Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ubinafsi unavyokwaza muungano wa upinzani

Ukawa Ubinafsi unavyokwaza muungano wa upinzani

Wed, 24 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KWA zaidi ya muongo mmoja sasa, suala la vyama vya wapinzani kuunganisha nguvu ili kuviondoa vilivyopo madarakani hasa barani Afrika limekuwa la kipaumbele, lakini pasipo kuwa na mafanikio endelevu.

Kadhalika hapa nchini, muungano kama huo si jambo geni. Ulijitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wakati vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vilipounganisha nguvu zao kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Uchambuzi unaofanywa katika siasa za mataifa kadhaa, unadhihirisha kuwapo kasoro mbalimbali zinazovikwamisha vyama hivyo kuwa imara na kuziondoa madarakani serikali za Hali kama hiyo ipo Tanzania, ambapo tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na baadaye uchaguzi mkuu wa kwanza uliovishirikisha vyama hivyo mwaka 1995, hisia za wapinzani kuunganisha nguvu zao zilitokea. Lakini hawakufanikiwa.

Ndiyo maana haikushuhudia ukiungana mwaka 1995 wakati aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu (pamoja na nyadhifa nyingine), Augustine Mrema alitoa ushindani mkubwa katika uchaguzi huo.

Akiwania kupitia chama chga NCCR-Mageuzi, Mrema alipata kura 1,808,516 sawa na asilimia 27.77 nyuma ya aliyeongoza, Benjamin Mkapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82 na wagombea wengine walipata chini hapo.

Mrema alizichukulia kura hizo kama mtaji wa kuingia nao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, lakini hali ikawa tofauti na matarajio yake, akaambulia kushuka na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Mkapa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.

Hivi sasa Mrema hana matarajio ya kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa katika utawala wa nchi, badala yake ni kama amenyanyua mikono, akisimamia ukweli anaouamini kwamba ‘Rais John Magufuli anatosha 2020”.

Mwanasiasa huyo aliyevuma sana katika siasa za upinzani kwenye miaka ya mwishoni mwa 1990, bado anaiongoza Tanzania Labour Party (TLP) aliyokabidhiwa na aliyekuwa mtangulizi wake, Leo Lwekamwa.

Hata ulipofanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, wakati huo CUF ikiwa na nguvu kubwa kwa vyama vya upinzani, hoja ya wapinzani kuungana ilizungumzwa pasipo kufikiwa.

Kisha kila chama kikaingia kwenye uchaguzi na kama ilivyotarajiwa, Rais (mstaafu) Mkapa akaongoza kwa kura 5,863,201 (sawa la asilimia 71.74) akifuatiwa na Profesa Lipumba wa CUF aliyepata kura 1,329,077 (asilimia 16.26 na Mrema akaambulia kura 637,077.

Mwaka 2005, mambo yalibadilika katika kuwania nafasi hiyo ambapo Chadema ambayo mwaka 1995 na 2000 haikumsimamisha mgombea ubunge, ilimteua Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kuisaka Ikulu dhidi ya aliyekuwa mgombea kupitia CCM, Jakaya Kikwete.

Matokeo ya uchaguzi huo ulioguswa pia na minong’ono ya wapinzani kuunganisha nguvu zao, yalimpa ushindi Kikwete aliyepata kura 9,123,952 (sawa na asilimia 80.28) akifuatiwa na Profesa Lipumba (CUF) - kura 1,327,125 sawa na asilimia 11.68, Freeman Mbowe (Chadema) - kura 668,756 sawa na asilimia 5.88 na Mrema (TLP) kura kura 84,901 sawa na asilimia 0.75.

Mwaka 2010, kama ilivyokuwa kwa uchaguzi mkuu uliopita, vyama kadhaa vya upinzani vikashiriki mazungumzo ya kuunda muungano usio rasmi, lakini hakuwezekana na badala yake Chadema ikaingia ikiwa na nguvu kubwa hasa baada ya kumsimamisha aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk Wilbroad Slaa.

Kikwete wa CCM alishinda kwa kupata kura 5,276,827 - sawa na asilimia 61.17, akifuatiwa na Dk Wilbrod Slaa (Chadema) kura milioni 2.2 sawa na asilimia 26.34 na Profesa Lipumba wa CUF kura 695,668, sawa na asilimia nane. Wagombea wengine walipata chini ya hapo.

Nia ya kuwapo muungano wa wapinzani ikatimia mwaka 2015. Vyama vya upinzani vikisukumwa na kasoro walizozibaini kwenye Bunge la Katiba, wakajikuta wanasimama pamoja na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika uchaguzi huo, Rais mstaafu Kikwete alikuwa anamaliza muda wake wa utawala na hivyo, nchi ilikuwa inaelekea kumpata rais mpya wa awamu wa tano.

CCM ilidaiwa iligawanyika kimtazamo kama ilivyo kwa chama tawala katika nchi yoyote ambapo rais aliyepo anaondoka madarakani.

Ni mgawanyiko uliotafsiriwa kuwa mkubwa kutokea ndani ya CCM tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, ukishuhudia waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakihamia Chadema.

Katika kuhama huko, Lowassa aliyekuwa ameimarisha kambi yake ndani ya CCM, alipewa fursa ya kuwania urais kupitia Chadema, akiungwa mkono na Ukawa. Hata hivyo, pamoja na kampeni zake kusheheni umati mkubwa watu, alishindwa na CCM, Rais John Magufuli.

Katika Uchaguzi Mkuu huo wa 2015 ambao upinzani ulionyesha kupata nguvu zaidi kwa mgombea urais wake, Lowassa alipata kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97, akiwa nyuma ya mshindi, Rais Magufuli wa CCM aliyepata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46

Said Salim ni mchambuzi wa masuala ya siasa akiwa Unguja- Zanzibar anaiambia Sauti ya Ujerumani -DW kuwa msingi wa muungano wa vyama wakati wa uchaguzi mkuu una lengo jema la kufanikisha kuziondoa madarakani serikali zilizoshindwa kuwajibika ipasavyo kwa umma.

Hata hivyo, Salim anasema kwa hali inayojitokeza hususani Tanzania, muungano wa wapinzani unakuwa mfano wa kile alichokiita “mchezo wa kitoto” ulioghubikwa na maslahi binafsi. Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba vyama vya upinzani vinachelewa kuunganisha masuala yanapaswa kuwa katika umoja wao, badala yake kuibuka muda mfupi inapokaribia uchaguzi mkuu.

“Wanapokaribia kipindi cha uchaguzi ndipo wanapoibuka na kwa sababu hawana mambo ya msingi ya muda mrefu yanayowaunganisha, utawakuta wanagawanyika na kuendelea kuwakatisha watu tamaa,” anasema.

Mchambuzi huyo anahoji ikiwa wapinzani katika kuungana kwao, wamekuwa na nia ya dhati ama ni matokeo ya kutaka kukidhi ‘njaa’ ambayo hata hivyo hakuifafanua.

Anasema manufaa ya muungano wa wapinzani na uwezekano wa kufikia lengo la kuwatoa watawala madarakani, litafanikiwa ikiwa wanasiasa wataweka kando ubinafsi na kushughulikia masuala yenye tija kwa umma.

Anasema pamoja na changamoto zinazowakabili, muungano wa wapinzani umeonyesha mafanikio katika nchi kadhaa za Afrika ikiwamo Tanzania.

Hata hivyo, anasema katika hali inayoonekana kukosekana umakini wa kutosha, tayari Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amekaririwa akilalamika kuwa Chadema haikutekeleza makubaliano yakiwamo kuvigawia ruzuku vyama vilivyounda Ukawa.

Inavyoonekana muungano wa wapinzani nchini hauna tija sana kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika, kutokana na uimara wa CCM iliyojikita katika eneo kubwa la nchi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa wa nchini Kenya, Profesa Hermani Manyora, anasema hatua ya vyama vingi kuungana hakutokani na kuwa na itikadi na falsafa zinazofanana, bali wanachokitaka ni kutwaa uongozi.

Profesa Manyora anasema kutokana na hali hiyo, vyama hivyo vimejikuta vikishindwa kufikia malengo ya kupata ushindi ama kusambaratika mapema kwa vile vinavyofanikiwa kuingia Ikulu.

Anatoa mfano wa uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 1992 ambapo wapinzani waliungana kupitia FORD vikatawanyika na Rais wa wakati huo, Daniel Moi (marehemu) akashinda.

Pia anasema baada ya muda wapinzani waliungana tena nchini humo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002, sababu kubwa ikiwa ni kupinga hatua ya aliyekuwa Rais wa Kenya, Moi kumchagua Uhuru Kenyatta kuwania urais kupitia chama cha KANU.

Anasema kilichowaunganisha wapinzani hao wakiwamo waliotoka katika KANU haikuwa itikadi ama falsafa zinazofanana, bali hasira zao dhidi ya hatua ya Moi kumteua Kenyatta.

Hata hivyo, Profesa Manyora anasema muungano wa vyama vya upinzani una manufaa kwa nchi za Afrika hasa zile zinazoongozwa na serikali zilizokithiri kwa ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live