Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uchambuzi wa Yanga, Club Africain uliishia Kariakoo

Tuisila TK Tuisila Kisinda akimtoka mlinzi wa Club Africain

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Celtic na Rangers au Glasgow Rangers kama tunavyoitambua huku duniani ni wababe wa soka nchini Scotland kwa miaka mingi. Imefikia wakati soka la Scotland haliwezi kutajwa bila ya majina ya wababe hao.

Kutokana na ubabe wao, kuna wakati ilipendekezwa kwamba vigogo hao wawili wahamie kucheza Ligi Kuu ya England kama ilivyo kwa Cardiff na Swansea City zinazotokea Wales kwa kuwa hakukuwa tena na mpinzani nje yao katika kinyang’anyiro cha ubingwa wa Scotland.

Hata hivyo, wazo hilo hadi sasa halijatekelezwa na kwa sasa mshawasha huo umepoa kutokana na jinsi mabadiliko yanavyozidi kufanywa katika mifumo ya mashindano barani Ulaya.

Ndugu hawa wawili wamelingana kwa mafanikio ya ndani wakiwa wamegawana ubingwa takriban sawa kwa sawa, lakini inapofikia michuano ya kimataifa tofauti yao ni ndogo sana. Wamefanikiwa sana kwenye michuano ya Kombe la Ulaya na la Washindi, ambalo siku hizi linaitwa Europa League.

Na mafanikio ya hivi karibuni ya Celtic ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, ilipoishia kwa kutandikwa mabao 5-1 na Real Madrid katikati ya wiki iliyopita, Rangers nayo ilikumbana na vipigo katika Kundi A ilikopangwa na Liverpool, Napoli na Ajax Amsterdam.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa vigogo hao wa Scotland kufika hatua ya makundi tangu mwaka 2007, ingawa mwaka 2011 Celtic ilipewa nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Europa League baada ya mpinzani wake katika mtoano, Sion ya Uswisi kubainika kutumia wachezaji ambao kikanuni hawakuwa halali.

Kwa maana nyingine wawili hao hawachekani inapofikia michuano ya kimataifa na huoni kejeli za vyombo vya habari kuhusu kuboronga kwao Ulaya. Wanajua iko siku, lakini kwa sasa wameshindwa kuvutia uwekezaji mzuri kiasi kwamba inakuwa vigumu kushindana na klabu kama za England, Hispania, Italia na Ujerumani.

Na uchambuzi kuhusu mwenendo wao Ulaya hauangalii nani amefanya nini zaidi ya mwenzake, zaidi ya kujikita katika sababu za kiufundi na kimfumo wa umiliki. Kwa ujumla soka la Scotland halijaweza kuvutia wengi na halijatangazwa sana kiasi kwamba ni timu chache ndio zinaweza kuwa akilini mwa watu walio nje ya nchi hiyo, ukitilia maanani kuwa Sir Alex Ferguson alitokea Aberdeen kabla ya kujiunga Manchester United.

Hivyo kiwango cha Rangers na Celtic hakiwezi kupimwa kwa kuangalia moja ya timu hizo na kufikia majumuisho kwamba klabu moja ikubali mafanikio ya mwingine na ‘iige’ mafanikio hayo kwa kuwa hazijafikia hatua ambayo mmoja kamzidi mwingine kimafanikio.

Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni hatua ambayo Yanga na Simba zimeshafikia, ingawa Simba amefikia mara nyingi katika miaka ya karibuni. Kama ukomo umekuwa ni hatua ya makundi, basi hatuna budi kuanza kutafuta mfano mwingine wa kuigwa, yaani mafanikio kama ya timu za Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Nigeria ambako klabu zake zimepambana sana kuondoa ubabe wa timu za Ukanda wa Kaskazini maarufu kama Waarabu kutwaa vikombe vya Afrika. Nje ya nchi hizo tatu ni Gor Mahia pekee ambayo imepata mafanikio dhidi ya Waarabu ilipotwaa Kombe la Washindi mwaka 1987, ikiwa ni baada ya kufika fainali mwaka 1979.

Hawa ndio mifano wa kuigwa kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa wamekuwa wenyeji kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na wameshatwaa angalau kombe moja la Afrika.

Kwa hiyo nilikuwa nashangaa wiki iliyopita kwa watu mbalimbali kuacha kuchambua mazuri na mabaya ya mechi ya mtoano kuamua timu zitakazoingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kujikita zaidi katika kile kinachoonekana ni ushabiki, au kutaka kukubalika kwa kundi fulani la watu.

Inashangaza mtu kukaa nyuma ya mic na kushauri kwamba; “Yanga haina budi kukubali kuwa Simba ni level nyingine!”

Swali linalokuja haraka sana baada ya ushauri huo ni “ili iweje?” Sijui Yanga itafanyiaje kazi ushauri kama huu hata ikikubali kwamba “Simba ni level nyingine”.

Wapo walioshauri kwamba ‘Yanga haina budi kuiiga Simba’. Swali linalokuja haraka sana ni ‘kuiga nini?’ Na wako walioshauri kuwa ‘Yanga ikubali tu haina lolote michuano ya kimataifa‚‘ Swali linalofuata ni ‘kwa hiyo?’

Nilidhani uchambuzi ungeishia katika masuala ya kiufundi yaliyojitokeza katika mechi hiyo dhidi ya Club Africain ya Tunisia kwa kuangalia mbinu za wageni, uzoefu wao, uzuri wao na udhaifu ambao Yanga wanaweza kuutumia kuvuka hatua ya mtoano. Ni vigumu kwa timu ambayo inajiandaa kwa mechi ya marudiano ambayo inaweza kuwapa nafasi ya kusonga mbele, kusikiliza ushauri kama huo nilioutaja hapo awali. Ushauri huo unamaanisha mechi zote mbili zishaisha na sasa Yanga inatakiwa ijipange upya.

Wapo waliojaribu kujikita katika uchambuzi wa kiufundi, lakini nikashangaa mmoja anasema kuwa zaidi ya wachezaji wanane hawakucheza kwa kiwango chao, hivyo ingekuwa vigumu kufanya mabadiliko ambayo yanahusisha wachezaji watano tu.

Sijui kama alijua mbinu za kocha na mfumo wake, kiasi kwamba eneo moja likiharibika linaweza kusababisha sehemu kubwa ya mfumo isifanye kazi vizuri. Kama tairi moja ya gari limepata pancha, ni vigumu matairi mengine yote kufanya kazi kwa ufanisi. Na huhitaji kubadilisha matairi mengine yote kwa sababu moja linasababisha mengine yasifanye kazi vizuri. Yaani unatoa tairi linalovuruga mfumo na kuweka lenye upepo na gari linaendelea.

Mtu angejua tatizo la mfumo wa Yanga lilikuwa wapi, ni rahisi kusema mabadiliko yangefanywa sehemu hiyo na mfumo ungeendelea kufanya kazi kama kawaida.

Hivyo uchambuzi wa mechi ya Yanga na Club Africain ulifikia hatua ya kupoteza madhumuni au malengo ya kuchambua. Wako waliotulia hivi sasa wakisubiri matokeo mabaya halafu waseme ‘Nilisema!’ Huo ni ubashiri na si uchambuzi.

Ubabe wa Simba na Yanga usitufanye akili zetu zigote hapohapo, ni lazima tuangalie mbali zaidi. Hatua ya makundi ishakuwa ya kawaida kwenye Ligi ya Mabingwa na hata Kombe la Shirikisho ambako Yanga, Simba na Namungo wameshafikia. Mafanikio yatakuwa kuvuka hatua hiyo ndipo na zaidi kutwaa kombe, hapo ndipo tutasema ‘tumuige fulani’ kwa kuwa ameshavuka ukomo wetu.

Simba na Yanga bado zinahitaji kusukumwa mbele zaidi ya hapo zilipo. Ubabe wao ni sawa na ule wa Celtic na Rangers ambazo, angalau zimeonja makombe ya Ulaya miaka hiyo, lakini hazijaweza kufanya vizuri katika michuano mikubwa, hasa ya Ligi ya Mabingwa licha ya ukongwe wao. Akili zikigota katika klabu hizo mbili, basi hatujui tafsiri ya mafanikio.

Columnist: Mwanaspoti