaongeza: “Mabadiliko hayo yalikuwa ya lazima kwa mazingira ya wakati huo. Jitihada nyingi zimefanyika kuinua hali ya maisha ya Watanzania.”

Kimsingi, licha ya juhudi nyingi kufanywa hadi kufikia mwaka 2015, bado watu wengi walikuwa maskini na rasilimali za nchi zilikuwa zinaendelea kupungua na kufaidiwa na wachache wakiwamo wa ndani na nje ya nchi; uzalishaji katika sekta binafsi kwa kiasi kikubwa ulikuwa unamilikiwa na kampuni za nje ya nchi na siyo wazawa.

Hata palipoelezwa kuwa na ukuaji wa uchumi, ukuaji huo haukuakisi maendeleo ya uchumi wa nchi. Baadhi ya Watanzania waliendelea kuishi kwa kukosa uhakika wa kupata walau mlo mmoja kwa siku huku wengine wakishindwa kupata, kufikia na kumudu gharama za matibabu na huduma nyingine za afya.

Baada ya mwaka 2015, Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kukuza uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja na juhudi za serikali bado zinaendelea ikiwa ni pamoja na kufuta mikataba yote michafu iliyoruhusu rasilimali za nchi kama madini ‘kuhamishiwa’ nje ya nchi na Watanzania kubaki na mashimo au mahandaki na kutilia mkazo uanzishaji na uendeshaji viwanda vya ndani ili kuongeza thamani ya bidhaa na mazao ya shambani au viwandani.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeondoa utitiri wa kodi na ushuru uliokuwa kero kwa wazalishaji wakiwamo wakulima na wafanyabiashara nchini na mianya mingi ya biashara imefunguliwa ikiwamo ya kuhakikisha wafanyabiashara wadogo (wamachinga) wasio na maeneo maalumu na wasio katika mfumo rasmi wa kodi wanapewa vitambulisho wanavyovipata kwa kuchangia Sh 20,000 ili watambulike, waheshimike na kufanya biashara zao mahali popote nchini bila bugudha.

Hii kimsingi, inalenga kuufanya uchumi wa nchi uwe mikononi mwa wananchi wengi (wote) na ukue zaidi kwa faida ya wote. Juhudi hizi za serikali zimeifikisha Tanzania katika uchumi wa kati (chini) kabla ya wakati uliokusudiwa yaani mwaka 2025.

Serikali inastahili pongezi za dhati kwani ukiona vinaendelea, ujue vimeundwa. Kinasema; “Inaaminika kuwa Uchumi wa Soko Jamii ni muhimu kwa ufanisi wa uchumi ulio imara.”

Kimsingi, katika suala la uchumi, ipo mifumo mikuu miwili inayotofautiana ambayo ni Uchumi wa Soko Huria (Ubapari) na Uchumi unaomilikiwa na kusimamiwa na serikali (Ujamaa). Hata hivyo, upo mfumo mwingine uitwao Mfumo wa Uchumi Mseto unaochukua baadhi ya tabia za uchumi wa soko huria na baadhi ya tabia za uchumi unaomilikiwa na kusimamiwa na serikali.

MFUMO WA UCHUMI WA KIJAMAA

Katika semina kwa wanahabari hivi karibuni iliyofanyika Kurasini Dar es Salaam mintarafu mfumo wa uchumi wa soko jamii, Ntui katika mada yake anasema: “Katika mfumo huu, mambo yote yanapangwa na serikali kuu na kuratibiwa kupitia mpango wa kitaifa wa uchumi na hakuna uhuru wa kufanya shughuli za uchumi kwa watu binafsi au vikundi.”

Anaongeza: “Uzalishaji na umiliki wa mali lazima uwe mikononi mwa vikundi halali chini ya umma. Hapa, sekta binafsi na ubunifu huwa dhaifu na ufanisi huwa wa kiwango cha chini.”

MFUMO WA UCHUMI WA SOKO HURIA (UBEPARI)

Kitabu kiitwacho “Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii Kwa Tanzania; Kuelekea Maendeleo ya Uchumi Jumuishi na Endelevu” kinaandika: “Mambo ni tofauti na mfumo wa kiserikali ambapo shughuli nyingi za kiuchumi huwa mikononi mwa watu binafsi au kikundi binafsi na huratibiwa tu na bei za bidhaa na huduma sokoni.”

Kinaongeza: “Katika mfumo huu, ugatuaji wa madaraka wa kupanga na kuratibu huachwa mikononi mwa soko ambapo upatikanaji ama upungufu wa bidhaa na huduma unatokana na bei za bidhaa au huduma.”

Hapa ifahamike kuwa, upungufu wa bidhaa au huduma (mahitaji mengi kuliko uzalishaji na upatikanaji) husababisha bei kupanda na upatikanaji au uzalishaji wa bidhaa au huduma huduma hizo kwa wingi kuliko mahitaji, husababisha bei kushuka.

UCHUMI WA SOKO JAMII

Dk Kitima anasema: “Huu ni mfumo unaounganisha uchumi wa soko huria pamoja na jukumu la serikali katika kudhibiti hali ili haki itendeke kwa wote na kuleta ushindani unaofaa, kudhibiti hali ya ukuaji wa uchumi, kupunguza mfumuko wa bei, kupunguza upungufu wa ajira, kuboresha hali ya mazingira ya kazi na kuleta ustawi wa jamii kwa jumla.”

Akitumia chapisho hilo, Dk Kitima anasema katika mazungumzo na wanahabari hivi karibuni: “Mfumo huu unalenga kutengeneza uwiano kati ya uchumi wa soko huria na usimamizi wa serikali kwa kiasi kinachofaa ili kuleta maendeleo.”

Anasema mfumo wa uchumi wa soko jamii ukieleweka na kupokewa, utachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwani kila mmoja kwa nafasi yake atazalisha kupitia ujenzi wa mnyororo wa thamani wa mazao ya shambani na viwandani hali itakayoongeza ajira kwa watu na ongezeko la kipato kwa taifa kwa kuwa, badala ya Watanzania kuuza malighafi nje ya nchi na watauza bidhaa itokanayo na malighafi hiyo kwa bei ya tija.

Kwa mujibu wa uchunguzi, hali hii itasaidia kulinda uchumi wa kati Tanzania huku ukielekezwa katika uchumi wa kati wa juu kutoka wa chini. Kwa mujibu wa msomi huyo ambaye ni kasisi wa Kanisa Katoliki, tofauti na mifumo mingine ya uchumi, Mfumo wa Uchumi Soko Jamii ni jumuishi kwa watu wote na unaruhusu watu wote kushiriki na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao ikiwa ni pamoja na kulipa kodi zote halali.

Kimsingi, kuingia na kufanikiwa kwa mfumo huu unaotanguliza utu wa mwanadamu kutategemea namna watekelezaji watakavyouelewa na kuuhusianisha na shughuli za kibiashara katika ngazi zote tangu vijiji, wilaya, mikoan, taifa na kimataifa. Kwa mujibu wa chapisho hilo, maadili yanaweka msingi kwa washiriki wote katika uchumi na maendeleo ili kuhakikisha maamuzi yao na kile wanachofanya kinakuwa na mwongozo.

Columnist: habarileo.co.tz