Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uchaguzi umekwisha, nchi yetu iko kwenye mwelekeo sahihi

21cb28e3ae9210ccc5b3d47de6b81ded Uchaguzi umekwisha, nchi yetu iko kwenye mwelekeo sahihi

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HAPA nyumbani Uchaguzi Mkuu umeshafanyika. Dk John Magufuli anatarajiwa kuapishwa Alhamisi hii. Anatarajiwa na umma wa Watanzania kuwa atafanya makubwa zaidi kwenye miaka mingine mitano ijayo.

Maana Watanzania wamejionea kwa macho yao, mabadiliko makubwa ya kimfumo yaliyotokea kwenye nchi yao. Ni mabadiliko yaliyoleta maendeleo ya haraka ikiwamo ukarabati na ujenzi mpya wa miundombinu ikiwamo barabara na reli.

Ndani ya miaka hii mitano iliyopita, kumekuwepo pia na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama vile ufufuaji wa kampuni yetu ya ndege, ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya usambazaji maji vijijini na hata umeme vijijini.

Bila shaka yoyote Rais wa Awamu ya Tano, Dk Magufuli amesimama upande wa walio wengi na anaonekana kuwa anakerwa sana na rushwa na ufisadi.

Maana haijapata kutokea kwa miaka mingi, Rais mwenyewe akawatumbua watendaji wake hata walio waandamizi mara anapobaini kupitia vyombo vyake, kuwa wameingia kwenye kashfa za kula rushwa na ufisadi.

Ni ukweli rushwa na ufisadi ni kero nambari moja, ambayo umma umeifanya kuwa ajenda ya uchaguzi kwa miaka ya nyuma. Rais waliyemtaka Watanzania walitaka amaanishe kwa vitendo kuwa yuko tayari kupambana na rushwa na ufisadi.

Na hakika Rais Magufuli amefanya hivyo tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani. Na kwa kauli na matendo ya Rais Magufuli, umma wa Watanzania umekuwa nyuma yake katika kumuunga mkono kwenye kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi.

Ajenda hii ya kupambana na rushwa na ufisadi, wakati huo huo serikali kuboresha na kujenga miundo mbinu na kusimamia mpango wa Elimu Bure na mengineyo, ndiyo masuala yaliyochangia kuufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa mwepesi zaidi kwa mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Magufuli na chama chake, CCM.

Ni kwa sababu chini ya Uenyekiti wake, Magufuli ameonesha kusimamia nidhamu na maadili ya viongozi ndani ya chama chake. Na tuwe wakweli, Magufuli amefanya vema sana kwenye uongozi wake kwa kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita.

Ameonesha kuwa anaaminisha anaposema anachukia rushwa na ufisadi. Tunaona hata serikalini, watendaji wasio waadilifu wanaishi kwa mashaka.

Na kwa anavyojitahidi kuwamulika watendaji wengine wenye kuhusishwa na rushwa na ufisadi, imesaidia sana kwenye kuleta nafuu ya maisha kwa wanyonge walio wengi.

Na haya aliyokuja nayo Magufuli kwenye Awamu hii ya Tano, yatabaki kuwa ni mapinduzi makubwa kimfumo yatakayobaki katika historia ya kukua kwa nchi yetu kwa karne nyingi zijazo.

Na kuna waliotutangulia kufanya mapinduzi ya kimfumo na wamefanikiwa. Tuone mfano wa nchi ya Singapore. Imeandikwa kuwa Singapore, ‘chunusi kwenye uso wa Malaysia’ , ina eneo dogo sana (kilomita mraba 646 sawa na eneo la Jiji la Chicago , Amerika).

Idadi ya watu haifikii milioni tano, ambao wamejigawa ki-uzawa; yaani, wa-Hindi, wa-Malay na wa-China. Zaidi wamejigawa ki-dini; yaani, wa-Islamu na wa Budha.

Masuala ya siasa, ubaguzi wa rangi au dini hayaruhusiwi kuwa viini vinavyozungumziwa na wasanii. Kisiwa cha Singapore kilianza kama kijiji cha wavuvi wachache.

Kilijaa mabwawa ya mbu wengi wenye kueneza ugonjwa wa malaria. Bandari na madhari ya ufukwe wake kulijaa mitumbwi .

Walevi wa madawa ya ‘opium’walijaa kwenye sehemu walikoishi jamii ya wa-China, ambao walikuwa wakichungulia madirishani na huku wamewaka chakari, wacheza kamari na kusheheni biashara ya u-malaya (changudoa).

Baadae Singapore iliamua kujijenga ili kujikomboa kutoka madhambi, majuto na mavune ya miaka mingi kabla ya 1960. Ilipiga marufuku makasino, kamari na kuongeza kodi kwa tumbaku, na vinywaji vikali na kudhibiti biashara ya madawa ya kulevya.

Ili kudhibiti umaskini na mazoea yasiyo ya maadili mema, serikali ililivalia njuga suala la kupambana na rushwa na ufisadi ili ifanikiwe kupunguza umasikini.

Singapore ilianza kufyeka na kujenga upya bandari na madhari yake. Leo hii, Singapore ni bandari-ghala (entrêport) kubwa kwa nchi zote za Australia, New Zealand na Asia Mashariki ya Mbali.

Biashara ya huko ni kubwa sana. Waziri Mkuu Awamu ya Tatu, Lee Hsien Loong alipanua mianya ya biashara. Alitaka Singapore kuingiza mapato zaidi.

Aliruhusu watalii na kuzidisha biashara kwa ajili ya kujenga tabaka la kati bila upendeleo. Singapore ikatajirika kushinda nchi nyinginezo za Asia.

Shirika la Ndege (Singapore Airlines) linaongoza duniani kwa sifa za juu. Kiasi cha asilimia 90 ya wananchi wa Singapore wanaishi majumbani mwao na biashara inasheheni bila urasimu, ufisadi na rushwa.

Singapore inasifika kwa uwazi na utawala bora huku ikishindana kila mara kuwa ya kwanza; ilikataa kuwa namba mbili. Kuna majengo marefu na alama za utajiri.

Mji ni msafi sana – hakuna uchafu wa mazingira. Bandari yake leo hii inag’aa kwa biashara Elimu ni ya kiwango cha juu na wengi wameelimika hadi chuo kikuu na wengi wamehitimu elimu kazi/ajira kupitia vyuo vya ufundi mbalimbali.

Wanatumia ‘intaneti’ ya spidi kali (broadband), kuna uhuru wa biashara na serikali inapendelea wawekezaji. Kuna uwazi wa hali ya juu katika fani za kazi na biashara na hakuna ufisadi na rushwa.

Kuna utawala bora, hakuna upendeleo kazini – wafanyakazi wanaajiriliwa na kupandishwa vyeo kulingana na sifa zao za ujuzi na ufanisi. Wafanyaazi wa umma wanalipwa sawa na wale wa sekta binafsi.

Nionavyo, na sisi Watanzania chini ya Rais Magufuli tunaweza kufika mbali, kwa vile Rais wetu wa Awamu ya Tano anamaanisha kwa vitendo kuwa anachukia rushwa na ufisadi.

Columnist: habarileo.co.tz