Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ubakaji, ulawiti janga ukatili kwa watoto

Ubakajiiii Ubakaji, ulawiti janga ukatili kwa watoto

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Zaidi ya watoto watatu kati ya watano wenye umri wa chini ya miaka tisa walioripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono kwenye Kituo Jumuishi cha Manusura wa Ukatili wa Kijinsia, ni watoto wa kike.

Kituo hicho kilichopo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kilichozinduliwa Januari 27, mwaka huu kinajumuisha huduma za saikolojia, ustawi wa jamii, matibabu, polisi na kisheria.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa hospitali hiyo, Elvira Mutagwaba alisema wamekuwa wakipokea watoto wengi wenye umri wa chini ya miaka tisa ambao hufanyiwa vitendo hivyo na jamii.

“Kundi hilo la watoto linaongoza kwa kufanyiwa ukatili kati ya watu 10 wanaofanyiwa vitendo vya ukatili saba wanakuwa na umri wa kati ya miaka 0 hadi tisa huku asilimia 60 wakiwa ni wasichana ambao hubakwa au hulawitiwa,”alisema Elvira.

Hata hivyo, alisema lipo kundi jingine la watoto wa shule wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 16 ambao wengi wao wanafanya vitendo hivyo kama mchezo unaojulikana kwa jina la “kubambiana”.

Kuhusu watuhumiwa, Elvira alisema watuhumiwa wengi wa vitendo hivyo, ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 25 na hao ni madereva bodaboda, ndugu, vijana wa mitaani na wasiojulikana katika maeneo wanayotoka watoto hao.

“Tunapokea kesi zinazofanywa na baba, baba wadogo, wajomba. Kesi za ndugu zimekuwa changamoto sana kwanza hadi manusura afikishwe katika kituo chetu unakuta ni siku ya tatu ama ya nne tangu afanyiwe vitendo hivyo,”alisema.

Alisema hali hiyo, inafanya manusura kuchelewa kupata huduma ambazo wakati mwingine zinahitajika kutolewa kabla ya saa 72 tangu kufanyiwa vitendo hivyo.

Elvira alisema ucheleweshaji huo unatokana na ndugu kutafuta suluhu ya kulimaliza jambo hilo nyumbani, huku changamoto nyingine ikiwa kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.

Maeneo hatari kwa watoto

Alisema watoto wenye umri wa kati ya miaka 0 hadi tisa mara nyingi hufanyiwa vitendo hivyo katika maeneo karibu na nyumbani kwao.

“Kwa hiyo huwa wanafanyiwa kwenye mapagale na vichakani unakuta mtu anamuita mtoto njoo uchukue pipi anampeleka. Na pengine ni nyumbani kwao kwasababu wengi wao huwa ni ndugu,”alisema.

Elvira alisema manusura wa kati ya miaka 10 hadi 19, wanafanyiana katika vyoo vya shule, vichaka na mapagale wanapotoka shuleni.

Lifti zatumika kuwalaghai

“Ile mtu anasema twende nikusogeze jua kali. Na wengine wanafahamu hata ratiba za mabinti na hivyo wanawachukua asubuhi wanawapeleka shule na jioni pia wanakuwa wamekubaliana watakapokutana ili amrudishe nyumbani,” alisema Elvira huku akieleza kuwa watoto miaka 10 hadi 19 wengi huathiriwa.

Alisema watoto wa chini ya miaka tisa, wanashawishiwa na pipi, biskuti, penseli na fedha ambazo zinaanzia Sh200 hadi Sh2,000.

Aliishauri jamii kushirikiana na Serikali kutokomeza vitendo vya ukatili na wazazi ama walezi wawafuatilie watoto wao ili waweze kugundua viashiria vya hatari kwa watoto wao na kuzuia.

Madhara wanayoyapata

Daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Albert Chota alisema waliofanyiwa ukatili wa ngono wanapata maumivu ya mwili yanyotokana na sehemu zao za via vya uzazi kuwa ndogo.

Alisema ikiwa ubakaji ama ulawiti ni wa kutumia nguvu wapo watoto wengine huwekewa vitambaa mdomoni kuzibwa, ili wasipige kelele na hivyo huweza hata kusababisha vifo.

Kingine ni kusababishiwa magonjwa ya ngono (STDs) ikiwemo Ukimwi na kwa wale wanaolawitiwa wanashindwa kuzuia haja kubwa kutoka.

“Wazazi wengi wanakwambia kuwa mtoto wangu anashindwa kujizuia haja kubwa, inakuwa mara kwa mara anajichafua. Anakuwa na aibu, anakuwa anatoa haja kubwa mara kwa mara na anakuwa hawezi kusema,”alisema.

Dk Chota alisema pia wanapata mfadhaiko wa kifikra ambao humsababishia hata kurudisha nyuma maendeleo yake ya darasani.

“Hawezi kumwambia mtu yeyote alivyofanyiwa, inaleta sonono hawezi kufanya vizuri kabisa kwenye masomo yake. Anaweka hasira na wakati mwingine anakuwa victim (mwathirika) sasa anajenga mazoea. Na inapofika umri wa kuingia katika uhusiano inawafanya wengine kubaki katika ndoa za jinsia moja,”alisema.

Dk Chota alisema kuwa yapo matibabu kwa mtoto aliyeharibiwa haja kubwa na akaweza kurudi katika hali yake ya kawaida.

Mwanasakolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Erasto Kano alisema watoto wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia, wakiwa wakubwa wanaweza kuwafanyia wenzao kwa sababu wanadhani ni mambo ya kawaida.

“Nyingine inaweza kumfanya mtoto kukata tamaa kwamba hakuna mahali ambapo anaweza kusaidiwa tena katika maisha yake. Pia inatengeneza ubaya kama binti amefanyiwa ukatili na mwanaume anatengeneza generalization (ujumla) kuwa wanaume wote ni katili na wabaya, atakuwa na wasiwasi, hofu, kujitenga na kutojiamini ,”alisema.

Mbinu kuzuia ukatili

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki), Janeth Mawinza alisema ili kukomesha hilo kunahitajika kujenga stadi za malezi kwa wazazi ili waweze kuwa na uelewa.

Janeth alitaka pia wazazi kuwasikiliza watoto wao na kwamba wazazi wengi hawataki kuwapa fursa watoto wao kujieleza na wao kuwasikiliza ili kujua kama wanakabiliana na viashiria vyovyote vya ukatil.

Alitaka pia adhabu stahiki kuchukuliwa kwa watoto waliotenda vitendo hivyo, ili kuwaogopesha wengine.

Sheria ya Makosa ya Kujamiana (SOSPA), inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela ama maisha kwa mtu aliyekutwa na makosa ya ubakaji au ulawiti.

Janeth alisema watu wengi wamekuwa hawaogopi sasa hivi , kwa kuwa watuhumiwa wengi wa ubakaji na ulawiti, wamekuwa wakiachiwa bila kuadhibiwa.

Vituo jumuishi ni msaada

Mchambuzi wa masuala ya jinsia kutoka Shirika la Engender Health, Dk Katanta Simwanza alisema uwepo wa vituo jumuishi kwa kila mkoa na wilaya, ndio mapendekezo ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwa).

Alisema uanzishwaji wa vituo hivyo utaondoa urasimu na kuondoa fikra ya kudhalilishwa kwa manusura wa ukatili wa kijinsia kutembea maeneo tofauti kutafuta huduma za polisi, kisheria na kiafya.

“Sababu ya pili ya pendekezo la kuanzishwa kwa vituo hivyo ni baadhi ya huduma kuwa na time frame (muda maalum) wa kupatiwa huduma, nyingine zinatakiwa ndani ya saa 72 awe amepata matibabu. Mambo kama kuzuia Ukimwi, mimba magonjwa ya ngono intervention inatakiwa ifanyike haraka sana. Na ili zifanyike wadau wote wanahitajika,”alisema.

Usuli

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 jumla ya manusura wa ukatili wa kijinsia 194,368 walifika vituo vya kutolea huduma za afya ikilinganishwa na 164,209 mwaka 2021/ 2022.

Katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, asilimia saba ya wahanga wa ukatili walikua ni watoto, kati yao, 13,130 wa jinsi ya kike na 836 jinsi ya kiume.

Mikoa 10 iliyoongoza ni pamoja na Dar es salaam (17,774), Shinyanga (11,986), Geita (11,210), Tabora (10,205), Mara (10,020), Mwanza (9,730), Kagera (8,627), Kilimanjaro (7,006), Kigoma (6,951) na Arusha (6,066).

Columnist: mwanachidigital