Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uchumi Utashi wa kisiasa utaokoa mazingira na kuondoa umasikini

E85128b24dd7b272a9f7dd67c64d5885 Uchumi Utashi wa kisiasa utaokoa mazingira na kuondoa umasikini

Wed, 27 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA miaka ya karibuni uhusiano kati ya umasikini na uharibifu wa mazingira umeanza kueleweka vizuri.

Mathalani, uharibifu wa mazingira husababisha umasikini kwa kupunguza upatikanaji wa maji safi, rutuba katika udongo, mazao na huduma nyingine muhimu kwa afya na maisha ya binadamu.

Aidha umasikini nao husababisha uharibifu wa mazingira kwa kudhoofisha juhudi na uwezo wa binadamu kusimamia na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.

Ripoti ya utafiti wa jarida la matibabu la Lancet inaonesha gharama kubwa zinazotokana na vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, magonjwa na ustawi, na kukadiria gharama hizo zinafikia dola bilioni 4.6 katika hasara za kila mwaka au sawa na asilimia 6.2 ya uchumi wa dunia.

“Kile ambacho watu hawatambui ni kwamba uchafuzi wa mazingira unaathiri uchumi. Watu ambao ni wagonjwa au wafu hawawezi kuchangia katika uchumi, wanahitaji kutunzwa,” anasema Richard Fuller, mmoja wa waandishi wa utafiti na mkuu wa shirika la kimataifa linalochunguza masuala ya uchafuzi wa mazingira la Pure Earth.

Kulingana na utafiti huo, mzigo wa kifedha pia unaathiri nchi masikini zaidi, na nchi za kipato cha chini zikitoa asilimia 8.3 ya Jumla ya Pato la Taifa (GNP) ili kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, ikilinganishwa na asilimia 4.5 katika nchi tajiri.

Hapo awali suala la mazingira halikupewa kabisa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya uchumi na kuondoa umasikini. Lakini hivi sasa uelewa wa jamii umeanza kuongezeka na kupewa kipaumbele katika kuandaa mipango ya maendeleo.

Tunao Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta) unaotambua kuwa mazingira bora ni msingi wa maendeleo endelevu na kupunguza umasikini, kama ulivyoainisha malengo 15 yanayohusu mazingira.

Mikakati thabiti ya uhifadhi wa mazingira ilianza wakati wa uongozi wa Awamu ya Nne, chini ya Jakaya Kikwete, baada ya kulifanya suala la mazingira kuwa miongoni mwa mambo 10 muhimu ya kushughulikiwa na serikali.

Mchakato wa kujumuisha mazingira katika Mkukuta ulihusisha ukusanyaji wa maoni, mawazo, mifano na kuwakutanisha viongozi mbalimbali, hali iliyosaidia kukua kwa ufahamu miongoni mwa watoa maamuzi.

Hii ilitokana na Sera ya Taifa ya Mazingira ya 1997 ambayo imeainisha changamoto sita: uharibifu wa ardhi; uharibifu wa misitu; kupotea kwa makazi ya viumbe-pori na bioanuai; kukosekana kwa maji salama mjini na vijijini; kupungua kwa ubora wa mifumo ya maji; na uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya mijini.

Changamoto hizi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa ukuaji wa uchumi na juhudi za serikali katika kupunguza umasikini, na hivyo kuathiri maisha na ustawi wa jamii.

Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pia imeeleza wazi wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali kuanzia serikali za mitaa hadi taifa. Hata hivyo, kuna tatizo mahali kuhusu njia tunazochukua katika kukabiliana na changamoto hizi.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2019 tukashuhudia nchi yetu ikichukua hatua ya dhati katika uhifadhi wa mazingira, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza marufuku ya kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa.

Waziri Mkuu alitoa kauli bungeni jijini Dodoma, mnamo Aprili 9, 2019 kwenye mkutano wa 15, wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alisema matumizi ya plastiki nchini yameleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka.

Kilio kuhusu madhara yatokanayo na mifuko ya plastiki kilikuwa cha muda mrefu sana kwani inajulikana wazi kuwa mifuko hiyo ni moja ya vyanzo vikubwa vya uchafuzi wa mazingira duniani, na harakati za kukomesha matumizi yake zimelenga kulinda mazingira.

Pia katika kutekeleza jukumu hili, Ofisi ya Makamu wa Rais ikatekeleza mipango na programu kadhaa ikiwemo ile ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira, Sheria ya Mazingira na Kanuni zake.

Kwa mfano, kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Act) serikali imetunga kanuni za mwaka 2019 za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, ili kulinda mazingira.

Utekelezaji wa majukumu hayo ulitokana na hotuba ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba aliyowasilisha bungeni kuhusu makadilio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018, na kusema uchumi wa nchi yetu na maisha ya Watanzania yanategemea kwa kiasi kikubwa maliasili tulizonazo kama vile ardhi, maji, misitu na hewa safi.

Alisema uwepo wa maliasili hizi kwa mahitaji yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo hutegemea namna tunavyozingatia uhifadhi wake na matumizi endelevu.

Hata hivyo, utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki ukatuacha midomo wazi baada ya kauli kutoka kwa mwanasheria wa Baraza la kitaifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Heche Suguti aliposema kuwa kilichopigwa marufuku ni ile mifuko ya plastiki tunayobebea mizigo na kwamba vifungashio vimesamehewa.

Baadaye siku hiyo hiyo Waziri Makamba akasema kuwa vifungashio kama vile vya maji (maarufu maji ya Kandoro), karanga na ice cream na hata korosho n.k. navyo vimepigwa marufuku.

Lakini cha ajabu hatukuambiwa mbadala wa vifungashio hivi ni nini. Na hapo ndipo tulipoanza kuona kuna tatizo sehemu katika utekelezaji wa mpango huo. Matokeo yake hadi leo vifungashio hivyo vipo mtaani na vinazidi kuenea na kuchafua mazingira, huku wahusika wakishindwa kulitolea ufafanuzi jambo hili.

Mwaka jana, NEMC kupitia Mkurugenzi Mkuu, Dk Samuel Gwamaka waliweka kuwa hadi mwishoni mwa Disemba mwaka huo kuwa mwisho ya utumiaji wa vifungashio vya chupa za maji, karanga au ubuyu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk Gwamaka alisema kuwa limekuwako ongezeko la uzalishaji wa vifungashio vya plastiki ambavyo chanzo chake hakijulikani na ni vifungashio ambavyo havina kibali cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Alisema utengenezaji, usambazani na matumizi ya vitu hivyo ni uvunjaji wa Kanuni ya 3 na 4 za Sheria ya Mazingira ya 2004, kanuni ambazo zilitungwa na kutangazwa 2019 ili kutekeleza katazo la serikali la matumizi ya plastiki.

Kanuni namba 3 inawataka wazalishaji kuwa na kibali kutoka TBS baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, lakini hali haiko hivyo kwa sasa. Dk Gwamaka akaongeza kwamba kuwapo kwa vifungashio hivyo sokoni ni kinyume cha kanuni ya 4 (b) ambayo imetungwa na kutangazwa ili kulinda afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa kanuni za upigaji marufuku mifuko ya plastiki, ni marufuku kutengeneza, kuuza, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Dk. Gwamaka anasisitiza kuwa Baraza lazima lisimamie sheria na kuzuia matumizi ya bidhaa zisizoruhusiwa kisheria nchini humo.

Lakini pamoja na katazo hilo bado tunaendelea kushuhudia vifungashio hivi vikizagaa mtaani, na hatujui hatma yake ni nini.

Kwa mtazamo wangu, kiini kikubwa cha yote haya ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa. Makatazo kama haya yanashindikana kwa kukosa uungwaji mkono na viongozi wa kisiasa ambao husababisha mabadiliko ya kisera.

Juni 5, 2018 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliwataka wanasiasa nchini kuwa na utashi katika kuelimisha na kuhamasisha jamii katika uhifadhi wa mazingira.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau mbalimbali kusimamia sera na sheria pamoja na mikakati mbalimbali iliyowekwa katika kusimamia uhifadhi wa mazingira, lengo likiwa ni kukabiliana na athari zitokanazo na mazingira.

Kwa muda mrefu kumekuwepo ripoti mbalimbali zikionesha au kuashiria uwepo wa uharibifu mkubwa wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu ya maliasili zetu.

Ripoti maalumu ya tathmini ya rasilimali za misitu ya mwaka 2015 (National Forestry Resources Monitoring and Assessment Report, 2015) inaonesha kwamba uhitaji wa miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini kama kuni na mkaa unazidi kiwango cha miti inayoweza kuvunwa katika kiwango endelevu kwa mwaka.

Uhitaji wa miti ni mita za ujazo milioni 62.3 huku idadi ya miti (au kuni) inayofaa kuvunwa kwa kiwango endelevu ikiwa ni mita za ujazo milioni 42.8 tu.

0685 666964 au [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz