Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Yanga wasijitoe kwenye reli ya ubingwa wa ligi kuu

Yanga+prisons+pic UCHAMBUZI: Yanga wasijitoe kwenye reli ya ubingwa wa ligi kuu

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

YANGA imefanya mabadiliko ya benchi lakenla ufundi mara mbili kabla hata msimu haujaisha baada ya kumtupia virago kocha Cedrick Kaze na kwa sasa timu hiyo ipo chini ya kaimu kocha, Juma Mwambusi.

Kabla ya Kaze, timu hiyo ilikuwa chini ya kocha Zlatko Krmpotic ambaye naye aliachishwa kazi baada ya kuitumikia kwa muda usiozidi miezi mitano tangu alipojiunga nayo.

Zlatko aliondolewa huku timu hiyo ikiwa inaongoza msimamo wa ligi ikiwa haijapoteza mechi yoyote, ikipata ushindi katika michezo minne na kutoka sare moja.

Sababu kubwa iliyopelekea Yanga iachane na Zlatko licha ya kwamba ilikuwa haijapoteza mchezo na inaongoza msimamo wa ligi ilikuwa ni staili ya kiuchezaji ya timu ambayo haikuwa inafurahisha wengine ndaninya klabu hiyo ambayo ilikuwa ni ya kujilinda kwa muda mrefu hata pale ilipokuwa inakutana na timu za daraja la wastani au la chini yake.

Baada ya Zlatko akaletwa Kaze ambaye wakati anawasili, kulikuwa na matumaini makubwa kwa Wanayanga kuwa sio tu atawafanya wafanye vizuri katika mashindano wanayoshiriki bali pia kikosi chao kucheza sok maridadi na la kuvutia hasa kutokana na kocha huyo kuwahi kufanya kazi katika kituo cha vijana cha klabu ya Barcelona ya Hispania.

Lakini pamoja na matumaini hayo kwa Kaze, naye ameshindwa kutimiza hata miezi mitano baada ya kuonyeshwa mlango wa kutokea licha ya kikosi chake kuongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 50.

Related Kagere avunja ukimya SimbaNi wazi kwamba matokeo ya mechi mbili za Ligi Kuu kabla haijasimama ambayo Yanga iliyapata dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania yalichangia kwa kiasi kikubwa kuushawishi uongozi wa Yanga kumtimua Kaze.

Kitendo cha kupoteza mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu baada ya kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union lakini pia sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania ni kama kilikoleza petroli kwenye moto wa kumchoma Kaze kwani kabla ya mechi hizo tayari kelele zilishaanza kupigwa na mashabiki na baadhi ya wadau wa timu hiyo wakidai hawafurahishwi na namna timu yao inavyocheza.

Makocha hao wote wawili waliotangulia ndani ya Yanga msimu, sababu hasa iliyowaondoa ni timu kutocheza soka la kuvutia kwenye mechi zake hivyo Wanayanga wenyewe wanaona kama ni jambo ambalo hawastahili.

Mashabiki wengi wa Yanga wanaamini kwamba timu yao inastahili kucheza soka safi na la kuvutia kama lile linalochezwa na watani wao wa jadi Simba na pamoja na matokeo mazuri wanayoyapata wanaona kama bado wanahitajika kupata kitu kikubwa zaidi ya hicho.

Sio kosa kwa mashabiki wa Yanga kutaka kuona timu yao inacheza soka la kuvutia lakini nyakati ambazo wanataka kuona hilo linatokea sio sahihi kutokana na presha na ushindani wa ubingwa uliopo kati yake na Simba na Azam.

Mabadiliko hayo ya benchi la ufundi ambayo timu inayafanya huku msimu ukiwa unaendelea yameonyesha kuwa na athari kubwa kwa timu huku faida zikiwa chache.

Athari ya kwanza ni wachezaji kulazimika kuanza kuzoea upya mbinu na falsafa ya kocha mpya jambo ambalo mara nyingi huchukua muda mrefu na kuathiri mwenendo wa timu katika ligi.

Lakini pia kocha mpya anaweza kufanya mabadiliko ya kikosi chake na kuwafanya baadhi ya wachezaji ambao tayari walishaanza kuzoeana kutopata nafasi ya kucheza na kupanga wale ambao hawakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza jambo linaloweza kuwafanya wahitaji muda mpya wa kuzoeana ndani ya uwanja.

Wanayanga wanapaswa kufahamu kuwa kwa sasa itajio la ubingwa ni jambo kubwa zaidi kwao kuliko timu kucheza vizuri kama wanavyotaka huku ikiwa haijapata hayo maandalizi ya kucheza soka la kuvutia.

Kikosi chao kimekuwa kikibadilika mara kwa mara na wachezaji wanalazimika kuanza upya kuzoeana pamoja na kuzoea na kushika mbinu na falsafa za makocha kila wakati.

Wanapaswa kushukuru kwamba pamoja na kutocheza vizuri, bado timu ipo kwenye ushindani wa ubingwa na bado nafasi ya kutwaa taji bado wanayo hivyo wanapaswa akili yao waielekeze katika kusaka ubingwa.

Tamaa ya kulazimisha kucheza vizuri itakuwa inasababisha kila kukicha watimue makocha na kuiathiri timu katika malengo makubwa ya msimu na kuwanufaisha wapinzani wao.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz